Hata Kama Ni Adui Yako, Jifunze Hekima Hii Kutoka Kwake.
Kitabu kitakatifu (Biblia) kinamueleza nyoka kuwa ni mnyama mwerevu kuliko wengine. Huyu ndiye aliyefanikiwa kumdanganya Eva ili wale matunda ya mti wa katikati waliyokuwa wamekatazwa na Mungu. Alijenga hila hii kwa kubadilisha fikra za mwanadamu. Hiki ndicho kilikuwa chanzo cha mwanadamu kuanguka katika dhambi.
Baada ya nyoka kufanya kosa hilo Mungu akamlaani kuliko wanyama wengine wote na kumpa adhabu ya kutembelea tumbo maisha yake yote. Pia Mungu aliweka uadui kati ya nyoka na mwanadamu kwa makosa waliyoyafanya: Mwanadamu amponde kichwa akimkuta nyoka na yeye nyoka amgonge mwanadamu kisigino. Hivyo bado kuna uadui kati ya mwanadamu na nyoka.
Licha ya uadui uliopo kati ya nyoka na binadamu, kuna hekima au werevu ambao mwanadamu anaweza kujifunza kutoka kwa nyoka na kumsaidia kupiga hatua zaidi. Iko hivi ndugu yangu, nyoka ana tabia ya kujivua gamba lake la nje kila baada ya muda fulani. Inaelezwa sababu za kujivua gamba hilo ni kuruhusu ukuaji. Mwili wake unapokua na gamba la zamani hubaki kwenye umbo la zamani na hivyo kuzuia mwili wake kuongezeka kirahisi. Hivyo hujivua gamba mara kwa mara ili kuruhusu mwili wake kuongezeka.
Sababu nyingine ya nyoka kujivua gamba inasemekana ni kuwatoa vimelea vya magonjwa na wadudu wengine ambao wanaweza kumdhuru ambao wanakuwa kwenye gamba hilo. Hivyo huvua gamba la zamani ambalo ni chafu na kubakia na gamba jipya ambalo ni salama zaidi kwake. Hapo kuna mambo mawili mkubwa sana ambayo wewe kama mwanadamu unaweza kujifunza kwa adui yako na yakaboresha sana maisha yako.
Moja; Nyoka anapovua gamba ili kuruhusu ukuaji wewe vua tabia zote zinazozuia ukuaji wako. Kuna tabia unazoziishi zinazokufanya uendelee kubaki ulipo kwa muda mrefu. Miongoni mwa tabia hizo ni kuridhika na ulicho nacho, yaani kuona unafahamu kila kitu na huhitaji tena maarifa, hutakua kimafanikio kama hutakua kimaarifa kila siku. Tabia nyingine zinazokuzuia usikue ni kama kutoweka akiba, kutoweka malengo, kuacha hisia zikutawale nk. Hizi ni baadhi ya tabia ambazo inabidi uzivue mara moja ili kuruhusu ukuaji wa mafanikio yako.
Mbili; Nyoka anapovua gamba ili kutoa vimelea vya magonjwa na wadudu wengine hatari kwako, wewe inabidi uwe unavua marafiki na watu wengine ambao sio msaada kwako. Hawa ni watu ambao badala ya kukusaidia kukua, wanakurudisha nyuma na kuhatarisha maisha yako. Kumbuka mafanikio yako ni wastani wa mafanikio ya watu watano wanaokuzunguka. Watu unaokaa nao kwa muda mrefu wana athari kubwa kwenye hatima ya maisha yako. Changuza rafiki zako kama wanaweza kukusaidia kutoka hapo ulipo na ukaenda hatua nyingine ya juu zaidi. Kama Hapana huna budi kuwavua kama nyoka anavyochukua jukumu la kuvua gamba lenye wadudu.
Umeona ndugu! Licha ya uadui ambao unao na nyoka lakini kuna hekima unayoweza kujifunza kwake. Hii inadhihirisha kuwa huwezi ukakosa kitu cha kujifunza kutoka kwa kila mtu au mnyama. Ukijiandaa kwa nia ya kujifunza kutoka kwa mtu, utapata vitu vya kujifunza. Leo chukua jukumu la kujifunza kutoka kwa nyoka. Anza leo kwa kuanza kuacha tabia zile ambazo hazikufanyi ukue kama tulivyoainisha hapo juu, Kisha badilisha tabia hizo na zile nzuri ambazo zitaruhusu ukuaji wako. Tabia za ukuaji ni kama njaa ya maarifa, kuweka malengo, kuchukua jukumu la maisha yako n.k.
Pia chukua jukumu la kuangalia watu unaokaa nao muda mrefu, wanakujenga au wanakubomoa? Kama wanakubomoa wavue haraka iwezekanavyo na vaa wale anakusaidia kupiga hatua.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz