Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujiona Mtu Wa Maana Katika Dunia Hii.


Categories :


Kujiona mtu wa maana limekuwa ni hitaji muhimu sana la binadamu. Mtu hujisikia raha, amani na ridhiko pale unapojiona ni wa maana katika dunia hii. Kujiona wa muhimu kunahusisha kutambuliwa na watu wengine. Jamii inapotambua uwepo na mchango wako ndipo inapohisi una thamani mbele ya dunia hii.

Licha ya umuhimu mkubwa huu wa kuwa wa maana katika dunia hii, kupata maana hiyo imekuwa changamoto kwa watu wengi. Kuna watu wamefanya mambo mengi ambayo wao walifikiri yangewapeleka katika hali ya kuridhika na kuona wa maana katika dunia hii, lakini hawakufikia hali hiyo. Kuna watu walifikiri kuwa baada ya kusaka na kuupata utajiri wangeweza kufikia ridhiko hilo, lakini walipoupata utajiri huo wakaona bado watupu.

Naamini ni kiu yako pia kuridhika na maisha haya na kuuona umuhimu wako katika maisha ya hapa duniani. Nitaanzia wapi? nifanye nini? Nitafanyaje ili nipate maana ya maisha yangu? Umaana wa maisha yako unaanza kwa kuipa dunia thamani ambayo inatarajia kutoka kwako. Kila mwanadamu ana kitu cha pekee ndani yake ambayo ni zawadi kwa dunia. Unapofanikiwa kuitambua zawadi hiyo na kuipa dunia ndipo unapoanza kuridhika moyoni mwako na kuona kuna kitu cha thamani unakifanya. Si hivyo tu bali hata dunia itaanza kutambua thamani hiyo unayoitoa. Yafuatayo ni mambo unayoweza kuanza kuyafanya ili kuanza kuona maana yako hapa duniani;

Tambua na ishi kusudi lako. Kazi ya maana ya nyuki ni kutengeneza asali, kazi maalumu ya basi ni kusafirisha abiria na si kulima. Maana yako itaanza kuonekana baada ya kujua kazi maalumu ya wewe kuwepo hapa duniani. Hii ni kazi iliyobebwa na kusudi la maisha yako. Upo hapa duniani kufanya nini? Kwa kutambua na kuishi kusudi lako utaziba uwazi ambao dunia bado inakusubiri wewe mtu pekee uuzibe.

Ndoto. Unapoota ndoto ya kawaida unaona mfululizo wa matukio fulani yakitokea. Ndoto ya maisha yako ni picha kamili ya nini unachotaka ukipate au ukifanye maishani mwako. Hiki ni kitua ambacho unataka ukipate ungali hai. Kuwa na ndoto, hasa kubwa kunakupa matumaini kuwa kuna kitu unacho na utakikamilisha, kwani utakuwa unauona mwisho tangu mwanzo na hivyo kujiona wa maana kwa kuiishi ndoto hiyo.

Malengo. Malengo ni mwelekeo. Kutojua wapi upo na wapi kwa kueleke ni sawa na kupotea. Hakuna matumaini yoyote kwenye kupotea. Unaweka malengo na kuyatimiza, kunakupa uhakika kuwa upo njia sahihi na kuwa kuna matokeo unayoyazalisha ambayo ni muhimu kwa watu wengine. Hii inakupa kujiamini na kupanga makubwa zaidi baada ya kutimiza malengo madogo. Hatua za kuyatimiza na matokeo ya malengo yanakufanya ujione unaweza kufanya kitu fulani chenye maana maishani mwako. Weka malengo leo na anza kuyatimiza sasa.

Thamani kwa watu wengine. Unachokifanya kinakuwa na maana kama kinakuwa na mchango kwa watu wengine. Utahisi una maana katika maisha yako kama kitakuwa kinagusa maisha ya watu wengine. Yaani kina thamani kwa watu wengine. Hakikisha unachokifanya kinagusa na kuboresha maisha ya wengine.

Muda. Muda ndiyo rasilimali muhimu sana katika maisha yako. Ukipoteza muda hutaupata tena. Kadri muda unavyo kwenda bila ya kufanya kitu chenye thamani ndipo unavyozidi kujiona huna thamani. Baada ya kuweka malengo yako, weka nidhamu na kazi kuhakikisha unatumia muda vizuri na kupata matokeo.

Ndugu! Una nafasi ya kutafuta maana ya maisha yako tena. Maana hiyo ipo ndani yako. Iamshe kwa kutambua kusudi lako, kisha kuliishi kwa kuweka malengo yatakayokupa matokeo ya kukuridhisha wewe na kugusa maisha ya watu wengine.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *