Unataka maziwa! Mwaga kwanza chai ya rangi iliyopo kwenye kikombe chako


Categories :


Kama una kikombe ulichojaza chai ya rangi na ikatokea unataka maziwa, haiwezekani ukatumia kikombe hicho kunywea mziwa. Itakupasa kumwaga kwanza chai iliyopo kwenye kikombe hicho ili upate nafasi ya kumimina maziwa.

Utaratibu huu umekuwa tofauti kwenye maisha ya watu kwani wametaka kuvinywa vyote kwa wakati mmoja kwa kutumia kikombe kilekile. Badala yake wameendelea kukosa maziwa kwa kuendelea kung’ang’ania chai ya rangi kwenye kikombe. Unaweza kushangaa ni wapi ulifanya hivyo! Umefanya hivyo kwa kutaka mabadiliko ya nje yenye sifa ya maziwa wakati ndani yako kikombe bado kimejaa chai ya rangi.

Vitendo unavyovifanya vinavyozalisha matokeo unayoyapata ni matunda ya tabia ulizozijenga tena kwa muda mrefu. Ili uweze kuyabadili matokeo hayo usiyoyapenda huna budi kubadili kwanza tabia zinazozalisha matokeo hayo. Mabadiliko ya kweli yanaanzia ndani na sio nje. Ukitaka kubadili matokeo huna budi kubadili kwanza tabia.

Kama huna furaha katika maisha yako, tambua kuwa kuna tabia ambazo zimevuta huzuni maisha mwako. Je ni kuyaweka mawazo hasi akilini mwako? Au una tabia ya kutomsamehe aliyekukosea na hivyo kuendelea kuyakumbuka maumivu aliyokupa? Je una tabia yakufukua mambo yaliyopita na kuendelea kuumia nayo? Je huna moyo wa shukrani kiasi cha kushindwa kushukuru kwa mafanikio madogo uliyoyapata wakati unasubiri makubwa? Hivyo kama unataka mabadiliko katika kipengele hiki cha mafanikio yako, huna budi kumwaga kwanza tabia hizi ilizitoke kwenye akili yako.

Kama una shida ya kifedha, kipato hakitoshi, unakosa mataji wa kuanzishia biashara tambua kuna tabia ambazo zimesababisha haya yote kutokea. Ili uweze kutoka hapo huna budi kubadili tabia zilizokusogeza hapo na kujenga tabia zitakazokupeleka unakotamani kufika. Je ni tabia ya kutoweka akiba kwenye kila kipato ndiyo iliyokufikisha hapo? Je ni tabia ya kutoongeza thamani kwenye unachofanya kwa sababu unafanya kimazoea? Kutatua changamoto za kifedha huna budi kuanza kujenga tabia mpya katika maeneo mbalimbali ya fedha ikiwa ni pamoja na akiba na thamani.

Warren Beffett amewahi kusema “The chains of habit are too light to be felt until they are too heavy to be broken” ikitafsiriwa kuwa minyororo ya tabia ni myepesi sana kiasi cha kutoihisi mpaka pale itakapokuwa imara sana kiasi chq kutovunjika kirahisi. Tabia ulizonazo sasa umezijenga kwa muda mrefu sana, zimeshakomaa na ni ngumu sana kwa sasa kuvunjika. Ili kuzivunja tabia hizo unahitaji nia ya dhati na kujitoa sana.

Ukianza kuzivunja tabia za zamani, inakuwa sawa na kumwaga chai ya rangi kwenye kikombe na kutengeneza nafasi ya chai ya maziwa. Hivyo wakati unavunja tabia za zamani anza kujenga tabia nyingine mpya na sahihi. Acha tabia ya kutoweka akiba, anza kuweka akiba sasa. Acha tabia ya kutokushukuru hata kwa madogo, anza kushukuru hata kwa mambo madogo.

Kuvunja tabia sio kitu rahisi japo kinawezekana. Tabia inakuwa ni kitu ulichokizoea, kuna ukinzani mkubwa sana utakaokutana nao unapoanza kuvunja tabia uliyoijenga kwa muda mrefu. Unahitaji kuwa na msimamo thabiti ili usirudi nyuma. Anza kidogo kidogo kisha utakuwa imara. Kama Warren Buffett alivyosema hapo juu kuwa unapoanza kutengeneza tabia unaweza usiihisi, hivyo wewe endelea tu kuweka nguvu, usipokata tamaa utakuja kuijenga tabia nzuri imara ambayo itakuwa ngumu kuivunja.

Ndugu ni maeneo gani ya maisha yako hayakuridhishi? Je ni mahusiano? Je ni uchumi au biashara? Au kazi? Kwenye eneo lolote linalokuudhi una kitu kimoja cha kuanza kufanyia kazi nacho ni tabia. Mwaga tabia za zamani kutoka kwenye mfumo wako wa maisha na anza kumimina tabia njema.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *