Mafanikio Yako Yapo Kwenye Vitu Usivyopenda Kuvifanya.


Categories :

Mbio za kutafuta mafanikio zimekuwa ni ndefu tena ngumu sana. Watu wanavuja jasho hata damu ili kuyapata mafanikio. Watu wanapanda milima na mabonde ili kuyatafuta mafanikio. Watu wanasafiri umbali mrefu kwa lengo la kutafuta mafanikio. Watu wengine wanafanya hata mauaji kwa lengo la kupata mafanikio.

Licha ya jitihada zote hizo zinazofanywa na binadamu lakini mafanikio yamekuwa yakiwakimbia watu. Yaani imekuwa kama kukimbiza kipepeo, ukimsogelea kwenye ua hili ili umshike anarukia ua jingine. Hii imesababisha watu wakate tamaa na kuona basi waliofanikiwa wana bahati fulani ambayo wasiofanikiwa hawana. Mafanikio yako wapi sasa?  Mafanikio yako yapo upande mwingine, yaani kwenye vitu usivyopenda kuvifanya.

Katika maisha yako kuna vitu ambavyo umekuwa unapenda kuvifanya, bila kujali thamani yake. Mafanikio ni matokeo ya visababishi. Thamani ya kisababishi ndiyo inayoamua ni kiasi gani cha mafanikio uyapate. Vitu vingi wanavyopenda watu ni vile vyenye thamani ndogo, ni vile ambavyo havina maumivu yoyote. Hivi ni vitu unavyoweza kufanya kimazoea, yaani ukafanya kama ulivyofanya jana bila ya  hata kuumiza kichwa au kukutana na hali zinazokutoa kwenye eneo lako uhuru.

Kwa mfano kisababishi cha kuongezeka mauzo ni kuongeza wateja au manunuzi. Kama wateja wako watabaki wale wale  na kununua kwa kiasi kile kile usitarajie kupata mauzo zaidi ya yale uliyoyazoea. Hatua ambayo mfanyabiashara aliyotakiwa kufanya ni kutafuta wateja zaidi waje wanunue na kupata mauzo zaidi. Kazi ya kutafuata wateja na hasa wale wasiofahamika si jambo rahisi na halipendwi na wafanyabiashara wengi. Lakini hili ndiyo jambo ambalo linaweza kukupa mafanikio makubwa zaidi ambayo hujawahi kuyapata.

Ili uweze kupata mafanikio makubwa, mara nyingine inakubidi kuchukua hatua za hatari. Hizi ni hatua ambazo huna uhakika wa asilimia nyingi  na matokeo yake. Watu wengi huwa hawapendi kuchukua hatua za hatari na hivyo kuamua kuendelea kufanya vitu vile walivyo na uhakika navyo. Kwa kufanya hivyo hawapati matokeo ya tofauti. Albert Einstein alikiita kitendo cha mtu kuendelea kufanya kitu kwa namna ile ile huku akitegemea majibu tofauti kuwa ni wazimu. Vifuatavyo ni miongoni mwa vitu usivyovipenda kufanya lakini ndiko mafanikio yako yalikojificha;

Kukataliwa. Neno HAPANA ni miongoni mwa maneno ambayo watu wengi hawapendi kuyasikia. Watu wengi wanapenda kusikia neno ndiyo. Kwa kuwa na mapenzi na neno ndiyo, wanaamua kufanya vitu ambavyo wana uhakika wataambiwa ndiyo. Kuna mafanikio makubwa kwenye hapana. Mara nyingine unajiwekea hapana mwenyewe lakini uhalisia wake ni ndiyo. Wauzaji mashuhuri na watu wenye mafanikio makubwa ni wale ambao hawakuogopa hapana na hivyo wakaambiwa hapana mara nyingi kabla ya kupata ndiyo nyingi zaidi ya hapana.

Presha’ ya kiuchumi. Moja ya presha ambazo watu wengi huwa wanakwepa kukabiliana nazo ni presha inayohusu fedha. Kwa mfano hata kama una kipato kidogo, huna budi kuweka akiba ili uweze kupata mtaji zaidi wa kuwekeza na kupata fedha zaidi. Kuanza kuweka akiba inakuhitaji ujinyime baadhi ya matumizi uliyozoea kuyafanya. Hii ni changamoto kwa watu wengi. Na kwa sababu hawapendi kujinyima wanakwepa kufanya hili.

Kutokukata tama. Kinyume cha kutokukata tamaa ni kuendelea na kile unachokifanya hata kama hupati matokeo unayoyatarajia kwa muda huo. Watu wengi wameshindwa kupata mafanikio kwa sababu ya kuacha kufanya bila kujua walikuwa wanakaribia kupata matokeo. Wale waliofanikiwa wamejenga tabia hii ya kutokuacha kufanya kitu mpaka wamepata matokeo.

Ndugu huu ndiyo muda wa kuanza kufanya vitu usivyovipenda ili upate mafanikio ambayo umekuwa ukihangaika huku na kule bila kuyapata. Anza na haya matatu. Moja, kama unaamini kitu unachokifanya ni cha thamani, usiogope neno hapana hata kama ukiambiwa mara nyingi kiasi gani, mwisho wa siku hapana itakuwa ndiyo. Mbili , kabiliana na presha ya uchumi unapoendelea kutafuta uhuru wako wa kifedha. Acha baadhi ya starehe na weka akiba. Tatu, kama upo kwenye njia sahihi usiache safari yako mpaka umefika.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

2 thoughts on “Mafanikio Yako Yapo Kwenye Vitu Usivyopenda Kuvifanya.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *