Jinsi Usivyoweza Kutengenisha Mafanikio Na Maarifa.
Mafanikio na maarifa tungeweza kusema ni kurwa na doto, yaani mama yao ni mmoja. Hivi ni vitu viwili usivyoweza kutenganisha. Mafanikio imekuwa hamu ya watu wengi, lakini wale ambao wamejaribu kuyaacha maarifa nyuma, wameshindwa kupata kile walichokitamani.
Kwa kuyatenga mafanikio, wengi wamashindwa kuishi maisha wanayostahili. Hata mafanikio hayo ambayo mtu ameyapata ni kwa sababu ya tu ya maarifa ambayo ameyapata hata kama hajui. Lakini pia maisha ya watu yamekuwa kwenye hatari kubwa kwa sababu ya kutokuyaunganisha maisha yao na maarifa. Hata vitabu vitakatifu vimeweka msisitizo kwenye kupata maarifa na kuonyesha bayana athari za kutoyapata maarifa hayo. ‘’Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa’’ (Hosea 4:6a). Hii inaonyesha ni kwa namna gani unavyoweza kupata athari kubwa usipo yaishi maarifa kikamilifu.
Licha ya umuhimu huu wa maarifa, lakini kupata maarifa ya kutufikisha kwenye mafanikio tunayoyataka imekuwa ni changamoto kubwa. Licha ya hamu ya kila mtu kutaka mafanikio kuwa la watu wengi, lakini waafirika ndiyo tumekuwa na changamoto kubwa ya kuyapata maarifa kisha kupata mafanikio. Ndiyo maana kuna msemo wa kueleze jambo hili ambao unasema ukitaka umfiche kitu mwafrika hata kama ni fedha basi wewe kiweke kwenye kitabu.
Unaweza kupata maarifa kwa njia mbalimbali kama kwa kwenda shule,kuhudhuria semina, kusikiliza kaseti, pia kujifunza kwa kutazama mtu anavyofanya. Lakini kuna njia moja kubwa ya kupata maarifa ambayo unaweza kuitumia kupata maarifa makubwa kisha mafanikio makubwa, njia hiyo ni kwa kusoma vitabu. Vitabu ni maarifa yanayoishi baada ya kufa. Kupitia vitabu unapata maarifa hata ya watu waliokufa zamani. Kupitia vitabu unapata maarifa ya watu hata walio mbali sana na wewe. Na hivi ndivyo maarifa yanavyoweza kuleta mapinduzi makubwa kwenye mafanikio ya mtu;
Uzoefu. Kuna faida kubwa ambayo mtu anaipata anaposoma vitabu, nayo ni kujifunza makosa aliyekosea mtu mwingine. Kuna watu walishafanya kitu ambacho wewe unakifanya sasa, walifanya majaribio mara kadhaa wakashindwa mpaka walipojua njia sahihi ya kufanya kitu hicho. Hivyo ukisoma vitabu vyao unapata uzoefu bure ambao mtu mwingine alishaugharamikia. Hivi ndivyo unavyoweza kuongeza kasi ya kufanikiwa kuliko kuanza kujaribu kila kitu mwenyewe.
Mtazamo: Matokeo ya maisha unayoyapata sasa ni kwa sababu ya vitendo unavyovifanya sasa. Vitendo huwa vinaamuliwa na mtazamo wa mtu. Mtu hawezi kufanya tofauti na javionavyo vitu. Kibaya zaidi ni kuwa hutaweza kufanya tofauti na sasa kama mtazamo wako hautabadilika. Ndiyo maana Albert Einstein alisema ‘’Wazimu ni kufanya kitu kilekile kwa namna ileile huku ukitarajia matokeo tofauti’’ Njia pekee ya kubadili mtazamo ni kwa kupata maarifa mapya yatakayomfanya afikiri tofauti na kuwa na mtazamo tofauti. Huwezi kutambua kuwa utajiri ni mzuri mpaka upate maarifa mengine yatakayoondoa mtazamo wako wa zamani ulioamini kuwa utajiri ni mbaya.
Hamasa: Maarifa huonyesha historia za watu wengi waliofikia mafanikio makubwa baada ya kuvuka magumu. Huwezi ukajua historia hizo kama hutachukua jukumu la kusoma historia zao ambazo nyingi zimeandikwa kwenye vitabu. Historia hizi huleta hamasa za kuchukua hatua hata pale unapokubwa na magumu. Kama huna maarifa ya kukutia hamasa kuwa unachokifanya kinawezekana ni rahisi sana kukata tamaa.
Mabadiliko ya teknolojia. Ndugu tupo kwenye zama ambayo kasi ya mabadiliko ya teknolojia ni makubwa sana. Ni rahisi sana kuachwa nyuma kama hutakuwa na utaratibu wa kupata maarifa mapya kila wakati. Hakikishi ni kitu gani kipya kinaendelea kwenye biashara yako na kazi yako pia.
Mafanikio unayoyataka yatawezekana kwa kuunganisha na maarifa sahihi. Pia unaweza kuboreha mafanikio uliyoyapata kwa kupata maarifa sahihi na kuyatumia kwenye kile ulichokifanya. Anza leo kwa kutenga muda kidogo hata nusu saa ili uweze kusoma angalau kurasa kumi za kitabu kila siku. Na kila mwezi utasoma kitabu kimoja na vitabu kumi na mbili kwa mwaka; hutabaki kam ulivyo kama utafanikiwa kusoma vitabu hivyo na kuchukua hatua. Kuna vitabu vingi vya bure unavyoweza kupakua mtandaoni moja kwa moja japo vingi ni vya lugha ya kiingereza. Unaweza kupata vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya kiswahili kwa gharama nafuu kwa kupiga simu namba 0752 206 899.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz