Wewe Ndiye Unayeweka Mipaka Kwenye Kiwango Cha Mafanikio Unachotaka.
Ukiiangalia bahari huwezi kuuona mwisho wake. Ukiwa umesimama sehemu ambayo haina vizuizi unaweza kudhani kuwa mwisho wa dunia upo pale lakini kadri unavyosogea ndivyo unavyoona mwisho huo unazidi kusogea pia na kutoweza kuufikia. Kumbe kuna vitu duniani ambavyo si rahisi kuufikia mwisho wake.
Muonekano wa vitu hivyo ndivyo ulivyo kwenye fikra za mtu kwa kutazama mambo. Fikra zako zina uwezo wa kuweka taswira isiyo na ukomo. Lakini uwezo huo upo ndani yako bila kujali kama unautumia au laa.
Ukubwa wa kitu unaoufanya ni sawa na kiwango ambacho umekitengeneza kwenye fikra zako. Hii ni sambamba na kiwango cha mafanikio unachokipata. Kiwango unachokipata ni sawa na taswira ambayo tayari umeijenga ndani kwenye fikra zako.
Wale unaowaona wamepata kiasi kikubwa cha mafanikio walifanikiwa kujenga kwanza taswira kubwa ya mafanikio kwenye fikra zao. Walipofanikiwa kutengeneza fikra hizo, wakatengeneza mipango mikubwa pia iliyoendana na taswira walizokuwa wamezijenga.
Kama unaona unapata upingufu kwenye eneo fulani la maisha, au kuna matokeo unayoyapata hayakuridhishi, utambue kuwa ni kwa sababu ya taswira uliyoiweka ndani ya fikra ndiyo inayokupa matokeo hayo. Kama unataka matokeo ya utaofauti, anza kwanza kujenga taswira ya kitu au kiwango unachohitaji. Yafuatayo ni maeneo unayoweza kuanza kuongeza kiwango cha mafanikio unayoyataka;
Kipato: Kiasi unachokipata kinaendana na kiasi ambacho fikra zako zimekijengea taswira. Kabla ya kuanza kuweka jitihada za kuanza kuongeza kipato jenga kwanza taswira ya kiasi gani unakitaka. Wakati fikra ikikupatia uhuru wa kupanga kiasi chochote, watu wengi wamekuwa wakijipunja kwa kujikea viwango vidogo vya kipato. Weka kiwango kinachokuridhisha na nenda kakifanyie kazi.
Maarifa: Ili uweze kupata mafanikio makubwa huna budi kuwa na maarifa ya kutosha kwenye kile unachokifanya. Kadri unavyoyapata maarifa na kuyatumia ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi kubwa ya kupiga hatua kubwa. Kuna utele wa maarifa zama hizi, ondoa mpaka wa kupata maarifa ili uweze kuwa kwenye nafasi kubwa ya kupata mafanikio makubwa.
Mauzo: Kila anayetafuta mafanikio makubwa lazima awe muuzaji. Unaweza kuuza huduma au bidhaa. Watu wanaofikia mafanikio makubwa ni wale wanaoondoa ukomo kwenye mauzo. Hakikisha unaondoa ukomo kwenye mauzo ili uweze kuwauzia watu wengi uwezavyo na kupata faida kubwa na mafanikio makubwa. Muda wote amini dunia ina utele.
Fursa: Una fursa ya kufanya chochote ukiwa hapa duniani unachokitaka ukiamini kipo. Usione fursa fulani ni ya mtu fulani. Hapana ni yako pia. Ndani yako kuna fursa ya kipekee, ukiusikiliza moyo wako utakuambia ni nini?
Furaha: Usisubiri matukio ili uwe na furaha. Inakupasa uwe na furaha ili mradi tu u hai. Ondoa mipaka ya furaha, furahi kwa sababu bado upo hai. Kuwa na furaha ni hisia ambazo zinakupa nguvu za kufanya mambo makubwa. Furaha huitengenezea akili mazingira mazuri ya kufikiri vyema na kufanya maamuzi sahihi. Furaha huimarisha kinga ya mwili na kuupa mwili nguvu za kufanya kazi kwa muda mrefu. Wewe ni ‘boss’ wa fikra zako, huzuni inapokujia, ibadilishe na furaha.
Kiwango cha mafanikio unachoweza kukipata kipo kwenye himaya yako. Wewe ndiye unayeweka kiwango, usijipunje. Weka kiwango cha kipato ambacho unakitaka ndipo uanze kuweka nguvu za kutosha kupata kiwango hicho. Kuanzia sasa, furahi tu kwa sababu bado u hai wala usisubiri matukio. Ndipo mwili na akili yako vitakapokuwa tayari kukupa kiwango chochote cha mafanikio unachohitaji.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz