Geuza Kushindwa Kuwa  Maandalizi Ya Kushinda


Categories :



Neno kushindwa limekuwa na tafsiri tofauti tofauti miongoni mwa watu. Ni neno ambalo limewazuia watu wengi kutochukua hatua, hata za kuanza. Pia limewazuia baadhi ya watu kutoendelea baada ya neno hili kutafsiriwa vibaya maishani mwao. Kwa watu waliolitafsiri vibaya neno hilo kushindwa limetengeneza ukuta mnene kati yao na mafanikio yao.


Maana sahihi ya neno kushindwa kwenye harakati za kusaka mafanikio ni kuwa njia ulizotumia kupata matokeo tarajia hazijafanya kazi hivyo jaribu kwa njia nyingine. Hivyo kushindwa kunakupa nafasi ya kufanya tena na kuchagua kufanya kwa ubora zaidi. Hivyo kujipa kushindwa hata kabla ya kuanza kufanya kitu ni kujipunja kupiga hatua.

Hakuna mafanikio makubwa yaliyotokea bila kushindwa. Watu wengi unaowaona wamefikia mafanikio makubwa, walipitia kushindwa kwingi. Waliposhindwa hawakuona ni mwisho wa safari, bali ni nafasi nyingine ya kujipanga na kuja kufanya zaidi ya pale waliposhindwa. Jifunze kwa mtoto mchanga anapotaka kusimama au kutembea, huanguka mara nyingi na mara nyingine kuumia lakini huendelea kujaribu mpaka atakapoweza kutembea na kisha kukimbia. Aliyetengeneza taa ya umeme (Thomas Edson) ambayo mwanga wake unaufurahia leo, alijaribu zaidi ya mara elfu moja, lakini hakukata tamaa. Baada ya kushindwa, walitumia nafasi hiyo kufanya maandalizi ya kushinda. Hivi ndivyo unaweza kufanya maandalizi ya kushinda baada ya kushindwa;

Jifunze kutokana na kushindwa kwako. Kama tulivyoona hapo juu kuwa kushindwa kunakupa taarifa ya kuwa kuna kitu ulichokifanya ambacho hakikuwa sahihi. Hivyo baada ya kushindwa unapata nafasi ya kuchunguza makosa uliyoyafanya na kisha kurekebisha. Kumbe kwenye kila unachoshindwa kuna somo la kujifunza na kuwa mwelevu zaidi kuliko mwanzo. Je huwa unachukua hatua ya kujifunza baada ya kushindwa au unalalamika na kukata tamaa?

Boresha kutoka kwenye kushindwa. Kama utakuwa mwaminifu wa kujifunza kila pale unaposhindwa, utazidi kuwa bora zaidi kila unaporudi kukifanya kitu hicho. Itakuwa siyo rahisi kwako kurudia makosa uliyoyafanya mara ya kwanza. Jiandae kushinda kutokana na kushindwa kwako kwa kuhakikisha unarudi ukiwa bora zaidi kuliko ulivyoshindwa.

Endelea baada ya kushindwa. Jiwe kubwa huwa halipasuki kwa kugonga nyundo moja tu. Ingekuwa vigumu sana kupata mawe madogo madogo au kokoto kama mpondaji angekata tamaa na kutoendelea kushusha nyundo baada ya jiwe kutopasuka kwa kupiga nyundo mbili. Ndivyo ilivyo kwenye mafanikio makubwa, huwezi kuyapata baada ya kujaribu mara moja tu. Ukashindwa, fanya tena na kwa ubora zaidi. Usipokata tamaa, ni suala la muda tu kuja kupata matokeo unayoyataka.

Bobea. Kubobea ni kukifahamu kitu nje na ndani kiasi cha kuwazidi wengine kwa mbali sana. Kushindwa kunakupa zawadi hii ya ubobezi. Ukishindwa unapata nafasi nzuri ya kujifunza kitu, hivyo kadri unavyoshindwa mara nyingi ndivyo unavyokifahamu kitu kiundani zaidi. Ndugu kushindwa kwako kunatengeneza safari yako ya kufikia ubobezi. Unaposhindwa jiambie hii ni fursa kwangu ya kufikia ubobezi.

Tengeneza matokeo makubwa zaidi. Baada ya kushindwa andaa maarifa, umakini, nguvu na muda zaidi ya ilivyokuwa kabla ya kushindwa. Hii itakupa matokeo makubwa kadri unavyozidi kulirudia jambo hilo. Watu unaowaona wamebobea kwenye vitu mbali mbali hata sanaa kama kucheza mpira, ni kwa sababu wamefanya hivyo kwa muda mrefu kwa kurudia rudia hata baada ya kushindwa. Usiache baada ya kushindwa bali endelea kurudia na kujiboresha, hii itakuwa njia yako ya kufikia ubobezi.

Kuanzia sasa usitafsiri vibaya kuhusu kushindwa. Pia usirudi nyuma na kukata tamaa baada ya kushindwa. Tambua kuwa hayo ndiyo maandalizi yako ya kushinda tena makubwa. Tafakari mambo uliyoyaachia njiani baada ya kushindwa au uliyokuwa unayaogopa kuanza kwa kuhofia kushindwa kisha jifunze zaidi, weka umakini wako na muda wako ili yakufikishe mwisho wenye ushindi mkubwa.


Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *