Siku Ambayo Kobe Atamsusia Jirani Yake Nyumba Yake Ndiyo Utakuwa Mwisho Wa Uhai Wake


Categories :

Kobe ni mnyama ambaye mgongo wake umefunikwa na magamba magumu ambayo siyo rahisi kuyavunja. Mgongo huo huonekana kama nyumba kwake kwani akihisi hatari yoyote ile hujikunja ndani huku akizamisha kichwa na miguu yake na gamba tu ndilo linabaki likionekana. Hivyo mgongo huo ni nyumba inayotembea kwani huwepo popote alipo.

Kwa sababu ya nyumba hiyo kuunganika na mwili wake, si rahisi kuitenganisha na kufikiria kuiacha sehemu. Kobe huamini nyumba hiyo ni sehemu ya mwili wake na kubeba nyumba hiyo kama sehemu ya maisha yake. Siku atakayofikiria kuwa nyumba hiyo inamtesa na kuamua kumususia mwenzake ndiyo utakuwa mwisho wa maisha yake.

Nyumba anayoibeba kobe inafananishwa na kitu maalumu anachokibeba mwanadamu. Hiki ni kitu ambacho hakiwezi kutenganishwa, na pale unapofikiri unampa jirani yako ndipo unapokiua kwenye fikra zako. Kitu hicho maalumu ni upekee wako. Licha ya dunia kuwa na watu zaidi ya bilioni nane, lakini hakuna hata mmoja anayefanana na wewe kwa asilimia mia moja. Upekee huo upo ndani yako na umekuwa ukiubeba kwa maisha yote uliyokwisha kuyaishi.

Upekee huo ndiyo zawadi yako kuu ambayo umeipata hapa duniani. Kutambua upekee ndiyo kitu kinacholeta uhai wa mafanikio katika maisha yako. Imekuwa ni bahati mbaya kuwa watu wengi wanakufa bila ya kutambua upekee wao. Lakini pia ni bahati mbaya kuwa kuna watu pia wanaishi lakini wakiwa wameshauua upekee wao. Licha ya upekee huo kuendelea kuishi ndani yao, lakini fikra zao zimeuua upekee huo.

Pale unapofikiria kuwa wewe ni wa kawaida tu , wewe ni sawa na watu fulani, au maisha ya kipekee ni ya watu fulani na hivyo kuamua kuishi chochote, ni sawa na kobe anapoanza kufikiri kuwa nyumba yake anaweza kumsusia mtu yoyote. Kutokuchukua jukumu la kuishi upekee wako na kufikiri upekee uliotakiwa uuishi anaweza kuuishi mtu mwingine, ni sawa na fikra za kobe kujitenga na nyumba yake.

Fikra zako ndizo zilizohusika kuua upekee wako. Unaonekana wa kawaida kwa sababu fikra zako hazijatambua upekee wako, hivyo fikra zako zimejitenga na nyumba ya upekee wako na hivyo uhai wa upekee wako umekufa.

Habari njema ni kuwa licha ya kuwa upekee wako umekufa kwenye fikra tu, lakini ndani mwako bado upo hai japo umelala. Kinachotakiwa ni kuponya fikra zako ili kuuamsha upekee huo na kuanza kuuishi kuishi maisha unayostahili. Fikra zitakapopona zitajiunganisha tena na upekee ulio nao.

Upekee wako umejificha kwenye kusudi la maisha yako hapa duniani. Kwa sababu ya kusudi ulilonalo, ndani yako umebeba nyenzo za kipekee za kukuwezesha kuishi kusudi hilo kikamilifu. Kumbe ili uweze kuufaidi upekee wako huna budi kutambua kwanza sababu ya wewe kuwepo hapa dunia ndipo utakapoamsha uwezo wako wa kipekee kwa vipaji vyako vya kipekee kufanya mambo makubwa yenye viwango vya kipekee.

Ndugu! umeishi maisha ya kawaida kwa sababu ya kufikiri kuwa wewe ni wa kawaida na huna kitu cha kipekee ambacho unaweza ukakifanya na kuwa alama kubwa hapa duniani. Rudishia nyumba yako ya upekee kwa kuiambia akili yako wewe si wa kawaida, una upekee na unaweza kufanya mambo makubwa. Baada ya hapo jiulize maswali huku ukisikiliza sauti ndani yako kuhusu upekee wako. Je mambo gani unapenda kuyafanya kiasi cha kujisikia vibaya kama usipofanya? Mambo gani unaweza kufanya kwa viwango vya juu sana kuliko wengine? Huko ndiko upekee wako ulikojificha.

Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI kimeeleza kiundani kuhusu upekee wako ambao fikra zao zimeupoteza siku nyingi na namna unavyoweza kuuishi na kupata mafanikio makubwa. Kupata kitabu hicho piga simu leo namba 0752 206 899.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *