Utafanikiwa Kuishi Maisha Yenye Mafanikio Makubwa Pale Utakapoanza Kutumia ‘User Manual’ Yako.


Categories :

Kiwanda chochote baada ya kutengeneza kifaa chochote hasa vile vinavyotumia umeme hutengeneza mwongozo wa mtumiaji (user manual). Haya ni maelezo ya kina kuhusu kifaa hicho. Mwongozo wa mtumiaji huwa na vitu kama jina la kifaa, matumizi yake, namna ya kutumia, vifaa vingine vinavyoingiliana, shida unazoweza kukutana nazo na namna ya kuzitatua.

Mwongozo huo huelezea kwa uhakika namna gani kifaa hicho kinavyoweza kufanya kazi kwa ubora kama utakitumia kama ilivyotarajiwa. Lakini mtengenezaji huainisha pia shida zinazoweza kutokea wakati unaendelea kutumia, hivyo kupendekeza hatua unazoweza kuzichukua. Matatizo madogo unaweza kuyatatua mwenyewe na pia hukujulisha ni wapi upeleke pale unaposhindwa kutatua tatizo hilo. Hii yote ni kwa lengo la kuhakikisha kifaa hicho kinatimiza lengo lake.

Licha ya binadamu kutokuwa kifaa, lakini ili aweze kuwa na uhakika wa kufanya mambo makubwa kwa mafanikio makubwa, lazima atumie ‘user manual’ yake. Huu ni mwongozo ambao utamfanya mtu huyo aweze kutumika kama Muumba wake alivyotarajia. Mwongozo huo utamtambulisha yeye ni nani na ana kazi gani maalumu na nini akifanye ili kutimiza hilo kusudi. Pia utamueleza ni kwa namna gani ataweza kukabiliana na changamoto ili zisikwamishe ufanyaji kazi wake.

Vifaa kutoka kiwandani hufungashiwa mwongozo wa mtumiaji kwenye kifungashio chake. Lakini hakuna binadamu aliyezaliwa na mwongozo huo ukiwa ni maandishi. Hii imekuwa changamoto kwa watu wengi wakiamini yeye ni yeyote, anaweza kufanya chochote kwa namna yoyote ile. Hiki ndicho kilichopelekea watu wengi kushindwa kwa sababu ya kutokujua kazi maalumu waliyotarajiwa kuifanya na Muumba wao. ‘User manual’ yako tayari ipo, ipo ndani yako tangu kuzaliwa kwako.

Bahati mbaya user manual yako haipo kwenye maandishi kama vifaa vya kiwandani, bali ipo ndani ya moyo wako. Unahitaji kusikiliza moyo wako kwa ukaribu ili uweze kuutambua mwongozo huo kisha kuufuata ili uweze kuishi kikamilifu kama ulivyotarajiwa. Ukiufuta mwongozo huo utakupa vifuatavyo;

Utambulisho wako. Wewe ni nani? Hili siyo swali linalouliza jina lako, bali linabeba chanzo na jukumu ulilo nalo. Huwezi kupata jibu sahihi la swali hili kwa kuiliza jirani yako, hakufahamu wewe ni nani. Sikiliza moyo wako au uliza aliyekuumba kujua wewe ni nani.

Kusudi lako. Kila kifaa kinachotengenezwa kina kusudi lake. Mara zote kifaa hicho hulenga kutatua tatizo fulani ambalo lipo kwenye jamii. Kama binadamu una sababu maalumu ya kuwepo hapa duniani. Kuna uhitaji ambao inabidi uutatue. Sikiliza kwa karibu moyo wako, ndiyo wenye mwongozo wako wa kwa nini upo hapa duniani .

Kipaji chako. Ili uweze kutimiza kusudi lako unahitaji uwezo wa kipekee ambao utakuwezesha kufanya kazi kwa viwango vya juu sana. Uwezo huo wa kipekee upo kwenye kipaji chako. User manual yako inajua vitu ambavyo unaweza kufanya kwa ustadi mkubwa. Hakuna sehemu ya kusoma kujua kipaji chako, bali tafakari na usikilize moyo wako.

Mazingira ya kufanyia kazi. Kila kifaa huwa kinaelezwa kinafanya kazi maeneo gani. Hali ya hewa kama joto na unyevu vitazingatiwa kwenye mwongozo huo. Mazingira gani ukiwepo unapata hamasa ya kutumia kipaji chako vizuri?

Watu unaoweza kufanya nao kazi. User manual ya kifaa hueleza bayana kifaa kingine kinachoweza kufanya kazi pamoja na kifaa ulichonunua. Kama ni kompyuta user manual itaelezea kuwa inaweza kuunganisha kwenye spika nk. User manual yako inapasa ielezee watu ambao unaweza kufanya nao kazi na ukafanikiwa kupata mafanikio makubwa. Moyo wako na akili yako viamue ni watu utakaoshirikiana nao ili kutimiza ndoto.

Kutatua changamoto. Kama user manual ya kifaa inavyoweza kuelezea ni kwa namna gani unaweza kutatua changamoto zinazoweza kukikumba kifaa ndivyo unavyotakiwa kujua namna gani ya kuweza kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza wakati unafanya kazi yako. Je ukiona uwezo wa kutafakari umepungua utalala kwanza? Je utajifanyia tathmini kujua kama unatimiza malengo yako vema.

Ndugu! Unahitaji kujijua vizuri kuhusu wewe na kisha kujua ni namna gani unaweza kuliishi kusudi lako kikamilifu. Mwongozo wa namna unavyoweza kutumika vema, tayari upo ndani yako. Tulia na sikiliza moyo wako, utakupa mwongozo mzima. Hata pale unapoona unakwama, usome moyo wako utakuambia nini cha kufanya.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *