Boresha Vyanzo Hivi Sita(6) Ili Kuwa Na Maisha Bora Zaidi


Categories :

Ubora wa mazao ya mimea hutegemea ubora wa ardhi ambako mimea hiyo imejishikisha. Ni kupitia udongo ambako mimea itapata mahitaji yote muhimu kama maji, virutubisho na sehemu ya kujishikisha ili iweze kustawi. Mahitaji haya ndiyo yanayohitajika ili mmea huo uweze kukua vizuri na kustawi na kuzaa matunda. Ubora wa mazao hayo hauwezi kuzidi ubora wa vile vilivyopo kwenye udongo. Kama utaona mazao hayo yanasussua, sehemu ya kwanza ya kuchunguza ni kwenye chanzo chake.

Kuna vitu vingi sana unavyovifanya maishani ili kupata mafanikio. Kuna wakati umeweka nguvu kubwa lakini unachokiambulia ni kidogo sana. Umeona wengine wenye umri sawa na wewe wakiwa wamepiga hatua kubwa kuliko wewe. Umekuwa ukijiuliza utofauti huu unatoka wapi? Nini kinasababisha utofauti huu? Nini chanzo cha matokeo hafifu unayoyapata?

Kwenye kila matokeo unayoyapata kuna visababishi. Visababishi ndiyo vinavyoamu matokeo unayopata. Ubora wa matokeo unayoyapata unategemea visababishi hivyo pia. Visababishi hivyo ndivyo vyanzo vya matokeo unayoyapata. Kama muda ndiyo kisababishi pekee cha matokeo unayoyapata, basi kadri muda mwingi unavyotumika ndivyo unapotarajia kupata matokeo bora  zaidi. Kumbe  ‘huwezi kupata matokeo bora zaidi ya chanzo chake’. Kuna vyanzo vingi vilivyosababisha matokeo uliyo nayo. Unaenda kujifunza vyanzo hivyo na namna vinavyosababisha matokeo yako kisha utajifunza njia za kuboresha ili uweze kupata matokeo bora zaidi maishani;

Huwezi kuwa na fikra bora kuliko maarifa uliyonayo. Kile unachokifahamu ndicho kinakuwa mwongozo wa namna unayofikiri. Maarifa gani unayaingiza kwenye akili yako? Kama unaingiza maarifa bora unatarajiwa kuwa na fikra bora kwani chanzo chake kitakuwa bora. Kama hakuna maarifa mapya unayoyaingiza usitarajie kuwa na fikra mpya. Kitu kimojawapo ambacho kimekuwa kikikuangusha kupiga hatua ni uvivu wa kupata maarifa mapya na mazuri kila wakati kwa njia ya kusioma vitabu, kusikiliza kanda, kuhudhuria semina nk. Anza kuingiza maarifa mengi na sahihi kuboresha fikra zako ambazo ndiyo chanzo cha mafanikio yako.

Kipato chako hakiwezi kuwa zaidi ya thamani unayotoa. Kipato kidogo ambacho hakitoshi kimekuwa kilio cha watu wengi. Wengi wameishia kulalamika maisha ni magumu wakiamini serikali au watu fulani wanastahili kubeba lawama hizo. Ndugu, kipato chako ni zao la thamani unayoitoa, hivyo chanzo cha kipato chako ni thamani. Huwezi kupata kipato kikubwa kama thamani unayoitoa ni ndogo. Tafakari leo ni namna gani unaweza kuboresha bidhaa au huduma unazozitoa ili ziwe na thamani bora zaidi na ndipo utapata kipato zaidi.

Afya yako ya mwili haiwezi kuwa bora zaidi ya chakula,mazoezi na mapumuziko. Kuna vyanzo vinavyoamua afya yako kama vile chakula unachokula, mazoezi unayofanya na jinsi unavyopumuzisha mwili. Afya yako uliyonayo leo ni matokeo ya vyakula, mazoezi na mapumziko ya mwili ambayo umekuwa ukiyafanya muda uliopita. Kama una tatizo la uzito mkubwa huna budi kurekebisha vyanzo vilivyosababisha hilo. Afya ni mtaji wako muhimu wa mafanikio yako makubwa . Boresha vyanzo vya afya yako ili uimarishe.

Maamuzi yako hayawezi kuwa bora kuliko imani yako. Vitendo tunavyochukua vinategemea imani na tunavyofikiri. Bahati mbaya au nzuri ni kuwa hakuna kinachoweza kutokea kwako bila kufanya maamuzi. Maauzi yako bora ambayo yanaleta vitendo na matokeo bora yanategemea unafikiri na kuamini nini. Mawazo chanya ambayo yanatokana na kusikia na kusoma ndiyo yanayoweza kukutengenezea imani bora ya kufanya maamuzi bora.

Matokeo bora hayawezi yakazidi kazi unayoweka. Kama ulivyoona hapo juu, ni kazi ndiyo inayokupa matokeo. Hata uwe na maarifa mazuri kiasi gani usipoweka kazi kwenye maarifa hayo, ni bure. Vivo hivyo hata uwe na imani kubwa na bora kiasi gani, usipoweka kazi ni bure. Kama upo kwenye mwelekeo sahihi, weka kazi ziadi ilil utapate matokeo zaidi.

Huwezi kuwa na mahusiano bora kuliko msingi wake. Uhusiano ni mhimili muhimu sana wa mfanikio yako. Mafanikio yako hayana maana yoyote kama hayagusi watu wengine. Utawagusa watu wengine wengi na kwa kwa ubora kama kutakuwa na mahusiano mazuri. Msingi wa mahusiano unajengwa na upendo, uvumilivu,kujali, muda, wema nk. Kama mahusiano yako na watu wengine hayapo vizuri, anza kuboresha msingi wake.

Ndugu! Ni wakati wako wa kuongeza thamani katika kila eneo la maisha yako. Kaa chini na tafakari ni maeneogani ya maisha yako hayapo vizuri? Je ni fedha, kazi, afya au mahusiano?  Nenda kwenye vyanzo vyake na kuanza kuviboresha ili kuweza kuishi maisha bora unayoyatarajia.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *