Kuna mahali pa kuanzia, mahali penyewe ni hapo ulipo.


Categories :



Licha ya watu kuwa na ndoto kubwa ya kuishi maisha fulani, lakini wam Wamekuwa ekuwa wakiainisha sababu za kwa nini hawawezi kuishi ndoto hizo. na sababu ambazo zinatengenezwa na kuona ni za ukweli kabisa. Sababu mojawapo imekuwa kutokujua wapi kwa kuanzia.

Imekuwa rahisi kukutana na mtu akakuambia hajui aanzie wapi kuishi maisha anayostahili. Yaani sijui hata nianzie wapi! Imekuwa ni kauli inayotoka midomoni mwa watu wengi. Mara nyingine imekuwa ni kauli ya kukatisha tamaa mtu akiamini kama hapaoni pa kuanzia basi hawezi kupiga hatua ili kufikia malengo yake. Kama ni kuanzisha biashara, kauli hii imekuwa ikimaanisha hana mtaji hivyo hajui aanzie wapi. Lakini si kweli hakuna pa kuanzia kufanya kile unachotamani. Zifuatazo ni namna ambazo unaweza kuanza kupiga hatua kwenye yale unayoyatarjia hata pale akili inapojaribu kukuambia hakuna njia;

Anza na wazo: Kila kitu kinaanza kama wazo. Weka wazo lako vizuri, la nini unakitaka kukamilisha. Wazo huwa kama mwanga wa nini unaweza kufanya na kadri unavyoendelea kulitengeneza wazo lako ndipo unapoona wapi pa kuanzia. Mara nyingine tatizo si mtaji bali ni fedha. Je hujawahi kushuhudia mtu anashinda bahati nasibu, na kwa sababu ya kutokuwa na wazo anaishia kupoteza fedha zote na kubakia katika hali yake ya awali. Tengeneza wazo lako hata kabla ya kupata fedha.

Anza kuweka akiba. Sioni pa kuanzia inaweza kuwa kauli ya kukosa fedha ua mtaji wa kuanzisha biashara au uwekeza fulani. Wengi huongea kauli hii kwa kuona anachokizalisha ni kidogo sana, kiasi cha kutoweza kukusanya mtaji kupitia kipato hicho. Anza kukusanya mtaji hapo ulipo, yaani kutoka kwenye kipato cha sasa bila kujali udogo wake. Unaweza kuanza kutenga 10% ya kila kipato unachopata. Baada ya muda kiasi hicho kitakua na kupata mataji wa kuanzisha biashara au uwekezaji.

Anza na vitu usivyovitumia. Kuna vitu unavyo ambavyo unaweza usifikirie kuwa ndiyo mwanzo wa hatua kuelekea kufanya mambo makubwa uliyonayo. Mpaka pale utakapokaa chini na kutafakari vitu ulivyonavyo ndipo utakapogundua wapi pa kuanzia. Je nini unaweza kufanya na jokofu ulilonalo nyumbani? Je huwezi kuanzia kuuzia vinywaji baridi? Je nini unaweza kufanya na kompyuta au simu uliyonayo? Je huwezi kuitumia kufanya biashara kwa njia ya intaneti? Je hakuna vitu ambavyo huvihitaji kwa sasa unavyoweza kuuza ukapata fedha na ukatumia kama mtaji? Tafakari vitu ulivyonavyo, ni mahali pa kuanzia.

Anza kwa kubadili mtazamo.Mtazamo hasi ulionao unaweza ukawa ndiyo kikwazo kwako cha kuchukua hatua. Yamkini hupaoni pa kuanzia kwa sababu ya mtazamo hasi ulionao. Je una mtazamo gani kuhusu utajiri? Je una mtazamo gani kuhusu kazi unazoweza kuzifanya? Kama unafikiri kuna kazi fulani huwezi kuzifanya kwa sababu ya kiwango chako cha elimu, unahitaji kuanza kwa kubadili kwanza mtazamo wako. Ukifanikiwa kubadili mtazamo utaona mwanga wa wapi uanzie.

Anza na nguvu zako. Kama ni mzima na una nguvu, tayari una mtaji ambao unaweza ukaanza nao. Kuna vitu unavyoweza kuvifanya bila ya fedha yoyote. Umeshuhudia watu wakianza kwa kuwasaidia watu wengine kufanya kazi kwa sababu tu wana nguvu. Je huwezi kumsaidia mfanyabiashara kumtafutia masoko na ukalipwa kulingana na mauzo unayoyaingiza. Kama una una nguvu una mahali fulani pa kuanzia.

Ndugu kumbe kuna mhali pa kuanzia. Usiilazimishe akili yako iamini kuwa hakuna pa kuanzia. Mahali ulipo na vitu ulivyonavyo ni mwanzo mzuri wa kupiga hatua hata kama ndogo. Anza leo, pale ulipo kwa kutumia ulivyonavyo.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *