Fahamu Leo Yalikojificha Mafanikio Yako Ya Kweli.
Mafanikio umekuwa wimbo wa watu wengi hapa duniani. Kila mtu anatamani afikie mafanikio makubwa ambayo yangempa ridhiko. Lakini kwa bahati mbaya ua nzuri mafanikio yenyewe yamejificha. Hii inathibitishwa kwa watu wengi kuendelea kutafuta mafanikio hayo kwa nguvu na muda mrefu bila kuyapata. Watu wameishia kukata tamaa wakiamini kuwa waliofanikiwa wana bahati fulani ambayo watu wengine hawana. Mafanikio yamejificha wapi ili watu waende wakachukue huko?
Mafanikio makubwa yanapatikana kama dhahabu inavyotafutwa. Mchakato wa kuichimba dhahabu ni mrefu sana na wenye hatua nyingi na ngumu ili kuifikia na kuipata dhabahu hiyo. Kwa sababu hiyo, dhahabu ni miongoni mwa madini yenye thamani kubwa sana na thamani hiyo imekuwa ikipanda kila siku. Jinsi dhahabu inavyopatikana inatoa somo kubwa sana la jinsi unavyoweza kupata mafanikio yako makubwa ya maisha yako;
Ni vigumu kutengeneza dhahabu. Tofauti na madini mengine, ni vigumu sana kutengeneza dhahabu kutoka kwenye chembechembe nyingine. Licha ya zoezi hilo kuwezekana, lakini gharama yake ni kubwa sana kiasi cha kutoweza kuiuza ukilinganisha na ile ya asili. Hivyo watu huchagua kuipata kiasili kuliko kuitengeneza. Hii inaonyesha kuwa mafanikio yako yapo kwenye asili yako. Asili yako ni upekee wako. Mafanikio yako yanapatikana kwenye upekee wako. Usihangaike kutafuta mafanikio kwa watu wengine bali chimba ndani yako kupata mafanikio yako ya kweli na makubwa.
Maeneo inapopatikana dhahabu ni machache. Kuna maeneo machache sana duniani inakopatikana dhahabu, ndiyo maana si rahisi kuona watu wakichimba sehemu yoyote ile kuipata. Hii pia ndiyo inayofanya thamani yake kuwa kubwa mno. Mafanikio yako yamejificha kwenye uadimu wako. Kuna kitu unacho, ambacho si kazi rahisi kukipata sehemu nyingine. Yamkini dunia imekuwa ikitafuta kila siku lakini hawakipati, lakini kipo kwako. Siku ukitambua uadimu wako, dunia itakuwa tayari kununua thamani yako kwa gharama kubwa. Nini unafikiri unacho ndani yako na hukuoni duniani? Anza kukionyesha hicho.
Ni viguu sana kuchimba dhahabu. Kuichimba dhahabu kwenye maeneo yake ya asili ni kazi ngumu sana. Kuna kutoa jasho kubwa sana mpaka kuipata. Itakuhitaji kupasua miamba mingi na migumu sana ili kuitafuta ilipo. Itakuhitaji kuchimba mashimo makubwa na mrefu sana ili kupata kipande kidogo tu cha dhahabu. Inakuhitaji usikate tama ili uweze kuipata. Licha ya thamani kubwa uliyonayo ndani yako, unahitaji kuweka nguvu kubwa ili kuweza kutoa thamani uliyonayo na watu kuwa tayari kuilipia. Hata pale utakapojua nini unacho ndani yako, utahitaji kuweka kazi kubwa na kuvumilia ili kuweza kutoa ulicho nacho na kupata mafanikio makubwa.
Dhahabu hupatikana ikiwa imejificha. Dhahabu hupatikana ikiwa imejificha kwenye miamba mingine migumu. Hivyo licha ya kuchimba kwa shida na kupasua miamba bado dhahabu imeendelea kujificha mbali zaidi. Ni hatua nyingi utazihitaji ili kuifikia dhahabu ilipo. Ndugu umekuwa ukihangaika kujua mafanikio yako yalipo, inawezekana umekuwa ukiwaangalia watu na kujifananisha nao huku ukifikiri mafanikio yako yapo kwao. Mafanikio yako yapo ndani yako. Mwili na moyo wako vimekumbatia mafanikio yako. Unahitaji utulivu ili kuiingia ndani yako na kujisikiliza nini umekibeba. Usihangaike kwenda kuchimba mbali, chimba mafanikio yako ndani mwako.
Kwa mfano huu wa dhahabu utakuwa sasa umefahamu kuwa kumbe ulikuwa unajisumbua kwenda mbali kutafuta mafanikio yako makubwa na ya kweli. Mafanikio yako ni kitu adimu kilichojificha ndani yako ambacho dunia inakitafuta sana. Siku utakapoanza kukitoa kitu hicho itakuwa tayari kukulipa thamani kubwa. Anza sasa kuchimba ndani yako huku ukijiuliza nini cha thamani umekibeba. Ukipata jibu, weka kazi kubwa kuhakikisha unakitoa huko kilikojificha.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz