Chuma Kilivumilia Maumivu Ya Moto Ili Kiweze Kupondwa Na Kutengeneza Umbo zuri La Kifaa Kinachokupendeza Machoni Leo.
Kuna vitu vingi ambavyo umekuwa unaviona vilivyotengenezwa kwa chuma. Vingi vimetengenezwa kwa maumbo mazuri yanayovutia kuangalia, kwa mfano bati la kuezekea, sufuria, injini na bodi za magari nk. Usichoweza kukumbuka kwa haraka kuhusu maumbo hayo ni kuwa mwanzoni chuma hicho kililiwekwa kwenye moto mkali ili kilainike hata kufikia hali ya uji. Ili kuweza kupata umbo lililotakiwa, chuma hicho kilitakiwa kuvumilia moto huo na kupondwa kwake.
Watu unaowaona leo wamepiga hatua kubwa kwenye maisha yao, kiasi cha wewe kutamani kuwa hatua hiyo wana historia ambayo hujaisoma au haijawekwa bayana. Kama ilivyo kwenye chuma ili kutengeneza sura nzuri huhitaji moto, nao walipita kwenye moto mkali wa kuwatengeneza sura ya mafanikio unayoyaona leo. Moto wao haukuwa wa kuni, umeme au makaa ya mawe, bali mawazo yao na hata miili yao. Walikubali kuwa wanyenyekevu na kubadili ugumu kwenye akili zao ambao haukuwa na sura ya mafanikio kisha walilainisha akili zao ili kuunda sura mpya ya mafanikio.
Naamini unayataka mafanikio tena makubwa. Lakini akili yako ina sura ya kushindwa, ambayo haiwezi kukupa mafanikio unayoyataka. Unahitaji kuiweka akili na mwili wako kwenye moto ambapo utapondwa na kuwa na sura ya mafanikio. Usipokubali hutaweza kupata sura mpya ya (mafanikio). Moto wa kukuumbia sura ya mafanikio ni mkali na wenye maumivu. Lakini ili uweze kupata mafanikio hayo huna budi kuvumilia. Anza kukubali maumivu yafuatayo ili kutengeneza sura nzuri ya maisha yako ya mafanikio;
Kuacha tabia za zamani. Kuna tabia zilizokutengeneza wewe wa kushindwa. Tabia hizo umeziishi kwa muda mrefu. Ili uweze kutengeneza sura nyingine ya mafanikio huna budi kuziacha tabia za zamani kwanza. Kuacha tabia ulizozizoea si kazi rahisi, inahitaji kazi kubwa na uvumilivu. Tabia hizo ni kama kulala muda mwingi nakuchelewa kuamka, kuahirisha mambo, kulalamika nk. Orodhesha tabia zilizokukwamisha kisha weka mikakati ya kuanza kubadili moja baada ya nyingine.
Kuiendea hofu. Kama kuna adui mkubwa aliyefanikiwa kukuumba wewe wa kushindwa, basi ni hofu. Hofu ni zao la kuona matokeo usiyoyapenda na yanayoogofya hata kabla hujachukua hatua. Unapoyaona matokeo hayo, umekuwa ukitafuta namna ya kutoroka matokeo hayo. Mbinu mojawapo ambayo umekuwa ukiitumia na ndiyo iliyokufikisha hapo ni kutochukua hatua. Waliofanikiwa wana hofu pia, lakini wao wamejenga tabia ya kufanya kitu hata kama wana hofu. Imekuja kugundulika kuwa vitu vingi tunavyovihofia havitokei. Jipe ujasiri wa kuanza kuchukua hatua zile muhimu za maisha yako ulizozikimbia kwa sababu ya hofu.
Kuacha baadhi ya marafiki. Wanasema mafanikio yako ni wastani wa mafanikio ya watu watano wanaokuzunguka na kushirikiana nao. Mojawapo ni marafiki zako. Kuna wakati inakulazimu kufanya uamuzi mgumu wenye maumivu wa kuacha watu wa karibu ambao hawakupi msaada wa kutengeneza sura nzuri ya mafanikio. Si jambo jepesi, lakini itakulazimu na utahitaji kuvumilia.
Kuendelea hata bila matokeo. Fundi chuma huendelea kuchochea moto pale anapoona chuma bado hakijapashika au kuyeyuka. Wakati huo chuma huendelea kuvumilia ili mwisho wa siku kiwe kwenye sura nzuri. Matokeo ya malengo makubwa mara nyingine huchelewa au huja yale ambayo hukuyategemea. Huo sio muda wa kukata tamaa, bali kufikiri kwa kina na kuweka kazi zaidi ili kupata kile unachokitaka.
Kukubali kukosolewa. Ni kawaida ya watu wengi kupenda kusifiwa na sio kukosolewa. Kupenda hali hiyo ni kuzuia ukuaji wako. Huwezi ukawa sahihi kwa asilimia 100 kwenye kila kitu. Ili uweze kutengeneza sura nzuri ya mafanikio yako huna budi kuvumilia ukosoaji. Lakini pima ukosoaji unaoupata kisha jifunze pale inapotakiwa. Utaupata ukosoaji kwa njia ya maoni ya watu kwa vile unavyofanya au mpishano wa mtazamo wako kupitia kusoma vitabu au kuhudhuria semina.
Naamini unahitaji kutengeneza sura mpya ya mafanikio katika eneo fulani la maisha yako. Una nafasi hiyo kwa kukubali kuwekwa kwenye moto kisha kupondwa au kuyeyushwa ili kupata sura nzuri ya maisha. Kubali maumivu na kuyastahimili kwa kufanya mambo yaliyoainishwa hapo juu kukuruhusu kutengeneza umbo jipya na bora la maisha yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Asante kwa masomo haya mazuri.
Karibu sana Maureen. Karibu tuendelee kuwa pamoja. Lengo la mtandao huu ni kuhakikisha unaamsha uwezo mkubwa ulio ndani yako kufanya makubwa zaidi ya uliyokwisha fanya.
Je umeshafanikiwa kuweka malengo ya mwaka huu?
Jaribu
Alfred
Kocha & Mwl. wa Uwezo wako halidi