Kikuze hicho ulichonacho


Categories :

Kama umeisimama na ukanyoosha mkono wako, utagusa kimo fulani kifupi. Lakini ukiweka nguvu kwenye miguu na kuruka juu hata kama ni kidogo tu, mikono yako itagusa juu zaidi ya pale ulipokuwa umegusa hali ukiwa umesimama tu. Ukitafuta ngazi na kutumia kupanda, utafika mbali zaidi na kugusa juu zaidi ya pale ulipokuwa umesimama ardhini au baada ya kuruka.

Hii ni ishara kuwa katika mazingira hayo hayo unaweza kuongeza na  kufikia viwango vya juu zaidi. Watu wamekuwa  wakiishi katika viwango vilevile kwa muda mrefu wakifikiri wamefika mwisho. Licha ya kuwa na bahati ya kuwa na kitu anachokifanya, kwa mfano biashara, lakini ameshindwa kuboresha maisha yake kwa sababu ya kuendelea kuishi viwango vile vile kila siku.

Ni tabia ya asili kitu kuanza kidogo kisha kukua na kuwa kibwa sana. Hata mafanikio makubwa ambayo anayaona kwa watu, yalikuwa madogo kama yako, lakini sasa unayaona makubwa na kushangaza kwa sababu waliweka jitihada za kukuza kilichokuwepo muda huo na kukifanya kikubwa. Kwenye kila kitu unachokifanya kuna nafasi ya kukikuza kikawa kikubwa zaidi. Hivyo badala ya kuanza kufikiria kitu kingine, angalia fursa ya kukikuza kwanza ulicho nacho kwa sababu tayari una sehemu ya kuanzia.

Zifuatazo nai mbinu ambazo unaweza kuzitumia ili kukuza hicho unachokifanya na kupiga hatua kubwa kufikia ukuu wako;

Moja, tengeneza maono. Ili kupata mwamko wa kukuza kile unachokifanya lazima uhakikishe unakuwa na maono nacho. Kama ni biashara lazima utengeneze maono ya biashara yako. Maono ni taswira ambayo unatarajia jambo unalolifanya lifikie. Hii si taswira ya leo au kesho, bali ya muda mrefu ujao. Unataka kuwa nani? Unataka biashara yako ifike wapi? Unataka huduma yake ifike wapi? Mara nyingi maono huwa yanabeba taswira kubwa ya kule unakotaka kufika. Ukiwa na maono kwenye kile unachokifanya, yatakusukuma kukua kila siku na kufikia mafanikio makubwa.

Mbili, ongeza maarifa. Ukuaji wowote wa nje unaanzia ndani. Huwezi kubadilika nje kama ndani bado upo vile vile. Ukuaji wa ndani unahusisha fikra, yaani namna unavyopambanua mambo. Moja ya kitu ambacho kitakusaidia kukua ndani ili uweze kukuza mambo ya nje ni maarifa. Hakikisha unalisha akili yako maarifa sahihi kila siku kupitia kusoma vitabu, makala na kuhudhuria mafundisho mbalimbali yanayoendana na kile unachofanya.

Tatu, Ongeza thamani. Utafanikiwa kukua kama utaweza kuongeza kile wengine wanachofaidika kutokana na kile unachokifanya. Hii inaitwa thamani. Biashara yako haiwezi kukua kama utaendelea kutoa thamani ile ile kila siku. Huduma yako haitakua kama utaendelea kutoa kiwango kile kile kwa watu wale wale. Kwenye kile unachofanya angalia uwezekano wa kuongeza thamani kwa wanufaika; Je unaweza kuongeza kiwango cha uzalishaji na ubora? Je huduma yako inaweza kuwafikia watu wengi zaidi?

Nne, Acha mazoea. Albert Einstein alisema  “Insanity is doing the same thing over and over again and expecting different results.” ikitafsiriwa kuwa wazimu ni kuendelea kufanya kitu kwa namna ile ele huku ukitegemea kupata matokeo tofauti. Watu hufikiri vitu vitajibadilisha vyenyewe. Utamkuta mtu anafanya mambo kama alivyokuwa anafanya mwaka jana, lakini anategemea atapata matokeo tofauti. Kauli ya Einstein ni nzito na ya kuudhi ambayo unaweza kuitumia kuchukua hatua za kukua na kutoka hapo ulipo. Kama mbinu za awali zimefeli basi angalia mbinu nyingine zitakazo kufanikisha badala ya kuendelea kung’ang’ania mbinu ambazo hazikupatii matokeo unayoyataka.

Tano, vumilia. Ukuaji mkubwa huanza pole pole na chukua muda mrefu mpaka kuuona utofauti mkubwa. Kuna kasumba ya watu kutaka mabadiliko makubwa mara moja, ambapo ameweka nguvu leo na kutaka kuona matokeo leo leo. Hapo ndipo uvumilivu unapohitajika. Kama upo kwenye uelekeo sahihi, endelea kuweka nguvu, mbadiliko yataonekana tu.

Ndugu, kitu chochote kisichokua kinakufa, hivyo kuendelea kubaki ulivyo ni kujihakikishia kifo. Kuepuka kifo, hakikisha kila wakati unaongezeka kutoka hapo ulipo kwa kuwa na maono ya kile unachofanya, kuongeza maarifa, kuongeza thamani, kuacha mazoea na kuvumilia.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *