Usitegemee muujiza wowote kama utaendelea kubaki ulivyo
“Kitu kitaendelea kubaki katika hali yake ya utulivu kama hakutakuwa na nguvu yoyote kutoka nje itakayokifikia” Kanuni ya kwanza ya Newton ya mwendo.
Jiwe lililoko juu ya ardhi litaendelea kubakia hapo hata bila ya kutikisika kama hakuna nguvu yoyote kutoka nje itakayolifikia. Kadhalika mguu wako hautasogea popote kama hakuna nguvu yoyote itakayowekwa kwenye mguu huo.
Ndivyo ilivyo katika maisha yako, licha ya kuwa na hazina kubwa ya uwezo ndani yako, hakuna muujiza wowote utakaotokea maishani mwako kama hutachukua hatua za kuuamsha uwezo huo. Hakuna mtu asiyependa mafanikio makubwa maishani mwake. Pia hakuna mtu asiye na uwezo wa kufanya miujiza katika maisha yake.
Ndugu! Umekuwa ukitamani upate mafanikio makubwa maishani mwako. Umekuwa ukijiuliza kila siku ni kwa namna gani utaweza kupata mafanikio hayo? Ni habari njema kuwa nguvu ya kupata mafanikio hayo tayari ipo ndani yako tangu kuzaliwa. Lakini kwa sababu haijaamsha imeendelea kubaki katika hali ya utulivu, na ndiyo maana huoni ukitenda maajabu yoyote.
Umekuwa ukipata matokeo madogo yasiyokuridhisha na kukufanya kuwa mtu wa kawaida. Hayo sio matokeo unayostahili bali umeendelea kuyapata hayo kwa sababu ya kutokuwa na vichocheo vya kumasha nguvu yako halisi ya kufanya mambo makubwa.
Ili uanze kufanya mambo makubwa maishani mwako huna budi kuanza kuuamsha uwezo wako sasa. Kwanza amini kuwa una uwezo mkubwa ndani yako wa kufanya mambo makubwa na ya kushangaza dunia tofauti na matokeo madogo madogo ambayo umekuwa ukiyapata. Uwezo huo tayari upo ndani yako. Hivyo anza kwa kubadili taswira ndani ya fikra zako.
Hatua nyingine ya kuanza kuuamsha uwezo wako ni kutengeneza ndoto yako kubwa na kuanza kuiishi. Hii ni tofauti na ndoto za usiku ambazo unaota ukiwa umelala ukiamuka unaachana nazo au inachukua muda mfupi tu kisha inapotea. Bali inakuwa ni picha kamili na tena kubwa ya nini unataka ukikamilishe kabla hujafa. Hii ni picha ambayo itakupa mafanikio makubwa na kuacha alama kubwa hapa duniani na kukumbukwa hata baada ya wewe kufa.
Usiache uwezo wako uendelee kulala kama jiwe juu ya ardhi kwani uwezo huo ni haki yako na ni wa kipekee. Usipoutumia uwezo huo utakufa nao kwani hakuna mtu mwingine wa kuutumia kwa niaba. Weka malengo makubwa leo ya kuiishi ndoto yako kikamilifu. Malengo hayo yatakulazimisha kuamasha hazina kubwa ya uwezo wako iliyolala tu ndani yako. Lengo gani utaanza nalo na kuendelea nalo mapaka upate matokeo bila kujali chanagamoto unazoweza kukutana nazo?
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.
Mawasiliano:
Simu: 0752 206 899/0714 301 952