Tumia mbegu iliyoko ndani yako kutengeneza msitu
Watu wawili wanaweza wakawa na maono mawili tofauti kuhusu mbegu ya mti iliyojuu ya ardhi. Mmoja anaweza kuona ukuni kwenye mbegu hiyo. Huyu atakuwa ameamini kuwa mbegu hiyo ikipandwa itaota na baadaye kukua kuwa mti kisha kukatwa na kutumika kama ukuni. Mwingine akiiona mbegu hiyo ataona msitu ndani yake. Huyu atakuwa ameamini kuwa mbegu hiyo inaweza kupandwa ikaota na kukua kuwa mti. Mti huo utatoa mbegu nyingine zikapandwa na kupata miti mingine nayo ikazalisha mbegu nyingine na kuwa miti mingine mingi na hatimaye msitu. Wote wapo sahihi kutokana na maono yao.
Ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya kila siku, kila mtu ana mbegu ndani yake. Bila kujali aina ya mbegu uliyonayo, ilitarajiwa uzae msitu wa matokeo kutoka kwenye mbegu hiyo. Uwezo huo ulionao ndani unaanza kama mbegu. Kama ilivyo kwenye mbegu ya mti ndiyo ilivyo kwenye uwezo wa mtu. Unatarajiwa ukipata matokeo ya kwanza yatumike kama mbegu kwa matokeo mengine. Kwenye kila unachokifanya inakupasa ukifanye kukuza kipaji/uwezo ulionao ili uweze kukua na kuzaa msitu wa mafaniko.
Lakini hali ni tofauti kwa watu wengi, kwani wameishia kuwa mti wa kuni na sio msitu katika matumizi ya uwezo wao. Watu wanatumia kiwango kidogo sana cha uwezo wao.
Mbegu ya uwezo uliyonayo unaweza ukaiotesha, kuikuza na kisha kuzalisha msitu wa mafanikio.
Mafanikio madogo uliyonayo ni kwa sababu ya kuona ukuni kwenye uwezo ulio nao na sio msitu. Habari njema ni kuwa mbegu ya kutengeneza msitu wa mafanikio yako tayari ipo ndani yako. Mbegu hiyo ni uwezo uliowekwa ndani yako tangu kuzaliwa kwako. Ukifanikiwa kuuamsha uwezo huo unaanza kutengeneza msitu kwenye mbegu hiyo.
Uwezo ulionao ambao umebaki umelala ndani yako unawiana na jambo ambalo unapenda kulifanya hivyo ili uweze kujenga msitu wa mafanikio huna budi kuchagua jambo moja ambalo utaliwekea kazi na kupata matokeo. Lakini kwenye hilo jambo weka maono ya kupata mafanikio makubwa kwa muda maalumu.
Mbegu moja ikiota huzalisha mbegu nyingine kwenye mti wake ambazo nazo zikipandwa zinatoa mbegu nyingine. Hivyo na wewe hakikisha kupitia mafanikio madogo unayoyapata unaamsha uwezo wako kuzalisha na kupata mafanikio zaidi. Ukikamilisha lengo moja, basi panga lengo jingine ambalo ni kubwa zaidi ya la kwanza. Kwa kuendelea na mfumo huo utafikia mafanikio makubwa zaidi. Kamwe usiridhike na kile ulichokipata bali muda wote kitumie kama mbegu.
Usiiache mbegu ya uwezo wako ikaendelea kulala tu ndani yako, bali iamsha izae msitu. Kaa chini na tafakari huku ukijiuliza una mbegu gani ndani yako? Kitu gani unakipenda kukifanya? Kisha anza au endelea kufanya jambo hilo kupata mafanikio, na ukipata mafanikio hayo amsha uwezo zaidi ili kupata mafanikio makubwa zaidi ya yale ya awali. Hivyo ndivyo unavyoweza kutengeneza msitu wa mafanikio kwa kutumia mbegu ya uwezo uliyonayo ndani yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.
Mawasiliano:
Simu: 0752 206 899/0714 301 952