Muda Hautakuwa Na Subira Kwako Katika Mambo Haya Matano(5) Unayoyafanya.


Categories :



Siku ulipozaliwa tu, ulipewa kibali cha kuishi hapa duniani. Sambamba na hilo, muda wako wa kuishi hapa duniani ulianza kupungua kwenye akaunti yako ya muda. Kila sekunde unapovuta na kuitoa pumzi, muda wako wa kuishi hapa duniani unazidi kupungua.

Kila mtu amepewa muda maalumu wa kuishi hapa duniani ili aweze kutimiza kusudi lake la kuletwa hapa duniani. Muda pekee uliopewa unaweza ukautumia vizuri na kuacha alama ambayo dunia itaendelea kukukumbuka au unaweza kuutumia vibaya na dunia ikaendelea kukudai hata baada ya kufa.

Kufanya mambo sahihi na kwa muda sahihi ni kuamua kwenda sambamba na muda. Lakini kuna mambo ambayo ukiyafanya, muda utakuacha nyuma na hivyo kutokuwa na subira kwako. Nitakushirikisha mambo matano ambayo ukiyafanya muda utakuwa unakosa subira kwako.

Kuahirisha mambo. Watu wengi wamekuwa wepesi wa kupanga mambo ya kufanya. Hasa mambo yale yatakayotakiwa yafanyike muda ujao yaani baadaye, kesho, juma lijalo,mwezi ujao nk. Lakini ni watu wachache sana ambao wameweza kuyafanya mambo hayo baada ya muda huo kufika. Muda wa kuyafanya waliyopanga unapofika, wamekuwa wagumu kuyafanya badala yake wameahirisha na kusema watafanya kesho. Hii ndiyo imekuwa sumu ya kupata matokeo na kufikia malengo. Kama na wewe ni miongoni mwa watu hao wanaoahirisha mambo tambua kuwa muda hauna subira kwako; muda unaenda mbele, wewe unabaki nyuma.

Kuishi ndoto ndogo. Binadamu wote wamepewa muda sawa katika siku. Ni kupitia siku kila mtu anapata muda wa kufanya mambo mbalimbali. Katika muda huo, unaweza kuamua kuishi ndoto ndogo au kubwa. Hivyo hakuna tofauti ya muda katika kuishi ndoto ndogo au kubwa. Kuamua kuishi ndoto ndogo ni kujipunja na hutatumia muda mchache ukilinganisha na yule anayeishi ndoto kubwa. Tengeneza ndoto kubwa na anza kuiishi kwa kutumia muda unaotumia kuishi ndoto ndogo.

Kuiga maisha ya watu wengine. Kila binadamu anayeletwa duniani ana upekee ndani yake. Huo ni upekee ambao dunia inatarajia atafanya mambo ya kipekee na makubwa. Upekee huo upo ndani yako na sio kwa mtu mwingine. Unapoamua kuiga maisha ya mtu mwingine, unapoteza upekee wako na hivyo kuishindwa mambo makubwa na ya kipekee. Muda hautakusubiri wewe utakapoendelea kuiga watu wengine.

Kuishi bila malengo. Huwezi kuutumia muda wako vizuri bila kuweka malengo. Malengo yanakuwa dira ya nini ukifanye kwa muda gani. Kuna nafasi kubwa sana ya kupoteza muda unapoishi bila malengo na muda utakosa subira kwako.

Kuishi kwa hofu. Kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa nini kinaweza kutokea muda ujao, mwanadamu ana nafasi kubwa ya kutengeneza hofu katika maisha yake. Hii imekuwa sababu mojawapo ya watu kutoweka malengo makubwa kwa kuhofia kushindwa. Hofu ya kushindwa imewatawala watu. Watu wamekosa furaha kwa sababu ya hofu. Lakini kumbuka unapohofia muda hausimami, hivyo usiruhusu hofu itawale maisha yako. Weka malengo makubwa fanya kwa viwango vikubwa, iache asili ikupatie matokeo. Usihofu kushindwa, hutakuwa mtu wa kwanza. Pia kushindwa ndiyo ngazi za kuyapandia mafanikio yako. Furaha yako isitegemee matokeo, iishi leo kikamilifu, usiihofie kesho haijafika kwako.

Ndugu! Muda wako hautasimama na hautakuwa na subira kwa kufanya mambo hayo yaliyoainishwa hapo juu. Kitu gani unatamani ukikamilishe ungali upo hai? Weka malengo na mipango ya kuanza kuyatimiza hayo. Tekeleza uliyopanga kufanya leo, usisubiri kesho kwani inaweza isije. Furahi kwa sababu ungali hai kwani unapata nafasi ya kufanya tena uliyoshindwa.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *