Njia Tano(5) Za Kutoka Kwenye Uvuguvugu Na Kuwa Mtu Wa Moto.


Categories :

Naamini umekutana mara nyingi na maji ya vuguvugu. Licha ya kuwa na umotomoto kwa mbali, lakini maji hayo huwa yanakuwa hayana maajabu yoyote kwani hata ukiweka mkono wako kwa muda mrefu huwezi kuungua. Pia huwezi kutumia maji hayo kupashia au kuivishia chakula. Kadhalika huwa inakuwa ni suala la muda mfupi tu kabla ya maji hayo kupoteza moto huo na kuwa ya baridi. Maji ya vuguvugu yamekuwa shida kutambulika kwani huishia kusemwa yapo kati ya baridi na moto.

Uvuguvugu huu umehamia kwenye maisha ya watu. Watu wengi wamekuwa wakiisha maisha ya vuguvugu ambayo yamekuwa ni vigumu kuyapima. Haya ni maisha ambayo mtu mwenyewe anakuwa hajui ameshindwa au amefanikiwa. Kwa sababu watu wengi ndiyo wapo kwenye kundi hili, imeonekana kuwa ndiyo eneo sahihi la kuishi.

Ni kwa sababu ya uvuguvugu watu wameshindwa kupiga hatua na kufika mbali zaidi katika safari yao ya maisha. Uvuguvugu umewapa mazoea na kuendelea kubaki ndani ya boksi kwa kujizuia kufanya vitu vipya. Huwezi kupiga hatua kubwa kwa kubaki kwenye uvuguvugu. Ni mpaka pale utakapokubali kupashika na kuwa wa moto ndipo unaweza kutoka nje ya boksi.

Ukifanikiwa kutoka nje ya boksi utapiga hatua kubwa na kufikia ukuu wako. Naenda kukushirikisha njia tano za namna ya kutoka kwenye uvuguvugu na kuwa wa moto kisha kuanza kufanya maajabu.

1. Acha kuwa yoyote, kuwa wa pekee. Utakapochagua kuwa yoyote unakuwa wa vuguvugu. Kuwa mtu yoyote ni kuchagua kufanya chochote, hakuna maajabu yoyote kwenye kufanya chochote. Utaweza kufanya mambo mkubwa na ajabu pale tu utakapotambua kuwa wewe ni wa pekee, una nguvu za kipekee na upo hapa duniani kufanya kitu cha pekee na sio chochote. Tafakari ni kitu gani kipo kwako ambacho unaona hakipo kwa wengine? Huu ndio upekee wako.

2. Acha ndoto ndogo, tengeneza ndoto kubwa. Wale unaowaona wamefanya mambo makubwa ambayo na wewe unayashangaa, walitoka kwenye uvuguvugu na kuwa wa moto kwa kutengeneza ndoto kubwa. Wamebaki kuwa wa moto kwa kuzisimamia ndoto hizo mpaka zinatimia. Umejiweka kuwa wa vuguvugu kwa kuwa na ndoto ndogo ambazo hata zikitimia hazina maajabu yoyote kwako wala kwa jamii. Tengeneza ndoto kubwa sasa na uiishi mpaka itimie.

3. Fanya unapotakiwa, sio unapojisikia.  Watu wameng’ang’ania kubaki kuwa wa vuguvugu kwa kukosa nidhamu ya kufanya vitu kwa wakati. Kuwa moto ni kukubali kufanya kile unachopaswa kufanya bila kujali unajisikia au hujisikii. Hii ni hatua ngumu ambayo inakuhitaji wewe kujitoa. Kama unataka mafanikio makubwa huna budi kujisukuma kuchukua hatua zinazopaswa ili kutimiza ndoto zako hata pale utakapokuwa hujisikii.

4.  Usisimame, kuwa kwenye mwendo kila wakati. Kuwa vuguvugu ni kuondoa moto ambao ungeendelea kukupasha na kuwa wa moto. Umekubali kusimama baada ya kutopiga hatua zaidi kwenye kile unachokifanya. Kwa nini mafanikio yako ya mwaka jana ni sawa na mwaka huu? Kama hupigi hatua umekubali kusimama na hatimaye kurudi nyuma. Weka jitihada kuhakikisha kuwa unakua kila siku, hata kama ni matokeo madogo, yakikusanyika yatakufanya uwe wa moto.

5. Jilinganishe na wewe mwenyewe na siyo na mwingine. Ulipoukataa upekee wako kwa kujilinganisha na wengine ambao wengi wao ni vuguvugu, uliukaribisha uvuguvugu pia ndani yako. Utaweza kuwa wa moto na kupata mafanikio makubwa kwa kulinganisha kile ambacho ungeweza kufanya na nini umekifanya. Una uwezo mkubwa ndani yako wa kufanya makubwa, lakini utauona uwezo huu ukiacha kujilinganisha na watu wengine bali wewe  mwenyewe.

Ndugu! uvuguvugu ndiyo uliokufanya kuwa mtu wa kawaida. Lakini una nafasi ya kuukata ukawaida huo na kuamua kujua upekee wako na kutengeneza ndoto kubwa inayolingana na nguvu kubwa ndani yako. Usikubali kusimama kila siku piga hatua kwa kufanya kile kinachopaswa hata pale utakapokuwa hujisikii.

Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI kimeelezea kiundani zaidi kuhusu upekee wako na jinsi unavyoweza kujenga ndoto kubwa na kuiishi kikamilifu. Pata nakala yako leo kwa kupiga simu namba 0752 206 899 ili uanze kutoka kwenye uvuguvugu na kuishi maisha ya moto unayostahili.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *