Hii Ndiyo Sababu Ya Kwa Nini Kila Pampu Yako Haitoi Mafanikio.
Kuna kijiji kimoja kilichokuwa na ukame mwingi na hivyo kufanya kuwana shida ya maji. Watu walilazimika kutembea umbali mrefu ili kupata maji. Baada ya kilio hicho cha siku nyingi ufadhili ulipatika ambapo kuna shirika moja lilijitokeza na kutoa msaada wa kuchimba visima na kuweka pampu za mkono za kuvutia maji kutoka chini. Pampu hizo ziliwekwa mitaa mbalimbali ya kijiji hicho ili kurahisisha upatikanaji wa maji hayo.
Baada ya zoezi hilo kukamilika watu wa kijiji hicho walifurahi sana baada ya kutatuliwa shida iliyowakamata kwa siku nyingi. Kutokana na shangwe hiyo jamaa moja alitoka mbio nyumbani ili kwenda kisimani ili awe wa kwanza kupata maji. Alifika kwenye kisima kilichokuwa karibu na kuanza kupampu. Alianza kupampu kwa msisimko na alipopampu mara nne na kuona maji hayatoki akashangaa sana na kughadhabika sana huku akisema ni kitu gani kilichofanyika! Aliamua kwenda kisima kingine kwa hasira na kupampu mara nne tena bila mafanikio. Alienda kwenye visima vitano na kufanya hivyo hivyo bila mafanikio.
Akiwa bado yupo kwenye kisima cha mwisho, mama mmoja alikuja na kuanza kupampu maji, jamaa yule akawa anamtazama kwa dharau huku akiongea kimya kimya kuwa mama yule anajisumbua tu. Mama alipumpu mpaka zaidi ya mara nne na hata pale maji yalipokuwa hayatoki aliendlea kupampu tu, ilipofika mara ya sita maji yakaanza kutoka kwenye lile bomba. Ndipo yule jamaa alipoweka mikono yake kichwani na kushangaa sana kile alichokuwa anakosea yeye kutopata maji licha ya kutembea visima vingi.
Na wewe unaweza kuungana na huyu jamaa kushangaa ni nini kilikuwa kinatokea. Hiki ndicho kilichotokea. Yule jamaa alipokuwa anaanza kumpampu maji yalikuwa yanaanza kupanda lakini kupampu mara nne tu kulikuwa hakutoshi kufikisha maji kwenye mdomo wa bomba. Lakini kitendo cha kuacha kupampu, maji yote yaliyokuwa njiani yalikuwa yanarudi chini. Lakini kwa sababu mama Yule aliendelea kupampu bila kuacha maji yale yaliendelea kupanda mpaka yakafika mdomoni mwa bomba.
Kilichomtokea jamaa huyo ndicho kinachotokea kwenye maisha yako sasa. Mara ngapi umeanzisha jambo na kulifanya kidogo tu huku ukitegemea matokeo ya haraka na yalipochelewa ukaacha kuweka jitihada? Ni mara ngapi umeanzisha biashara baada ya kuambiwa inalipa, ulipoifanya kwa muda mdogo tu na kuona mauzo ni kidogo ukaamua kuacha na kuanzisha nyingine uliyoambiwa inalipa zaidi?
Mara nyingi huwezi ukaanzisha kitu na kupata matokeo hapohapo, lakini matokeo yanakuwa yapo njiani yakiendelea kujikusanya kadri unavyoweka nguvu. Lakini kwa kuacha kufanya jambo hilo, hata yale matokeo yaliyokuwa yanakaribia kuja yanayeyuka na kupotea. Umepoteza nguvu, muda na umakini wako kwa sababu ya kuhangaika na fursa mpya badala ya kutulia na moja.
Wakati umefika sasa wa kutafakari baada ya kuchoka kwa kuhangaikia fursa, chagua kitu kimoja ambacho unaamini matokeo yake yatakuvusha mbali kisha komaa na hicho kitu mpaka upate matokeo. Usihangaike na vitu vingine, bali komaa mpaka kieleweke. Ni biashara gani unapanga kukomaa nayo mpaka ikupatie mafanikio mkubwa? Ni uwekezaji gani unaamua kuufanya mpaka ukupe uhuru wa kifedha? Ni mahusiano gani unaamua kubaki nayo na kuzidi kuyaimarisha zaidi? Usihangaike kukimbia kutoa kisima kimoja kwenda kingine, endelea kupampu mpaka mafanikio yako yatokee kwenye bomba lako na kumwagika.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz