Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuanza Kufikiri Kama Waliofanikiwa Ili Na Wewe Upate Mafanikio Makubwa Kama Yao.
Kila kitu unachoona kinafanyika au kinatokea hapa duniani kinaanza kama wazo. Gari unaloliona lilianza kama wazo. Nyumba kubwa zenye ghorofa nyingi na kupanda juu sana zilianza kama wazo. Mawazo hayo yalitokana na kufikiri. Hivyo ubora wa mawazo ya mtu au watu hutegemea namna wanavyofikiri.
Kufanikiwa au kushindwa, mafanikio madogo au makubwa hutegemeana na namna ya watu wanavyofikiri. Waliofanikiwa wana namna tofauti wanayofikiri na kuendesha maisha yao ambayo walioshindwa hawafikiri hivyo. Kufikiri kwa mtu aliyefanikiwa kunatengeneza mawazo mazuri ambayo baada ya kufanyiwa kazi huzaa mafanikio makubwa.
Si kweli kuwa waliofanikiwa walizaliwa na namna wanayotumia kufikiri, bali wamejifunza wakiwa hapa duniani. Hii inakupa matumaini kuwa hata wewe unaweza ukajifunza namna hiyo na kuanza kufikiri vyema kisha kupata mawazo mazuri ambayo yatakuwezesha kupata mafanikio makubwa. Hivi ndivyo wanaotaka mafanikio makubwa wanafikiri tofauti na walioshindwa au wanaotaka mafanikio ya kawaida;
Haiishii kuishi maisha ya sasa bali na ya baadaye. Walioshindwa au waliopata mafanikio madogo hufikiri zaidi kuhusu maisha ya sasa lakini husahau kuishi maisha ya baadaye. Maisha ya baadaye ni ya muda mrefu ujao kama miaka mitano, kumi, ishirini au hamsini ijayo. Kwa mfano waliotengeneza mafanikio makubwa huweka akiba kwenye kila kipato wanachopata kisha kuwekeza zaidi kwa ajili ya kuja kupata fedha nyingi huko baadaye. Lakini wanaowaza mafanikio madogo huishi kutafuta fedha leo kisha kutumia yote.
Haangalii alivyo sasa bali anavyotaka kuwa. Walioshindwa au wanaotaka mafanikio madogo huwaza tu walivyo sasa. Lakini wanaofikiri mafanikio makubwa huenda mbali zaidi wakifikiri vile wanatamani wawe na kisha kujitengeneza vile wanavyotaka kuwa. Badala ya kuridhika na hali ya uchumi waliyonayo wanafikiri hali ya utajiri wanayotakiwa kuwa kisha wanaweka mipango ili kupata kile wanachokitaka. Unataka uwaje kwenye kila eneo la maisha yako? Pata picha hiyo kisha anza kujijenga kuwa kama unavyotaka uwe.
Hawaridhiki na uwezo walionao bali wanatafuta utaalamu wanaouhitaji. Ili mtu aweze kupiga hatua kubwa anahitaji kuwa na taaluma mbalimbali zaidi ya zile alizo nazo kwa muda huo. Wanaotaka mafanikio makubwa hawaishii kufanya kazi kulingana na taaluma walizonazo muda ule tu bali huangalia ni taaluma gani pia wanahitaji ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Utaalamu huo huwapa uwezo wa kufanya vitu kwa viwango vya juu sana. Ni utaalamu gani unafikiri unatakiwa uupate ili kuweza kupiga hatua kubwa zaidi ya hapo ulipo? Ukishatambua utaalamu huo, nenda kautafute kwa kuhudhuria mafunzo, kusoma vitabu husika au kujifunza moja kwa moja kwa wenye taaluma hiyo.
Hawaishii kuwa kama wanavyotaka kuwa wao bali kile wanachoweza kufanya kwa ajili ya wengine. Wanaotaka mafanikio makubwa wanaamini kuwa hakuna mafanikio yenye maana kama yatakuwa hayagusi au kuboresha maisha ya watu wengine. Hivyo badala ya kujifikiria wao wenyewe tu wanafikiria na watu wengine. Hufikiri ni kitu gani wanaweza kukifanya kikawasaidia watu wengine kupiga hatua? Unaweza kupata chochote kile kama utawapa watu wengine kile wanachokitaka.
Ndugu! Una nafasi ya kupiga hatua kubwa zaidi ya ulipofika sasa. Utaweza kufanikiwa hilo kwa kubadili namna unavyofikiri. Anza kuboresha namna ya kufikiri kwa kufikiri kama wale waliopata au wanaotaka mafanikio makubwa.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz