Ni Wakati Wa Kuweka Nguvu Kubwa Kabla Ya Kupata Mafanikio Makubwa.
Kabla ya ndege kuruka hukusanya nguvu kubwa kwa rubani kuiendesha kwa kasi kubwa ardhini kisha kuipaisha. Kabla gari halijashika kasi huwashwa na kuwekwa gia kubwa ili kuanza kujenga kupatia kasi kubwa.
Kuna jambo kubwa ulilolianzisha au unatarajia kulifanya ili kuweza kupiga hatua. Matokeo makubwa unayoyaona, huwa yana mwanzo wake. Mwanzo wowote huwa ni mgumu na unahitaji nguvu kubwa ili kuweza kupiga hatua. Wale unaowaona wamefikia hatua kubwa katika maisha yako, walifanikiwa kuweka kila jitihada kubwa kwenye mwanzo wa mambo wanayoyafanya.
Yafuatayo ni mambo unayoweza kufanya zaidi kipindi unapoanzisha jambo, ukiyafanya hayo utaweza kutengeneza msingi mzuri wa hatua zinazofuta;
Maarifa zaidi: Unapoanza jambo lolote unakuwa mgeni nalo, vitu vingi unakuwa huvifahamu. Kwa mfano unapoanza biashara fulani, mambo mengi kuhusu ile biashara unakuwa huyafahamu, hata kama utakuwa unafahamu, lakini ni kwa juu juu tu. Hivyo pia kwenye kazi, kama ndiyo unaanza, huna uzoefu, kuna vitu vingi vya kujifunza. Unahitaji kuweka nguvu kubwa katika maarifa unapoanza jambo ili kukifahamu kiundani zaidi.
Kujitangaza zaidi: Licha ya mambo unayoyafanya na kutoa thamani, kazi yako itakuwa haina maana kama thamani yako itakuwa haitambuliki kwa watu. Unapoanza kutoa thamani watu wanakuwa hawaitambui, unahitaji kuwafahamisha watu kile unachokifanya ili watu waweze kukitambua na kuifikia thamani hiyo. Umeanzisha nini sasa, au umekuwa ukifanya nini kwa muda ambacho hakijajulikana? Kama unataka kufikia mafanikio huna budi kuweka nguvu kubwa kwenye matangazo ili watu waje na wapate thamani yako. Bila kuweka nguvu kubwa utaendelea kusuasua.
Uvumilivu zaidi: Mwanzo huwa na changamoto nyingi, moja ya sababu ni uchanga wa jambo unalolifanya. Pia unapoanza kitu unakuwa hupati faida au kama unapata ni kidogo sana. Mara nyingine unapata matokeo ambayo hukutarajia. Katika hali kama hii wengi hukata tamaa na kurudi nyuma. Haya yanatokea unapoanza safari. Hapa ndipo unapohitaji uvumilivu zaidi. Jiandae, utakapopata matokeo usiyotarajia usirudi nyuma, ni kipindi kinachohitaji uvumilivu wako.
Kazi zaidi: Kuanza kitu ni kutengeneza njia kwenye msitu. Kuna miti, vichaka na nyasi vya kuviondoa ili uweze kuendelea na kazi. Unapoanza biashara au mradi wako unahitaji kuweka kazi kubwa zaidi kuliko yule aliyeanza zamani na biashara na mambo yake kukaa vizuri. Weka kazi kubwa kwenye jambo ulilolianzisha. Weka muda na umakini pia
Utafiti zaidi: Kama ndiyo umeanzisha jambo jipya, unahitaji kufanya majaribio mbalimbali ili kujua mbinu unazoweza kuzitumia, na pia kuongeza uelewa wa jambo unalolifanya. Mbinu gani unazoweza kuzitumia zikazaa matunda zaidi? Fanya utafiti wa wapi biashara yako inafanya vizuri ili uwekeze nguvu huko. Fanya utafiti kujua watu unaoweza kuchangamana nao (connections).
Muda zaidi: Jambo jipya ni sawa na mtoto mchanga huhitaji muda mwingi wa kumuangalia kwani anakuwa hawezi kujitegemea. Jambo ulilolianza linahitaji uangalizi mkubwa, uwepo wako na umakini wako. Tenga muda wa kutosha kuhakikisha unalijengea misingi imara unalolifanya sasa.
Jambo gani umelianzisha sasa? Tambua ili uweze kufikia mafanikio makubwa, huna budi kuweka nguvu kubwa ili kulisukuma jambo hilo lisonge mbele. Angalia ni kitu gani inabidi kukipa nguvu zaidi ili uweze kusimama na kupia hatua.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz