Hangaika Na Kutoa Thamani, Mafanikio Yatakuja Yenyewe Tu


Categories :

Nyuki huwa hahangaiki kujua kama maeneo ya jirani kuna mrina asali ndipo aanze kutengeneza asali, bali yeye muda wote yupo ‘busy’ kutafuta mali ghafi kwa ajili ya kutengeneza asali iliyo tamu sana. Lakini kwa kujua thamani ya asali hiyo, mrinaji huwatafuta nyuki na asali ilipo. Kadhalika ng’ombe huwa hasubiri mpaka mchungaji wake apewe oda ndipo atengeneze maziwa, bali yeye huwa busy kuyatengeneza maziwa na wakati ukifika mchungaji humfuata ng’ombe mwenyewe kuyakamua maziwa.

Nini kipaumbele chako katika maisha yako? Kwenye biashara yako unahangaika na nini kwanza? Je unahangaikia faida ya fedha kubwa kwanza ili ukaiweke benki? Je umeanza na kuhangaika kwanza na biashara yako ikununulie gari? Kwenye mahusiano yako unahangaika na nini? Je upo busy ukiwalazimisha watu wako wa karibu wakupende kwa nguvu?

Licha ya mahangaiko makubwa ambayo umekuwa ukifanya, hujapata mafanikio yoyote au umepata madogo tu. Umejiuliza mara nyingi kwa nini licha ya mahangaiko yote hayo hujapata unachokitaka? Haya yote yametokea kwa sababu umeanza kuangalia maji kama yamechemka kabla ya kuwasha jiko la kuchemshia. Umekosa kile unachokitaka kwa sababu unataka kuvuna kabla hujapanda.

Thamani hutangulia mafanikio. Kipaumbele chako tena cha kwanza katika maisha yako inabidi iwe ni kutengeneza thamani kwanza kabla ya matokeo mengine yoyote. Kipaumbele cha biashara yako lazima kiwe kutoa thamani kwa wateja wako na sio kupata fedha kwa wateja wako na kutengeneza faida. Ukifanikiwa kutengeneza thamani kwa wateja wako, watakuwa radhi kukupa fedha unayoitaka.

Kwenye huduma yoyote ile unayoifanya, kipaumbele chako cha kwanza inabidi kiwe ni kuwapa thamani kubwa unaowahudumia. Vivyo hivyo ukitanguliza kutoa thamani ya upendo kwa wanaokuzunguka, hutahangaika kuwalazimisha wakupende, watakupenda kwa hiari tu.

Tamaa ya watu wengi ni kuwa na mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali, mahusiano, kiuchumi, kiroho, kazi nk. Tamaa hizo zitatimia pale kanuni hii ya thamani kwanza itakapofuatwa, vinginevyo itabaki kuwa tamaa tu. Kwenye kila eneo la maisha yako jiulize ni thamani gani naweza kutoa kwa watu wengine? Kumbe maisha ya mafanikio ni kuwahudumia watu wengine na huku ukirudishiwa mara dufu.

Kiwango cha mafanikio yako kinaendana na thamani unayotoa. Hivyo kama unaona una mafanikio madogo, tambua kuwa na kiwango cha thamani unachokitoa ni kidogo pia. Kama unataka kuongeza kiwango cha mafanikio yako basi anza na kuhangaika na kuongeza thamani unayowapa watu kwenye eneo husika.

Kadri unavyoongeza thamani ndivyo unavyozidi kuwavuta watu wengi zaidi na mafanikio zaidi. Hii ni kwa sababu watu hufuata thamani wanayoweza kuipata kwako na sio kutimiza mahitaji yako. Licha ya nyuki kutopita mitaani na kuwatangazia watu kuwa anatengeneza asali ambacho ni kitu kitamu sana, lakini watu wenyewe huenda porini kuwatafuta nyuki ili waipate asali hiyo. Pia ng’ombe wa maziwa huwa hasubiri mchungaji wake apewe oda kwanza na  watu ndipo aanze kutengeneza maziwa, bali yeye huendelea kutengeneza maziwa hayo na mchungaji wake humfuata mwenyewe akishaona thamani iliyopo kwenye maziwa yake.

Ndugu hangaika kutengeneza asali kwanza watu watakutafuta na wakishaipata asali watakupa unachohitaji. Tengeneza maziwa kwanza watu watakufuata na kukupa oda ya kupata thamani hiyo kila siku na kukulipa kiasi unachohitaji. Tafakari maeneo mbalimbali ya maisha yako ambayo unatamani ufanikiwe zaidi ya ulivyo sasa kisha angalia ni kwa namna gani unaweza ukaongeza thamani mara dufu nawe utarudishiwa mara dufu.

Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI kimeelezea kiundani namna ya kutoa thamani na kupata mafanikio makubwa. Pata nakala yako leo ili usiendelee kuhangaika tena na namna ya kutengeneza thamani kubwa. Kupata kitabu hiki piga simu 0752 206 899.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *