Unayaumiza Macho Yako Bure! Tumia Akili Kuona Gizani.


Categories :

Mtu ambaye ameshapita barabara fulani mara nyingi bila kupotea, ana uwezo wa kurudi nyumbani hata usiku wa manane kukiwa na giza nene bila ya kupotea. Dereva ambaye ameshaendesha gari kwenye barabara fulani, si rahisi kupata ajari au kuingiza gari kwenye makorongo ya barabara hiyo kwani anakuwa anaifahamu barabara hiyo vizuri sana. Pia kwa sababu dereva huyo anakuwa amenoa macho yake, la hasha kwa sababu kuna kitu kingine wanachotumia kuona.

Njiwa wa kufungwa aliyekaa na kuizoea nyumba yako hata umweke kwenye sanduku lenye giza na kumsafirisha maili nyingi sana kutoka nyumbani kwako na kumuachia huko, ni suala la muda tu atarudi tena nyumani kwako. Nini kinamrudisha tena nyumbani, alikuwa anaona na nini wakati anasafirishwa? Huu ni muujiza eh!

Hii ni nguvu ambayo na wewe unayo, unayoweza kutumia kuona gizani na kufika sehemu ya maisha unayotaka kufika. Lakini imeshindikana kwa sababu umekazana kutumia macho yako kuona gizani macho yako yanaumia na kushindwa kuona njia sahihi na kupotea njia. Huwezi ukafika unakotamani kufika maishani mwako kama utakuwa huoni kwa akili yako na kusikiliza kwa moyo wako. Hii ni nguvu ya maono ambayo akili yao inaanza kuona baada ya kuusikiliza na moyo wako pia.

Maisha ya duniani yamejaa vitu vingi vinavyosimama katikati yako na mafanikio unayoyataka. Umekuwa ukizunguka upande mmoja tu ambako upo bila kuona hata mwanga wa kule unakotarajia kuwa ni kwa sababu umekosa maono. Macho yako yanaona vitu vingi sana, na sio vya kwako.  Kwa sababu mpaka sasa akili yako haijaona kile unachokitaka, macho yako yameendelea kuona giza mbele yake na kuzidi kuumia.

Imefika wakati unasema unaona giza mbele yako kwa sababu akili na moyo wako hujavipa vitu vya kuona wazi. Akili yako haina budi kuona ndoto yako. Unayaonaje maisha yako baada ya miaka mitano, kumi, ishirini ijayo? Kuna kitu gani kinachokuja na kutawala akili yako kila mara? Kitu gani unatamani kuona ukikitimiza kabla hujafa? Je akili yako inaona ukiwa umefikia uhuru wa kifedha baada ya miaka kumi ijayo? Je akili yako inaona ukiwa kiongozi mkubwa wa nchi au taasisi fulani baada ya miaka ishirini ijayo? Akili yako inaona nini?

Maisha yako ya mafanikio makubwa yatatengenezwa na maono ya maisha yako ambayo yatatawala akili yako na kuaminiwa kwa moyo wako kuwa yatatokea. Tengeneza ndoto kubwa ya maisha yako kwani tayari una uwezo mkubwa ndani yako wa kutimiza ndoto yako. Ndoto huchukua muda mrefu kutimia, hivyo usipoteze muda mrefu kuishi ndoto ndogo. Akili yako ikifanikiwa kutawaliwa na ndoto yako kuna uwezekano mkubwa wa kupata kile unachokitaka.  Napoleon Hill alisema “What the mind of man can conceive and believe, it can achieve.” Akimaanisha kuwa chochote ambacho akili itakipokea na kuamini itakipata. Ni vigumu kupata kitu kile ambacho akili yako haikioni, kwani bila akili macho yako yataona giza tu kwenye jambo hilo.

Kaa chini na tafakari ni kitu gani unataka kukitimiza kipindi cha uhai wako wa hapa duniani? Tengeneza maono hayo kisha ujikumbushe mara kwa mara kwa kuyasema na kuandika mpaka akili yako iamini. Weka mipango ya kuanza kuyatekeleza na stahimili mpaka upate matokeo yake. Haya ni maono yako, na wengine hawaoni usikatishwe tamaa na mtu asiyekiona unachokiona.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *