Jenga Tabia Hii Ili Uweze Kufika Mwisho Wa Safari Ya Mafanikio Yako.


Categories :

Licha ya safari ya kufikia mafanikio makubwa kuwa ndefu na yenye magumu mengi, lakini kuna watu ambao wameweza kupitia njia hizo na kufikia mafanikio makubwa sana. Lakini idadi kubwa ya watu hawajaianza safari au wameishia njiani au wapo njiani wakisuasua. Kulingana na idadi ya watu waliofanikiwa kuwa ndogo sana, imejengeka imani kuwa hao walifanikiwa kuna vitu ambavyo wamependelewa na havipo kwa wale wasiofanikiwa.

Ukweli ni kwamba kila binadamu aliyepo duniani amependelewa. Hata wewe unayeamini kuna watu fulani wamependelewa, umependelewa pia. Waliofanikiwa na wale wanaoshindwa wametofautiana katika tabia. Ni tabia zinazoamua wewe ufanye nini, kwa namna gani na upate nini. Kwa hiyo wale wanaopita kwenye njia ngumu na baadaye kufikia mafanikio makubwa wana tabia ambazo watu wengine hawana.

Kuna tabia nyingi ambazo waliofanikiwa wanazo na zinakosekana kwa wale walioshindwa. Naenda kukushirikisha tabia mojawapo kati ya nyingi ambayo na wewe ukianza kuiishi tabia hiyo utaona mabadiliko katika maisha yako. Tabia hiyo ni shauku kubwa ya kupata kile wanachokitaka. Hii ni hamu kubwa ambayo watu wanaijenga ili kuweza kutimiza ndoto kubwa walizonazo. Kwa kuwa  shauku hiyo inawafanya wafikirie kuhusu kupata matokeo kwa namna yoyote. Shauku wanayoijenga inawasaidia kufanya yafuatayo;

Kuwa tayari kulipa gharama ya mafanikio: Kuna kila gharama ya kulipa kwenye kila mafanikio. Gharama hiyo inakuwa kubwa kadri unavyotaka kuwa na mafanikio makubwa. Ukiwa na shauku kubwa ya kutaka kupata unachokitaka unakuwa upo tayari kulipa gharama yoyote. Unaweza kujenga shauku hii kubwa ya kuwa tayari kulipa gharama yoyote pale ndoto na malengo yako yanaposhabihiana na kusudi la maisha yako.

Wanawaza ndoto hiyo muda mwingi: Huwezi kupata kile unachokitaka kama hukipi nafasi kwenye moyo wako na akili yako. Waliofanikiwa wanajenga shauku ambayo inawafanya jambo wanalotaka litokee litawale akili zao na kuliwaza kila wakati. Waza kile unachokifanya kila wakati ili akili yako itambue kuwa ndiyo kitu pekee ambacho unakitaka kitokee kwa gharama yoyote maishani mwako. Unaweza kufanikiwa kulifanya hili kwa kuliandika lengo hilo mara kwa mara, kwa mfano asubuhi, mchana na jioni au kwa kupata muda maalumu wa kukaa na kutafakari kuhusu kile unachokitaka.

Kuvumilia: Safari ya mafanikio makubwa ina changamoto nyingi. Zipo changamoto pia zenye maumivu makali. Kuna changamoto ya kutopata matokeo kwa wakati. Waliofanikiwa wana shauku ambayo inawafanya wavumilie na kuendelea na safari licha ya magumu wanayoyapitia. Ili uweze kufanikiwa kwenye mambo makubwa uliyopanga hakikisha unajenga shauku ya kuendelea kufanya hata pale matokeo yanapochelewa au pale unapokutana na maumivu.

Kujaribu mbinu mpya. Ni rahisi sana kukata tamaa pale njia ya kwanza inapogoma kukupa majibu. Lakini unapokuwa na shauku kubwa ya kukipata kitu, njia moja ikikataa, hubadilishi lengo badala yake unatafuta namna nyingine ya kutimiza lengo. Jenga shauku kwenye jambo unalolifanya kiasi cha kutokuogopa kujaribu mbinu nyingine ile ya awali inapogoma.

Kwenda peke yao: Kwa sababu ya ugumu wa safari ya mafanikio makubwa, si rahisi watu wengi kuendelea kukuunga mkono, hivyo shauku wanayoijenga watu waliofanikiwa huwasaidia kuendelea na safari licha watu waliokuwa wanaunga mkono kurudi nyuma. Jenga hamasa ambayo itakusaidia kuendelea na safari yako ya mafanikio hata ikitokea unabakia peke yako.

Kaa chini na tafakari ni kitu gani una shauku nacho ya kukitimiza katika uhai wa maisha yako? Huko ndiko unaweza kujenga malengo ambayo utakuwa na shauku nayo kuyatimiza. Hakikisha unafanikiwa kujenga shauku kwenye kile unachokitarajia kukipata, hapo ndipo unapoweza kufika safari yako licha ya changamoto mbalimbali unazoweza kukutana nazo.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *