Usiahirishe Mpaka Kesho Kama Hutamani Ufe Kabla Hujalifanya Jambo Hilo.


Categories :

Maisha ya mwanadamu ni muda. Ukishakufa muda wako wa maisha unasishia hapo. Mwanadamu upo hapa duniani kwa muda maalumu kukamilisha kazi maalumu. Ni kipindi cha uhai wako tu ndipo unaweza kutengeneza thamani yako hapa duniani ambayo itaendelea kukumbukwa hata baada ya kufa kwako.

Muda wa maisha yako umegawanyika sehemu tatu, ulipita, uliopo na ujao. Muda uliopita huna uthibiti nao kwani huwezi kubadili chochote kwenye yale yaliyokwisha pita bila kujali unayapenda  au unayachukia. Muda mwingine ulionao ni uliopo, yaani sasa. Huu ni muda wako wa kujidai ambao una uhakika nao wa kufanya kitu chochote unachotamani ukikamilishe kabla ya kufa. Huu ndiyo muda wa thamani sana kwako. Muda mwingine wa maisha yako ni muda ujao. Huu ni muda ambao bado hujaugusa, na ambao huna uhakika nao. Watu wengi huuishi muda huu kwa imani.

Kuna mambo ambayo naamini yapo ndani yako ambayo unawiwa kuyakamilisha kipindi cha uhai wako . Haya ni mambo ambayo usingependa ufe kabla hujayakamilisha. Haya ni mambo yanayohusu maisha yako ya ndani. Haya ni mambo ambayo ni deni ambalo unatakiwa ulilipe kabla hujaondoka duniani. Haya ni mambo yanayohusu kusudi lako na ndoto yako. Kumbuka kusudi lako na ndoto zako zinatimizwa kwa malengo. Kumbe haya ni mambo ambayo ulijipanga kuwa utayafanya kila siku. Ili uwe na uhakika wa kufanya mambo haya huna budi kuyakamilisha kwenye muda ambao una uhakika nao ambao ni leo.

Kuna tabia moja ambayo imesababisha watu kutokupiga hatua. Hii ni tabia ambayo imewafanya watu kufa wangali dunia inawadai. Tabia hiyo ni ya kuahirisha mambo. Imani ya kusema kesho ipo imewaponza wengi, ni kweli kesho ipo lakini inaweza isiwe ya kwako. Kuna uwezekano wa maisha yako yakaishia leo, je utakufa ukiwa na furaha kuwa umekamilisha mambo ambayo ulikuwa unatarajiwa kuyafanya au utakufa ukiwa na huzuni kwa kuwa hujaweza kukamilisha kile ulichotarajiwa?

Njia pekee ya kuyatendea haki maisha yako ni kuishi leo kikamilifu. Pangilia siku yako kufanya vitu vile ambavyo ni muhimu kwenye maisha yako na hakikisha unakamilisha kama uliyoyapanga. Usiingie kwenye mtego wa kujifariji utafanya kesho, haipo mikononi mwako na pia huna uhakika nayo.

Kila siku asubuhi jiulize mambo gani unataka kuyakamilisha yanayogusa hitaji lako la maisha yako? Jambo gani ukilifanya litagusa na kuboresha maisha ya watu wengine? Je kuna sababu yoyote ya kuendelea kunung’unika, kulalamika , kuhuzunika, kutosamehe na mengine yanayofanana na hayo? Chagua mambo mema na yenye thamani ya kufanya siku hiyo na hakikisha unayafanya bila kusubiri kufanya kesho.

Kumbuka kuna mambo uliyoyaahirisha miaka mingi au siku nyingi kwa kusema nitafanya kesho. Makala hii ina ujumbe kwako wa kukaa na kutafakari kuwa licha ya makosa uliyoyafanya, umepewa nafasi nyingine leo. Umeahirisha vya kutosha, anza kuyafanya leo, usisubiri tena kesho. Yafufue mambo yako ya muhimu uliyoyaua siku nyingi kwa kusema utafanya kesho.

Og Mandino alisema  “Work as though you would live forever, and live as though you would die today. Go another mile!” Akimaanisha kuwa fanya kazi kama vile utaishi milele na ishi kama vile unakufa leo, nenda mbali zaidi. Mandino bado anasisitiza namna unavyoweza kuiishi leo kikamilifu. Kila siku tamani kufanya kwa ubora na kwa viwango vya juu zaidi ya jana. Kuna uwezo ambao bado upo ndani yako, leo ndiyo siku ya kuutumia nenda mbali zaidi kwenye yale unayoyafanya.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *