Kwa nini uendelee kufanya licha ya kushindwa mara nyingi?
Licha ya kila mtu kutamani kuwa na mafanikio, lakini ni wachache sana wameweza kupata mafanikio makubwa katika maisha yao. Hii inaashiria kuwa safari ya mafanikio siyo rahisi, ina kupasa kuvuka mabonde na milima. Ina changamoto ambazo inabidi uzifanyie kazi ndipo uweze kufika mwisho wenye mafanikio.
Wanaofanikiwa wana tabia ambazo zinawafanya kupata mafanikio makubwa licha ya kupitia changamoto na kushindwa mara nyingi. Tabia moja wapo ni uvumilivu. Hawa huendelea kufanya kitu hata kama hawapati matokeo. Huendelea kuweka nguvu wakiamini watakuja kupata matokeo mbele ya safari.
Wanajua siri ambayo ipo kwenye uvulimivu na hivyo kuiishi. Na mimi leo nitakuibia siri hii ili uweze kutumia katika maisha yako kutafuta mafanikio makubwa. Nitakushirikisha sababu tano za kwa nini huwa wanaendelea kuweka nguvu kwenye vile wanavyofanya licha ya kushindwa mara kadhaa. Sababu hizi zitakupa hamasa ya kuendelea na safari ambayo uliikatia tamaa au kama ndiyo unaanza safari zitakusaidie usirudi nyuma pindi utakapokuwa unashindwa.
Sababu ya kwanza: Kuna ushahidi wa uwezekano. Kwenye mambo wanayofanya wana ushindi kuwa inawezekana. Kama jambo unalolifanya kuna watu walishalifanya, hii inakupa uhakika na wewe kuwa utapata matokeo usipo kata tamaa. Mambo yaliyowezekana yameendana na kanuni za asili za dunia. Kanuni mojawapo ni kisababishi na matokeo. Kwamba kwenye kila matokeo yanayotokea kunakuwa na kisababishi, kwa hiyo kama kuna watu walipata matokeo kwa kisababishi ambacho na wewe unakifanya basi na wewe ni dhahiri utapata matokeo hayo.
Sababu ya pili: Wanaweza kupata majibu yaleyale kwa kutumia njia nyingine. Waliofanikiwa wakishindwa mara ya kwanza hawakati tamaa, badala yake wanaagalia uwezekano wa kufanya jambo hilo kwa namna nyingine na kisha wanapata matokeo kadri wanavyojaribu njia tofauti tofauti. Mara nyingi kila jambo huwa linakuwa na nmna tofauti ya kufanya, hivyo uvumilivu tu ndiyo unaohitajika ili kujaribu kufanya jambo lililoshindikana mara ya kwanza kwa njia nyingine.
Sababu ya tatu: Wanafaulu mtihani wa dunia. Dunia hujaribu watua wanaotafuta vitu kama kweli wana nia ya dhati. Waliofanikiwa, licha ya kushindwa mara kadhaa huendelea kuweka nguvu wakitambua kuwa dunia inawapima kama kweli wana nia ya dhati. Ukishindwa usiache, tambua dunia inakujaribu, hivyo endelea ili kushinda jaribio la dunia.
Sababu ya nne: Bado wapo hai. Sababu moja kuu ya kumfanya mtu asiendele kufanya baada ya kushindwa ni kifo. Waliofanikiwa wanaamni kuwa kama wapo hai ina maana wana nafasi ya kufanya tena yale waliyoshindwa mpaka wafaulu. Hivyo ndugu kwa sababu bado upo hai endelea kufanya licha ya kushindwa.
Sababu ya tano: Tiba ya muda. Ndugu kama mbegu ni nzima na imepandwa kwenye mazingira mazuri kwa mbegu kuota, basi ni suala la muda tu mbegu hiyo itaota. Waliofanikiwa hujitathimini kuona kama wapo kwenye uelekeo sahihi kwenye yale wanayofanya, wakithibitisha hilo huendelea kuweka juhudi kwenye mipango yao licha ya kushindwa mara nyingi. Katika hili huamini kuwa muda utatibu kushindwa kwao.
Ndugu, umeona sababu hizo tano za kwa nini uendelee kuweka juhudi kwenye lile unalofanya licha ya kushindwa mara kadhaa. Tumia sababu hizi kufufua mipango mizuri uliyoizika baada ya kushindwa mara kadhaa kwani una nafasi ya kufanikiwa katika hiyo. Pia tumia sababu hizi kujiandaa kwa ajili ya mipango mipya unayoanza kuifanyia kazi,ili utakaposhindwa uvumilie na kuendelea kuwaka jitihada mpaka ufanikiwe.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.
Mawasiliano:
Simu: 0752 206 899/0714 301 952
Email: alfred@amshauwezo.co.tz