Usikubali Kuzuiwa Na Vikwazo Hivi Vinne (04) Kwenye Safari Yako Ya Mafanikio.
Maji yanayopita juu ya ardhi huhangaika kutafuta njia ya kupita kila wakati. Ikitokea yamezuiwa kushoto yatahamia kulia. Yakizuiwa kushoto na kufanya yasimame, kuna mengine yatashuka ardhini wakati mengine yakipanda angani kama mvuke.
Safari ya maji inafananishwa na safari yako ya mafanikio. Umeweka mipango mingi iliyo mizuri kwa ajili ya utekelezaji. Lakini kuna uhakika kuwa safari yako ya kufikia mafanikio hayo haitakuwa rahisi kwani kuna vikwazo vingi vitaibuka ukiwa njiani wakati wa kuelekea kwenye mafanikio. Je utafanya nini, utakubali vikwazo hivyo vikuzuzie usifike safari yako au utapambana kama maji yanavyo pambana kutafuta njia? Katika safari ya mafanikio yako umekuwa au utakutana na vikwazo vingi, leo nitakushirikisha baadhi ya vikwazo hivyo na namna ya kuvivuka.
Moja, Fikra zako: Fikra zako ni kikwazo cha kwanza cha safari yako ya mafanikio. Namna unavyofanya vitu inategemea na uwazavyo. Umeziandaaje fikra zako katika kuyatimiza malengo ya kufikia mafanikio yako? Je akili yako inaamini bila shaka yoyote kuwa utayafikia malengo uliyo nayo? Fikra zako ndiyo za kwanza kukushawishi kuwa ulichopanga kukifanya hakiwezekani?
Suluhisho: Ili uweze kufikia mafanikio makubwa unayotarajia, hakikisha fikra zako zinakuwa sahihi kuhusu malengo ya mafanikio yako. Lisha akili yako kwa maarifa sahihi ili iwe na hamasa na uelewa thabiti kuhusu malengo yako. Ili fikra zako zisiwe kikwazo hakikisha unazilisha na kauli chanya kila wakati.
Mbili, Jamii. Inasemekana kuwa mafanikio yako ni wastani wa mafanikio ya watu watano wanaokuzunguka. Marafiki au watu wengine wa karibu yako ambao unatumia nao muda mwingi, wana machango mkubwa sana kwenye mafanikio yako. Jamii inayokuzunguka inaweza kuwa ni kikwazo kama watakuwa hawaendani na mipango uliyo nayo. Kwa mfano kama malengo uliyonayo ni makubwa kuliko fikra zao zinavyoamini usitarajie watakuunga mkono zaidi ya kukukatisha tamaa.
Suluhisho: Hakikisha unazungukwa na watu sahihi. Weka ukaribu zaidi na watu wenye kiu ya mafanikio na ambao wapo tayari kubadilika. Hakikisha unaungana na jamii inayoweza kukutia hamasa ya kuchukua hatua hizo kubwa na ngumu za kufikia mafanikio yako makubwa. Ndege wanaofanana huruka pamoja. Kaa na changamana na watu wanaofanana na wewe.
Tatu, Mwili wako: Mwili umekuwa ni kikwazo kikubwa pia cha watu kupiga hatua. Umekuwa haupendi kutumia nguvu zake kirahisi. Je hujawahi kuona ulikuwa umepanga kufanya shughuli fulani kwa muda mrefu lakini baada ya muda mfupi tu unahisi umechoka sana? Ndipo akili na mwili vinaanza kushauriana kuwa uache kwa muda utafanya baadaye au kesho. Pale unapoona umechoka si kweli kuwa unakuwa umeishiwa nguvu, bali mwili hutaka kutunza nguvu.
Suluhisho: Mwili wako usikudanganye wala usiusikilize na kuutii kiasi hicho. Tafiti zinaonyesha kuwa pale unapojisikia umechoka sana, unakuwa umetumia 40% tu ya nguvu zako kumbe ukiulazimisha zaidi, mwili wako utaendelea kufanya kazi. Hii inathibitishwa pale dharura inapotokea; hata kama utakuwa umechoka sana, simba akitokea utakimbia kwa kasi kubwa mpaka mwenyewe utashangaa. Hivyo mwili wako ukianza kuuambia umechoka uambie unanidanganya.
Nne, Matokeo ya haraka: Matokeo ya chapu chapu yamekuwa ni kikwazo kwa watu wengi kupiga hatua kubwa. Mara nyingi hatua kubwa huhitaji muda mrefu kuzaa matunda na hivyo watu kukosa uvumilivu wa kuenelea kuweka nguvu bila matokeo ya haraka. Hii ni sababu ya mipango mingi mikubwa kuishia njiani. Watu wengi wamekimbilia kwenye mipango ya muda mfupi ili kujipatia matokeo ya haraka.
Suluhisho: Kwanza tambua kuwa mafanikio makubwa huhitaji muda mrefu, hivyo ukiona hupati matokeo ujue muda wake bado na jitihada bado zinahitajika. Pili inakuhitaji kujenga tabia ya uvumilivu ili kuweza kufikia mafanikio yako makubwa. Usiyumbishwe na mipango ya muda mfupi ambayo mingi hukufanya uishie kupata matokeo madogo ya muda mfupi au upotee kabisa.
Ndugu! Kama maji yanavyohangaika kutokatishwa na kizuizi chochote kwenye safari yake ndivyo na wewe unavyopaswa kukataa kizuizi chochote kile kukukatisha kufika safari yako ya mafanikio. Tafakari ni vizuizi gani vinainuka katika safari yako ya mafanikio na tumia mbinu hizo hapo juu kuvikabili.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.
Mawasiliano:
Simu: 0752 206 899/0714 301 952
Email: alfred@amshauwezo.co.tz