Mtambue Leo Aliyekupangia Kiasi Cha Mafanikio Unayoyapata


Categories :

Je unaridhika na kiasi cha mafanikio unayoyapata? Je unajua ni nani aliyekupangia kiasi hicho? Je umekuwa ukimlaumu nani kwa mafanikio kidogo unayoyapata?

Inawezekana na wewe ni miongoni mwa watu  ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta mtu au watu wa kuwalaumu na kuwalalamikia kwa mafanikio madogo waliyoendelea kuyapata. Umeilaumu serikali, wazazi au jamii kwa kuona ndiyo chanzo cha mafanikio hayo usiyoridhishwa nayo.

Naomba nikupe pole kuwa wale uliokuwa unawafikiria na kuwalaumu kwa kupimia kiasi kidogo cha mafanikio yako sio wao. Kuna mhusika mwingine wa kweli usiyemfahamu. Ndiyo maana licha ya kuwalaumu, maisha yako yameendelea kubaki vilevile. Najua una hamu kubwa ya kumfahamu mhusika huyo. Nasikitika kukuambia kuwa mhusika huyo ni WEWE. Ndiyo WEWE MWENYEWE. Usishangae! 

Kupitia akili yako umekuwa ukijipangia kiasi cha mafanikio ambayo unaweza kuyapata. Inawezekana ulikuwa unafanya hivyo bila kujua, hivyo leo nitakujuza ili ufahamu ni kwa namna gani ulikuwa unajipunja na ili ufanye mabadiliko kufikia ukuu wako.

Kiasi cha mafanikio mtu anaweza kupata ni sawa na eneo ambalo mbuzi aliyefungwa kamba anaweza anaweza kula nyasi. Mbuzi huyohawezi kula nyasi zaidi ya urefu wa kamba yake. Ndiyo ilivyo kwako, huwezi kupata mafanikio zaidi ya kiasi kile ambacho akili yako inaamini inaweza kukipata. Ukiona mtu ana mafanikio makubwa ambayo akili yako inayashangaa, ujue akili ya mtu huyo haishangai kiasi cha mafanikio hayo bali inaamini na kuona inastahili.

Umekuwa ukijipangia kiasi hicho kidogo cha mafanikio kwa  kujitathimini akilini mwako na kuamini kuwa wewe ni wa daraja fulani la mafanikio. Akili yako imeweka mpaka wa kiasi gani cha fedha unaweza kukimiliki. Ndiyo maana baada ya wewe kujiona ni mtu wa milioni moja, ulipopata milioni mbili tu akili yako ilichanganyikiwa na kupanga bajeti zisizo na maana kuitumia fedha hiyo ya ziada. Ilipobaki milioni akili ilianza kutulia. Pia iliposhuka mpaka laki moja, hapo akili ilianza kuchangamka na kuhisi imepungukiwa. Ulitafuta namna ya kuongeza kipato chako kirudi tena kwenye milioni moja au karibu na kiasi hicho.

Hivi ndivyo WEWE umekuwa ukijipangia kiasi cha mafanikio.  Hakuna mtu mwingine anayeweza kurekebisha kiasi hicho, isipokuwa wewe mwenyewe. Inakupasa urudi kwenye akili yako utoe kwanza ukomo uliojiwekea. Kabla hajachukua hatua yoyote iambie akili yako na uamini kuwa unaweza kupata mafanikio makubwa yoyote unayoyatamani. Kama ulijiwekea ukomo wa milioni moja basi iambie na uiaminishe akili yako kuwa wewe ni bilionea. Ukitoa mipaka hiyo na kuamini, ndipo unapoweza kuchukua hatua za kupata mafanikio hayo bila kukuta tamaa. Pia hata utakapofikia kiasi hicho (bilioni) akili yako itatulia kwani itajua kuwa ni kiasi unachostahili.

Njia kuu ya wewe kuvunja mipaka ya kiwango cha mafanikio madogo uliyoishi nayo kwa muda mrefu ni kutengeneza ndoto yako. Hii ni picha ya jambo au mambo makubwa ambayo mtu anatamani ayafikie katika maisha yake. Ni picha ambayo utakuwa unaiona wewe mwenyewe tu, na ukimusimulia mtu mwingine anaweza asikuelewe na kutokukuamini pia. Unapokuwa na picha hii thabiti na kuanza kuiwekea mipango ya kuitimiza ndipo unapoivunja ile mipaka ambayo akili yako ilijijengea. Kwa kufanya hivyo taratibu utaanza kutoka kwenye viwango vya sasa vya maisha ya kawaida na kufikia maisha ya mafanikio makubwa unayostahili.

Tafakari jinsi ulivyoishi maisha ya kawaida ambayo huridhiki nayo kwa muda mrefu. Anza leo kutengeneza ndoto ya maisha yako na weka mipango ya kuanza kuchukua hatua mara moja. Kumbuka unaweza kupata chochote ambacho akili yako itakipanga na kukiamini, hivyo usijipunje.

Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI ni mwongozo mzuri wa namna ya kutengeneza ndoto yako kamili na kuiishi kikamilifu kufikia mafanikio makubwa.  Pata nakala yako sasa kwa kupiga simu 0752206899 ili uanze kutengeneza ndoto yako mara moja.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *