Haya Ndiyo Maajabu Usiyoyajua Yanayotokea Baada Ya Kuweka Na Kuanza Kuyatimiza Malengo Yako.


Categories :

Kuweka na kutimiza malengo imekuwa ni changamoto kwa watu wengi. Watu wengi wamekuwa wakiishi bila malengo. Hii inaweza kuwa sababu ya mazoea yaliyojengeka kwa sababu ya kuzaliwa na kukua bila kushuhudia wazazi au walezi wake wakiweka malengo. Wapo wanaoweka malengo lakini yanakuwa hayana ubora, yameishia kuwa ni matamanio tu na hivyo yamekosa nguvu ya kutimizwa. Wapo wengine wanaofanikiwa kuweka malengo yenye ubora lakini wameshindwa kuyatimiza kwa sababu ya kukosa hamasa. Hivi ndivyo malengo yamekuwa changamoto kwa watu wengi.

Licha ya changamoto hizo hapo juu, kuweka na kutimiza malengo imekuwa ni miongoni mwa vigezo muhimu vya mtu kupata mafanikio makubwa. Hatua ya kuweka na kuanza kuyatimiza malengo yako imekuwa ni hatua kubwa sana katika kuyafikia mafanikio yako. Kuna maajabu makubwa sana yanayotokea baada ya kufanikiwa kuweka na kuanza kuyaishi malengo yako. Kujifunza muujiza huo ni fuatilia zoezi hili na kuona ni kwa namna gani kuweka malengo kunaweza kukuletea maajabu ya kufikia mafanikio makubwa.  

Zoezi hili linafanyika kwa kumtoa njiwa wa kufungwa kwenye banda lake na kumweka kwenye boksi na kisha kulifunika boksi hilo na blanketi. Zoezi hili unaweza kuliendeleza kwa wewe kuchukua boksi hilo na kuweka kwenye buti ya gari na kuliendesha gari hilo umbali wa maili zisizopungua elfu moja kuelekea upande wowote ule. Ukifika umbali huo, chukua boksi hilo nje ya gari kisha kulifungua. Mrushe njiwa huyo hewani. Nini kitatokea? Kitakachotokea ni kitu ambacho kinaweza kukushangaza sana. Njiwa huyo ataruka hewani na  kuzunguka hewani kama mara tatu hivi kisha kuanza safari ya kurudi nyumbani kwake bila ya kukosea licha ya umbali wa maili elfu moja uliomtenga na nyumbani kwake. Haya ni maajabu ehee!

Huyu ni miongoni mwa viumbe vya dunia vyenye uwezo mkubwa sana wa kufanya kazi ya kufuatisha malengo. Uwezo huu kwa lugha ya Kiingereza huitwa ‘cybernetic’. Kiumbe mwingine ambayo yupo zaidi ya njiwa huyu ni wewe binadamu. Cybernetic ni sayansi ya mfumo wa mawasiliano na uthibiti wa moja kwa moja ambao unapatikana kwenye mashine na viumbe hai.

Maajabu ya nguvu hii yatatokea kwako pale utakapotambua kwa wazi kabisa nini hasa unakitaka. Hapo ndipo utaanza kuelekea kwenye  lengo lako bila ya kukosea wala kushindwa. Kadhalika ndipo na lengo litakapoanza kuelekea kwako na kukutana nawe mahali sahihi na muda sahihi. Mara nyingi tumewaona watu wanaofanikiwa kuwa wana bahati baada ya kupata kitu fulani ambacho unaamini na wewe ungeweza kukipata. Tofauti ni kwamba wengi unaowaona kuwa wamebahatika, walikuwa na maandalizi ukilinganisha na wale wanaokosa. Maandalizi hayo ni kuweka malengo. Mwanafalsafa wa Roma, Seneca, alisema “Luck is what happens when preparation meets opportunity”  ikitafsiriwa kuwa bahati ni kile kinachotokea pale maandalizi yanapokutana na fursa.

Nguvu hii ya maajabu ya kukufikisha kwenye mafanikio ya malengo makubwa ipo ndani yako pia ikiwa imezama ndani ya akili yako. Unachopaswa kufanya ili kufaidika na nguvu hii ni kuweka malengo yenye sifa bora na kuanza kuchukua hatua. Hapa ndipo nguvu hii itakapoanza kukuendesha na kukukutanisha na matokeo ya malengo yako. Inawezekana unajiuliza nitawezaje kuweka malengo yenye sifa na kuweza kuipata nguvu hii ya ajabu? Usiwaze sana kuhusu hilo, kwa sababu ninitamani sana upate mafanikio unayostahili, nimekuandalia mwongozo wa kuweka na kutimiza malengo yako. Unaweza kuupata mwongozo huo kwa kubonyeza kiunganishi hiki https://www.amshauwezo.co.tz/mwongozowamalengo

Ni wakati sasa wa kuweka au kuboresha malengo yako, yawe wazi kisha kuanza kuyasogelea ili uweze kukutana na nguvu hii kubwa ya maajabu ya ‘Cybernetic’. Ni nguvu ambayo kila mtu anayo, anza kuiamsha sasa na kunufaika.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi

Mawasiliano;

Simu; 0752206899/0714301952

Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *