Mambo Matano(5) Ya Kufanya Baada Ya Kuchelewa Kuanza Kuishi


Categories :

Maisha ya mwanadamu yapo kwenye muda tangu kuzaliwa kwake mpaka anapokufa. Katika kipindi hicho ndipo anapotarajiwa kuishi maisha yake. Historia anayoiacha duniani baada ya kufa hutegemea kile alichokifanya kipindi cha uhai wake. Bahati mbaya baada ya kufa hawezi kuibadili historia yake.

Binadamu huwa na mipango mingi sana wakati anaendelea kuishi maisha yake. Lakini kwa sababu mbalimbali mipango mingi pia huwa inaweza isifanikiwe.  Haya huwa ni masikitiko makubwa kwa mwanadamu  pale anapoishiwa muda huku hajafanikiwa kuishi maisha yale yanayomridhisha.

Inawezekana ni muda sasa umepita tangu uzaliwe au uazimie kufanya kitu lakini hujafanya mpaka sasa. Inawezekana pia umekuwa na mipango mingi ya muda mrefu ya kufanya ili uweze kupiga hatua kubwa lakini hukufanikiwa. Unakaa na kutafakari unaona kama hujapiga hatua na hali hiyo inakukatisha tamaa. Mara nyingine unajilinganisha na mtu mwingine, unaona wewe umechelewa sana kiasi kwamba huwezi kufanya jambo lolote kwa sasa.

Kama bado upo hai una nafasi ya kufanya jambo lolote. Kuna msemo unasema kuwa muda wa kupanda mti wa kivuli ulikuwa miaka ishirini iliyopita lakini kama hukufanikiwa kupanda kipindi hicho muda mwingine ni sasa. Kuna maisha ambayo ulistahili kuyaishi hapa duniani. Hayo ndiyo yangekupa ridhiko la moyo, lakini unaona hujayaishi. Ndugu muda mwingine wa kuanza kuyaishi maisha  hayo ni sasa. Hujachelewa!

Hivi ndivyo unavyoweza kuanza kuishi maisha unayostahili baada ya kuchelewa;

Tambua kusudi lako: Kwa kuwa umeshachelewa, usiendelee kupoteza muda tena. Kazi kubwa ya wewe kufanya hapa duniani ni kuishi kusudi lako. Hii ni sababu iliyokuleta hapa duniani. Pia hii ni sababu ya wewe kuendelea kuwepo licha ya kuishi miaka kadhaa bila ya kuiishi sababu hiyo. Kila mwanadamu aliyefanikiwa kuja hapa duniani ana sababu maalumu ya kuishi. Una kazi maalumu ambayo inabidi uikamilishe kabla ya kufa. Licha ya kuchelewa, una nafasi ya kuanza kuishi kusudi lako sasa. Kaa chini na tafakari kitu amabcho ungetamani kukikamilisha kabla hujaondoka hapa duniani. Hali gani inakuudhi ambayo unafikiri unaweza kuirekebisha? Huko ndiko kusudi lako lilipo. Usikilize moyo wako una majibu ya kusudi lako.

Tengeneza ndoto yako: Inawezekana umechelewa kwa sababu umekuwa unahangaika na mambo madogo madogo yaani ndoto ndogo. Wakati umefika sasa wa kutengeneza ndoto yako kubwa. Hatua gani unataka kufikia maishani mwako? Au kitu gani unataka ukipate maishani mwako? Alama gani unataka kuiacha hapa duniani? Je unatamani ufikie uhuru wa kifedha maishani mwako? Je unatamani siku kuwa kiongozi mkubwa nchini au duniani? Baada ya kuchelewa, anza hima kutengneza ndoto yako na kuiishi.

Weka malengo: Huwezi kuishi ndoto yako kikamilifu kama hutaiwekea malengo. Malengo yatakuwa ni dira ya kukamilisha ndoto yako. Weka malengo yako sahihi na kuyagawa kiasi cha kuwa na kitu cha kufanya kwa ajili ya ndoto yako kila siku. Tathmini malengo yako mara kwa mara ili kujihakikishi kuwa unapiga hatua.

Usipoteze muda tena: Umeshapoteza muda sana, inatosha!. Hakuna muda mwingine tena wa kupoteza, ni muda wa kazi sasa. Baada ya kujua sababu ya wewe kuwepo hapa duniani, kutengeneza ndoto na kuwa na malengo huna budi kutopoteza muda tena. Jenga nidhamu kubwa kuhakikisha unafanya vile ulivyopanga. Jisukume kuhakikisha kila siku unachukua hatua stahiki.

Usiishi historia, ishi sasa: Hakuna kitu chochote unachoweza kubadili kwenye mambo ambayo yalikwisha kutokea. Njia pekee unayoweza kunufaika na historia ni kujifunza kwenye makosa uliyofanya tu. Vinginevyo historia ya yale yaliyochelewa isikufanye ushindwe kuishi maisha yako ya sasa. Achana na historia yenye maumivu, ishi mipango yako ya sasa.

Ndugu! Kwa sababu bado upo hai, una nafasi ya kuanza au kuendeleza kuishi maisha yako kikamilifu sasa. Hujachelewa kwani muda mwingine wa kuishi maisha hayo ni sasa. Chukua hatua zilizoainishwa hapo juu ili kurekebisha makosa uliyoyafanya na kuanza kuishi kiusahihi sasa.

Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI kimeelezea kiundani zaidi namna ya kujua kusudi lako, kutengeneza ndoto kubwa na kuweka malengo. Pata nakala yako leo kwa kupiga simu 0752 206 899 ili uanze kuishi maisha yako. Usichelewe tena.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *