Huwezi Kung’aa Kwa Kupaka Mafuta Taswira Yako Unayoina Mbele Ya Kioo.
Ukisimama mbele ya kioo cha kujitazamia utajioni jinsi ulivyo. Hata chochote utakacho kuwa unafanya wewe, taswira yako pia itakuwa inakifanya. Ukitabasamu na taswira yako itatabasamu, ukinuna kadhalika taswira yako itanuna. Kwa hiyo chochote utakachokuwa unafanya wewe na taswira yako itaitikia.
Lakini kitu cha ajabu ni kuwa ni taswira itakayokuwa inakuitikia kile unachokifanya na kamwe taswira haiwezi kuanzisha kitu chochote na wewe ukaitikia. Hivyo kipi taswira yako ikifanye kinategemea wewe utakuwa unafanya nini. Hata kama taswira yako itakuona unataka kuondoka ukiwa umesahau kupaka mafuta uso wako, haiwezi kukukumbusha. Hii inaashiria kuwa taswira ipo kwa sababu wewe upo. Itatokea kama wewe utatoke. Hivi ndivyo ilivyo katika maisha yako ya mafanikio, lazima wewe ufanye kitu kabla mafanikio yako hayajakufikia.
Umekuwa na hamu ya kupata mafanikio makubwa katika maisha yako. Mara nyingine umefikiria kuwa mafanikio hayo yapo sehemu fulani, ni ya kuchukua tu. Mara nyingine umefikiri kuwa mafanikio yako yameshikiliwa na mtu fulani kwamba siku akiwa mwema akakuachia basi yatakufikia mara moja. Kumbe mafanikio yako hayo unayoyataka yanatokana na kile unachokitoa wewe. Mafanikio yana kisababishi na kisababishi hicho ni thamani unayoitoa kwa wa watu wengine.
Kuna huduma au bidhaa ambayo inawapa thamani wengine na wapo tayari kukulipa. Hivi ndivyo unavyoweza kupata mafanikio. Ni thamani gani unaitoa sasa kwa watu wengine? Kitu gani unauza na watu wengine wapo tayari kukulipa?
Kiwango cha mafanikio unachoweza kupata kinategemea na thamani unayotoa kwa watu wengine. Ni sawa taswira yako mbele ya kioo, ukitaka itikisike kwa nguvu kubwa huna budi wewe kwanza kutikisika kwa nguvu. Wewe ndiye mwenye uwezo wa kubadilisha matokeo. Kama kuna hali fulani haikufurahishi, basi wewe ni mtu wa kwanza kuchukua hatua ya kuibadili vinginevyo itabaki vile vile. Kama changamoto ni umasikini, utabaki vile vile mpaka pale utakapochukua jukumu la kukabiliana nao. Kama shida ni kipato kidogo kisichokidhi, kipato hicho kitaongezeka utakapoongeza thamani unayoitoa kwa watu.
Hatua za kuchukua
Mosi; Kama huna thamani yoyote unayowapa watu ili wakupe mafanikio, ni wakati sasa wa kutafuta bidhaa au huduma ambazo zitatatua changamoto za watu na kisha kisha watu kuwa tayari kukulipa. Kuna changamoto au matatizo mengi yanayowakabili watu. Ili kuweka thamani ambayo watu watakuwa tayari kukulipa ni lazima ufanye tathmini na kutambua shida walizonazo watu. Usianze biashara aua huduma ndipo uanze kutafuta wenye shida, bali anza na uhitaji kisha leta huduma au bidhaa zitakazotatua shida za watu.
Pili: Kama tayari unatoa thamani kwa watu lakini mafanikio yamekuwa kidogo, ni wakati sasa wa kuhakikisha unaongeza ubora wa huduma au bidhaa unayoitoa ili kuongeza thamani na watu kuwa tayari kukongezea mafanikio. Bado una nafasi ya kuongeza ubora wa huduma unayoitoa, bado unaweza kumkarimu mteja zaidi ya pale unapofanya. Unaweza ukaongeza idadi ya huduma unazozitoa zikawa nyingi zaidi na thamani yake ikaongezeka zaidi.
Ndugu! Hakuna mafanikio yatayokuja yenyewe. Hakuna mtu atakayeleta mafanikio yako. Mafanikio yako yapo mikononi mwako, lakini yansubiri wewe ufanye kitu, ambayo ni thamani. Usisubiri taswira yako ikupake mafuta, bali wewe ndiye mwenye uwezo wa kujipaka mafuta na taswira yako ikang’aa sana.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz