Fikra Zako Zisizoonekana Kwa Macho Ndizo Zilizojenga Maisha Yako Yanayoonekana Kwa Macho


Categories :

Kuna vitu tunavyoviona kwa macho na kuishia kuvishangaa, kuvipenda au kuvichukia. Vitu hivyo ni pamoja n vile ulivyovizalisha mwenyewe. Licha ya kuhusika kuvizalisha lakini wewe mwenyewe umekuwa mstari wa mbele kuvishangaa, kuvichukia na mara nyingine kuvidharau. Umeenda mbali zaidi kwa kuwalalamikia watu wengine  bila kujua wewe ndiye uliyevizalisha.

Vitu vyote unavyoviona kwa macho na vinavyokupa majawabu mbalimbali, havikuwa vitu vinavyoonekana kwa macho. Maisha uliyonayo ni majawabu ya hivyo vitu ambavyo vilikuwa havionekani kwa macho. Kabla vitu hivyo havijaonekana, vilikuwa kwenye hali ya fikra (mawazo). Kumbe kiasi na ubora wa vyote ulivyonavyo sasa vinategemea ubora wa fikra ulizo nazo kipindi hiki. Kumbe kabla hujalalamika kuhusu mazingira ya nje yanayoonekana, huna budi kulalamikia fikra zako kwanza.

Kumbe kama kuna  maisha unayoyaishi sasa na huridhiki nayo, usipoteze muda kuangalia au kulalamika badala yake nenda kwenye chanzo halisi cha matokeo ya yale unayoyaona, ambacho ni fikra. Chochote unachokiona nje kinatokea baada ya kuumbika kwanza ndani. Mahusiano uliyo nayo ni matokeo ya yale uliyokuwa unawaza na kuchukulia  kuhusu mahusiano  yako na kisha kuyatenda. Unaweza kubadilisha maisha uliyonayo na kupata maisha unayoyatamani kwa kuanzia kubadili fikra. Fikra zifuatazo ni muhimu kuanza kuzibadili ili kuwa na maisha unayoyataka;

Fikra binafsi: Haya ni mawazo yanayokuhusu wewe moja kwa moja. Unajionaje? Wewe ni mtu wa namna gani? Je wewe ni jasiri au mwoga? Wewe ni mtu wa hadhi gani? Je unajiona ni mtu maalumu au wa kawaida tu? Majibu unayojipa kwenye maswali haya ndiyo yanayoamua wewe ni nani? Kumbe daraja ulilonalo sasa, ni wewe mwenyewe uliyehusika kujiweka. Wewe ni wa daraja la juu sana. Badili fikra zako kisha utakaa kwenye nafasi unayostahili. Fikara binafsi ni eneo muhimu na la kwanza kutibu kwani fikra za maeneo mengine huathiriwa kwa kiwango kikubwa na fikra hizi binafsi.

Fikra za utajiri. Wengi huona matajiri ni watu waliobahatika, labda kwa sababu ya kuzaliwa katika familia au maeneo fulani. Lakini ukweli ni kwamba umasikini au utajiri ni zao la fikra. Una fikra gani kuhusu utajiri? Je utajiri ni mzuri au mbaya? Fikra huvuta vitu, kile unachokiwaza na kukiamini ndicho kinachotokea. Hivyo ili uweze kupata utajiri lazima uwaze vema kuhusu utajiri. Kwanza amini kuwa utajiri ni mzuri. Pili mtu yoyote, ikiwa pamoja na wewe anaweza kuwa tajiri. Kisha fikri njia ambazo zitakupa utajiri.

Fikra za mahusiano. Unawaonaje watu wengine? Unafikiri wana msaada kwako? Wanastahili thamani kiasi gani kutoka kwako? Kiungo kikuu cha mahusiano mazuri ni upendo. Kwa sababu huwezi kumjali na kumthamini mtu ambaye humpendi. Je unawapenda watu kwa kuwabagua? Fikra zako zimekuwa na athari kubwa sana kwa jinsi unavyowachukulia watu na pia unavyofikiri watu wanakuchukuliaje? Mara ngapi umekosa amani kwa kufikiri tu wewe hupendwi hata kama sio kweli? Sahihisha fikra zako kwa kuona una sababu ya kumpenda kila mtu na pia kupendwa na kujaliwa na watu linabakia kuwa jukumu lao. Wape watu thamani kubwa nao watakupa unachokitaka.

Fikra za afya. Je afya ina umuhimu kiasi gani katika safari ya maisha yako? Je unadhibiti vyakula na vinywaji unavyoingiza mwilini mwako?  Au unafikiri unaweza kufanya chochote kwenye mwili wako? Fikra hasi zimekuwa na athari hasi kwenye afya yako ya mwili, akili na roho. Chagua vyakula na kuwaza kwa muda mrefu ili afya yako iwe imara.

Fikra za utele. Je unaiona dunia yenye vitu vichache au yenye utele? Ukifikiri kuwa dunia ina utele utapata nguvu za kuendelea kukitafuta kile unachokitaka hata kama kitakawia. Lakini kama una fikra za uhaba, utaamini kile unachokitafuta kimeshachukuliwa na watu wengine. Dunia ina utele kila mtu anaweza kupata chochote kwa kiwango chochote. Fikri hivyo na anza kutafuta unachokitaka.

Fikra zako ndizo zilizokufikisha hapo ulipo. Usihangaike na matokeo ya nje, badala yake anzia ndani yako kwa kubadili namna unavyofikiri. Ukifanikiwa kubadilisha fikra zako utabadilisha na matendo yako  kisha kupata matokeo unayoyatamani.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *