Timiza Malengo Yako Kwa Kuiishi Leo Kikamilifu
Huu ni mwanzo wa mwaka ambapo watu wengi wanakuwa wanaweka malengo ya kuuishi mwaka huu kwa mafanikio. Baada ya mwaka kumalizika, waliofanya vizuri na ambao hawakufanya vizuri wote wana hamu ya kuweka malengo kwa ajili ya mwaka mpya. Waliofanikiwa kwenye mwaka uliopita wana hamu ya kuweka malengo mengine ili mwaka huu wafanye vizuri kuliko mwaka jana. Kadhalika hata wale ambao hawakufanya vizuri mwaka ulipita wanaweka malengo wakiwa na hamu ya kurekebisha walikokosea mwaka jana ili mwaka huu wafanye vizuri.
Watu wengi wameweka malengo mazuri ambayo ukiyasikia au ukiyasoma malengo hayo yanavutia sana. Shida kubwa kwa watu wengi imekuwa si kuweka malengo, bali utekelezaji wa malengo hayo. Ndiyo maana malengo yanayopangwa Januari yanaanza kusahaulika miezi michache tu ijayo. Hata wale wanaoendelea kuyakumbuka malengo yale huishia kukamilisha kwa asilimia ndogo sana.
Kama umefanikiwa kuweka malengo bora, kushindwa kupata mafanikio ni tafsiri kuwa kuna shida kwenye namna ya utekelezaji wa malengo hayo. Kupanga ni rahisi, kazi utekelezaji. Kila mtu anaweza kuongea nini anataka, lakini ni wachache sana wanaoweka kwenye vitendo yale wanayoyasema. Ndiyo maana wanasema vitendo vinaongea kuliko maneno. Jambo mojawapo linalowaangusha watu wengi ni nidhamu, yaani kutofanya yale waliyoyapanga.
Ili uweze kutekeleza malengo makubwa uliyojiwekea, hii ni mojawapo ya nidhamu muhimu inayohitajika. Nidhamu hiyo ni kuiishi siku yako kikamilifu. Licha ya mipango ya muda mrefu uliyonayo, lakini utekelezaji wake utategemea namna unavyoiishi siku yako. Na siku yenyewe ni leo. Utaiishije leo kikamilifu?
Ipangie leo nini cha kufanya. Ili uweze kutimiza malengo yako ya mwaka hakikisha unaipangia leo nini cha kufanya. Usiiruhusu siku yako kuanza bila ya kujua kitu gani utaenda kufanya na wakati gani. Umekuwa ukilalamika kuwa muda hautoshi kufanya yale uliyoyapanga, lakini sababu mojawapo ya kuona muda hautoshi ni kutoupangia muda wako kitu cha kufanya. Usipopanga kitu cha kufanya kuna nafasi kubwa ya kwenda kufanya kitu chochote hata kile kisichokuwa na mchango kwenye malengo yako.
Panga cha kufanya leo kutoka kwenye malengo yako. Kuna mambo mengi sana ya kufanya usipokuwa na kipaumbele. Kwenye orodha ya mambo unayoenda kufanya leo weka kipaumbele cha yale yanayogusa malengo yako. Ili uweze kufanikiwa katika hili ni lazima uyafahamu vizuri malengo yako. Unaweza kujua nini ufanye leo kwa kuangalia malengo yako ya wiki uliyoyapata baada ya kugawa lengo kubwa.
Weka kazi kwenye yale uliyoyapanga. Hakuna kitakachotokea kwenye malengo yako kama hutaweka kazi kwenye kile ulichopanga. Hapa ndipo unapohitaji nidhamu kubwa. Kuna vitu vingi vinaweza kutokea baada ya kuipangilia siku yako, huna budi kuhakikisha unajisukuma kuchukua hatua za utekelezaji. Kazi ndiyo itakupa matokeo ya malengo yako.
Ianze leo mapema. Kama tulivyoona hapo juu kuwa kuna mambo mengine yanayoweza kujitokeza kwenye siku yako na yakakwamisha kuchukua hatua. Hivyo ili uweze kuiishi siku yako kwa ushindi huna budi kuianza kwa ushindi pia. Ushindi mmojawapo unaoweza kuupata kwenye siku ni kuamka mapema. Ukiamka mapema unapata muda mzuri wa kuitafakari siku yako unavyotaka iende, unapata muda mzuri wa kuipangilia siku yako. Pia unaweza kutumia muda huo wa asubuhi kusoma, kuandika, kufanya tahajudi, kusali nk ambavyo vitaandaa mwili, akili na roho yako tayari kwa siku unayoiendea.
Itathmini leo yako. Usiiache siku yako ikaisha bila kujua imeendaje. Kabla hujalala na kuianza siku nyingine kaa chini na kuitafakari siku yako. Umekamilisha nini kwenye yale uliyopanga? Umekutana na changamoto gani? Umejifunza nini? Hakikisha umefanikiwa kukamilisha angalau 80% ya yale uliyoyapanga. Kuainisha changamoto ulizokutana nazo zinakusaidia kuziepuka au kuzikabili kiufanisi siku nyingine. Kuna mengi unayoweza kujifunza kwenye siku kama utakuwa tayari. Unayojifunza kila siku yataongeza ufanisi wako.
Kuishi siku yako kwa ushindi ni kutabiri mafanikio makubwa ya malengo yako. Itathmini sana siku unayoipata kwa kuipangilia vizuri na kuwa na nidhamu kubwa na kuiishi kwa mafanikio makubwa. Anza kuiishi leo kikamilifu kwa kuzingatia vigezo hivi ili kujihakikishia ushindi kwenye malengo yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.
Mawasiliano:
Simu: 0752 206 899/0714 301 952
Email: alfred@amshauwezo.co.tz