Wewe Ndiwe “Boss” Wa Hisia Zako! Kataa Kunyanyaswa Na Hisia Hasi.
Mojawapo ya mahitaji makubwa ambayo mwanadamu huwa anatamani kuwa nayo ni mamlaka ya uthibiti wa hali mbalimbali. Huu ni uwezo wa kuwa juu ya hali yoyote ile, kuweza kuongoza kitu chochote na kikakutii. Mamlaka hii pia, binadamu huitafuta pia ili aweze kuwaongoza binadamu wenzake. Hii imekuwa sababu mojawapo ya watu kuendelea kung’ang’ania madaraka hata pale ilipotakiwa waachie ngazi.
Lakini licha ya jitihada ambazo mwanadamu amekuwa akizichukua ili kupata utawala ya maisha yake, kuna hali moja ambayo imekuwa ikimnyanyasa sana maishani mwake. Hali hiyo ni hisia na hasa hisia hasi. Hisia ni namna unavyojisikia kwenye tukio au hali fulani. Hisia hizo zinaweza kuwa chanya au hasi. Licha ya mapungufu yake, hisia chanya zimekuwa na faida kubwa kwa binadamu na ndizo zinazosababisha maisha ya furaha na afya njema kwa kwake.
Lakini watu wengi wamekuwa hawafaidiki na hisia chanya baada ya hisia hasi kuendelea kutawala maisha yao. Hisia hasi zimekuwa na hasara nyingi kuliko faida. Hisia hasi zinadhoofisha badala ya kuimarisha mwili kwa kuendelea kunyonya nguvu ambazo mtu angetumia kufanya maamuzi sahihi na kupata mafanikio. Pia hisia hasi zimekuwa chanzo cha magonjwa mengi pale zinapoachwa na kukutawala kwa muda mrefu na kukusababishia sonona. Umeshindwa kuishi maisha yako ya furaha na mafanikio kwa kuacha hisia hasi kama hasira, huzuni, hofu nk zikutawale na kufikiri kuna mtu au matukio fulani yatakayobadili hisia hizo. Nina habari njema kwako kuwa wewe ndiwe boss wa hisia zako.
Brendon Burchard kwenye kitabu chake cha High Performance Habits amesema “You are in-charge of how you feel; That is perhaps one of greatest human gift” Akimaanisha kuwa wewe ndio kiongozi wa hisia zako labda hiyo ni miongoni mwa zawadi kubwa alizopewa binadamu. Ni kweli moja ya uhuru ambao mwanadamu umepewa ni kuwa huru namna unavyofikiri na kuhisi. Kwenye tukio lolote hata kama wengi wanaweza kuona linahuzunisha, una nafasi ya kuhisi furaha. Uwezo huo upo ndani yako ni kazi yako kutumia zawadi hii muhimu kuachana na manyanyaso ya hisia hasi na kufaidika na hisia chanya. Hivi ndivyo unavyoweza kuzificha hisia hasi na kuruhusu hisia chanya zitawale maisha yako;
Jikite kwenye hisia chanya. Una mamlaka ndani yako ya kuchagua hisia gani itawale ndani yako. Usiache hisia zako ziwe ‘automatic ‘ yaani yoyote ile itawale bali amrisha akili yako ijikite kwenye hisia chanya kama furaha, amani, upendo, shukrani, msamaha nk. Pale hisia hasi inapokujia kutokana na tukio fulani itafutie mbadala wa hisia chanya mara moja. Kwenye tukio la kuhuzunisha, tafuta kitu gani kinakufurahisha. Utakipata kipo, kwani kila jambo lina pande mbili.
Tarajia matokeo mazuri. Sababu mojawapo ya watu kukaribisha hisia hasi ni kutarajia matokeo hasi kwenye mambo wanayoyafanya. Unapopata nafasi ya kufanya jambo fanya kwa viwango vya juu sana kisha weka matarajio ya kupata matokeo mazuri. Hii itakuondolea hisia hasi kama hofu.
Kuwa mtu wa shukrani. Dunia imejaa mambo mengi sana mazuri. Kwenye kila jambo unalokutana kuna kitu kizuri ambacho unastahili kushukuru kwa ajili ya hicho. Kushukuru kunakaribisha hisia chanya na kujisikia vizuri na kuwa na furaha na nguvu.
Fikiri mazingira mabaya unayoweza kukutana nayo. Huwezi kuzuia mambo mabaya yasitokee duniani. Matokeo mabaya ndiyo yamekuwa chanzo cha hisia hasi kwa kadri mtu atakavyotafsiri. Lakini ili matukio hayo yasikusumbue, fikiri mazingira uliyopo na ona uwezekano wa mambo mabaya kutokea. Unapofikiri kuna jambo baya linaweza kutokea, unapunguza makali ya hisia hasi na maumivu yake. Ndiyo maana kama umemuuguza mgonjwa kwa muda mrefu huzuni ya kifo chake inaweza kuwa ndogo kuliko angekufa ghafla bila ya kuugua.
Uwe makini watu wanaokuzunguka. Mitazamo ya watu wanaokuzunguka wanaweza kuwa sababu ya hisia zinazokuzunguka. Kama umezungukwa na watu wenye hisia chanya kama furaha, upendo, shukrani, msamaha nk muda wote, ni rahisi sana na wewe kuwa na nguvu ya kutawala hisia chanya. Lakini kama watu waliokuzunguka wametawaliwa na hisia hasi kama huzuni, chuki, hasira, visasi nk utakuwa na shida kubwa kutawala hisia zako.
Ndugu! Hisia hasi huchukua nguvu zako, umakini wako na kudhofisha mwili wako. Haya ni mazingira si rafiki kwako kupiga hatua. Lakini shukuru kwa kuwa una zawadi ya kuwa boss wa hisia zako. Kuanzia sasa kataa kuwa mtumwa wa hisia hasi badala yake tumia mamlaka yako kuamrisha hisia chanya kutawala maisha yako. Hapo ndipo utakapokaribisha furaha na mafanikio ya kudumu maishani mwako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz