Misuli Huimarika Kwa Maumivu


Categories :

Tofali bichi lililotengeneza kwa udongo huanza kuimarika na kuvutia macho baada ya kupita na kuvumilia kwenye moto wa tanuru. Kadhalika dhahabu huonekana safi na kung’aa baada ya kupitishwa kwenye moto mkali. Mtu anayefanya mazoezi makali, misuli yake huonekana imara baada ya kuvumilia maumivu makali wakati wa mazoezi.

Misuli, tofali bichi na dhahabu chafu vyote huonekana dhaifu sana kabla ya kupita hatua za awali na muhimu. Tofali bichi, huwa dhaifu sana, likikanyagwa au kudondoka hata kwa kimo kifupi tu huishia kuvunjika na kusambaratika. Lakini tofali hilo hilo likipitishwa kwenye moto mkali na kuvumilia maumivu hutoka likiwa imara sana na kuimarisha nyumba litakayojengewa. Kadhalika dhahabu huonekana haina dhamani kabla ya kupata maumivu makali ya moto, lakini baada ya hapo mng’ao wake huongezeka na pia kuwa na thamani kubwa.

Ndugu, kuna mafanikio unayatamani uyafikie maishani mwako, ni kweli mafanikio hayo ni yako na una haki ya kuyapata. Yamkini umeshashuhudia mtu mwingine akiyaishi mafanikio makubwa ambayo unatamani yangekuwa kwako. Una nafasi kubwa ya kupata ukishajua kile kinachotangulia kabla ya hatua hiyo unayotamani kuifikia na kuwa tayari kuipitia hatua hiyo kwa uaminifu.

Ili uweze kuyapata mafanikio unayoyatamani huna budi kuweka mipango thabiti ya kukufikisha unakotaka kufika.  Lakini kuna uhakika wa jambo moja kuwa kupata mafanikio makubwa na ya kudumu inawezekana lakini  haitakuwa kazi nyepesi. Ni kazi ambayo itaambatana na magumu mengi, milima na mabonde, ambapo ili uyafikie mafanikio hayo na kudumu nayo inakupasa uwe imara kweli kweli.

Kama ilivyo kwenye misuli inavyoimarika kwa maumivu makali na hivyo kuhitaji uvumilivu wakati wa kuijenga,  ndivyo ilivyo kwenye kujenga uimara wa kupata mafanikio makubwa. kuna changamoto utakazopitia utakapokuwa unajenga mafanikio yako makubwa.  Kupitia changamoto kunaweza kutaambatana na maumivu makali sana, kwa mfano kupata hasara kubwa mwanzoni mwa biashara. Katika hatua kama hiyo huhitaji kurudi nyumba badala yake kujifunza na kuona ni kwa namna gani unavumilia, kujifunza na kuendelea na safari. Haya ni maumivu ambayo yatakuimarisha na kuwa bora zaidi.

Uimara unaohitajika kuujenga unaanzia kwenye fikra. Tunafanya mambo na kuwa tulivyo kutokana na yale tunayoyawaza muda mwingi. Fikra imara zitakufanya uwe imara pale mawazo kinzani yatakapokujia na hivyo kubakia na msimamo wako wa kusaka mafanikio makubwa.  Kwa mfano unapopanga kutekeleza ndoto zako ili kufika kule unakokutamani, kuna kauli za kutoka ndani mwako au kwa watu wengine ambazo zitakukatisha tamaa, zikikuambia wewe huwezi kufanya mambo hayo makubwa. Hii ni vita ambayo inakuhitaji kuipinga kila wakati unapofikiwa na mawazo hayo. Unapoendelea kuyapinga mawazo hayo kwa muda mrefu ndipo unapojenga fikra imara zitakayokupeleka kule unakotamani.

Unaowaona wamepata mafanikio makubwa, walilipa ada kubwa ya kukosea mara kwa mara. Walivumilia na kujifunza, na hivyo kuwaimarisha. Hawa ni watu ambao hata wakipata changamoto kubwa kwenye mipango yao tayari wanakuwa na jibu la nini cha kufanya.

Kuna mipango mikubwa ya kufikia mafanikio makubwa uliyoiacha baada ya kupitia changamoto fulani na kuona huwezi kufika mwisho. Napenda kukuambia kuwa, ulikuwa kwenye hatua ya kujiimarisha ambayo ilikulazimu kuvumilia maumivu hayo, kujifunza, kuimarika na kisha kusonga mbele. Una nafasi ya kufufua mipango yako leo na kuendelea pale ulipoishia huku ukijua maumivu utakayopata yatakuimarisha ili kubobea kwenye kile unachofanya na kupata mafanikio makubwa.

Kwenye mipango mikubwa unayoipanga sasa ya kufikia mafanikio makubwa, tambua kuwa kuna gharama za kulipa ili kuyajenga mafanikio hayo. Moja ya gharama hizo ni maumivu utakayokuwa unayapata wakati unajiimarisha. Kama ni biashara tambua kuna uwezekano wa kupata hasara au kutokufanya vizuri na hasa mwanzo. Ukijua haya kabla hujaanza, itakusaidia kutorudi nyumba badala yake kusonga mbele pale yatakapotokea.

Ndugu, kuna nafasi kubwa ya kukutana na maumivu kwenye mambo unayoyafanya sasa au unayotarajia kuyafanya. Maumivu hayo yakija, yachukulie chanya na kamwe usishawishike kurudi nyuma, badala yake tumia kama darasa kujifunza na kubobea ili kupata matokeo makubwa unayoyatamani.

Ili uweze kuzishinda changamoto mbalimbali na kuishi ndoto yako kikamilifu huna budi kuwa na mwongozo imara wa kukusaidia kuvuka magumu utakayokutana nayo. Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI ni mwongozo kamili wa kutengeneza ndoto yako kubwa na kuiishi kikamilifu. Piga simu 0752 206 899 kupata nakala yako leo ili usiendelee kuififisha ndoto yako.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *