Ni Wakati Sasa Wa Kutengeneza Toleo Jipya La Maisha Yako.


Categories :

Ni asili ya binadamu kupenda vitu vipya au kufanya vitu vipya. Hii ndiyo siri waliyoing’amua watengeneza bidhaa kama vile nguo, magari au simu. Kila wakati wamekuwa wakitengeneza vitu vipya kwa matoleo tofauti ili kukata kiu ya wateja wao. Tumeshuhudia mtu akinunua nguo mpya si kwa sababu ya zamani imechakaa bali kwa sababu kuna toleo jipya limetoka. Watu wamekuwa si wavumilivu kwenye matoleo mapya, ndiyo maana toleo jipya la kitu chochote linapotoka, biashara hiyo hutoka kwa kasi kubwa. Hii ni kwa sababu watu huwa hawatamani kupitwa na toleo jipya au kuchelewa kupata toleo jipya.

Licha ya watu kuwa na hamu ya kupata vitu vipya lakini wamesahau kuwa na wao wenyewe wanahusika kwenye kutengeneza matoleo mapya. Wanawajibika kutengeneza matoleo mapya ya wao wenyewe. Kila mtu anawajibika kutengeneza toleo jipya la kwake mwenyewe. Mtu binafsi ndiyo kiwanda cha kutengeneza toleo lake jipya. Kitu ambacho huwa kinavutia watu kununua toleo jipya ni kuwa huwa linakuwa limeboreshwa kuliko toleo la zamani. Hivyo hata toleo jipya lako linatarajiwa kuwa bora kuliko la zamani.

Toleo lako jipya si la kubadili rangi yako au kimo chako au uraia wako. Bali toleo lako jipya ni lakubadili hali ya maisha yako kuanzia vile visivyoonekana kama fikra na tabia zako mpaka vile vinavyoonekana kama mali zako. Ndugu! Umekaa kwa muda mrefu sana katika hali uliyonayo sasa, ulipaswa uwe umeshajitoa matoleo mengi sana. Ungekuwa umeshafanya hivyo kwa kujiboresha kwenye kila eneo la maisha yako. Kama kuna eneo la maisha bado upo vilevile licha ya kukaa muda mrefu,  itadhihirisha kuwa wewe bado ni wa zamani hujatoa toleo jipya. Hivi ndivyo unavyoweza kuzalisha toleo jipya la wewe katika maeneo mbalimbali ya maisha yako;

Toleo la kipato bora: Hili ni eneo muhimu sana la maisha yako ambalo inakupasa uwe unazalisha toleo jipya kila wakati. Yaani uwe unakikuza kipato chako. Unaweza kukuza kipato chako kwa kuwa kuongeza vyanzo vya kipato chako. Pia unaweza kukuza kipato chako kwa kuongeza mauzo kwenye biashara ambayo tayari unayo. Tafakari katika eneo hili, Je mwaka jana ulivyoiisha ulifanikiwa kupata toleo jipya?

Toleo la Ustahimilivu: Kadri unavyozidi kukua unatarajiwa kukutana na changamoto kubwa zaidi ya zile zilizopita. Ili kuweza kusonga mbele kwa mafanikio ni lazima ujenge tabia za kukuwezesha kukabiliana na changamoto hizo. Moja ya tabia hizo ni kuwa na uwezo wa kustahimili changamoto hizo. Je unajifunza kwenye kila changamoto unayoipata ili kuongeza kinga ya kuzikabili nyingine zinazokujia. Jitathmini nini ulikifanya baada ya kupata changamoto iliyopita? Kama ulisimama imara na kuendelea na safari basi wewe ni toleo jipya kama sivyo basi wewe bado ni wa zamani na unahitaji kujenga toleo jipya katika eneo hili.

Toleo la uelekeo: Je kadri muda unavyoenda unajiona upo wazi kwenye kile unachokitaka maishani? Je kila siku unapoamka unajua ni kitu gani unaenda kukifanya siku hiyo na ndicho unachoenda kukifanya? Kama bado hujui nini unakitaka maishani mwako kama ilivyokuwa mwaka jana, tambua kuwa bado ni toleo la zamani. Tengeneza toleo jipya katika eneo hili kwa kila wakati kuwa wazi kabisa kwenye kile unachokitaka maishani mwako.

Toleo la ubobezi: Kwenye eneo la maisha ulilochagua kuliishi maishani mwako, huna budi kila wakati kuwa bora zaidi. Unahitaji matoleo mengi sana kulimiliki eneo hilo kwa kuwekeza utaalamu mbalimbali. Huwezi kufikia ubobezi kwa kuendelea kubaki na kile unachokifahamu sasa. Tengeneza mazingira ya kuendelea kujifunza  ujuzi zaidi kwenye eneo lako la ubobezi.

Huwezi kupiga hatua kwa kuendelea kubaki ulipo sasa bila kukua. Mafanikio makubwa huja kwa kuendelea kujitengeneza matoleo mapya kila wakati. Ili uweze kuongeza kasi ya ukuaji wa mafanikio yako huna budi kuongeza kasi ya matoleo yako. Weka mpango leo wa kuhakikisha unatengeneza matoleo mapya mara kwa mara kuzidi kukua zaidi.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi

Mawasiliano;

Simu; 0752206899/0714301952

Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *