Hii Ndiyo Sababu Inayokufanya Usifike Kila Safari Unayoianzisha.
Dereva anapoliwasha gari kutoka nyumbani na kuliingiza barabarani anakuwa na uhakika wa kufika safari yake. Lakini kama dreva huyo akifika kwenye tuta la barabarani na kusimama pale bila kuendelea na safari, hakutakuwa na muujiza wowote wa yeye kufika safari hiyo. Kadhalika akiamua kugeuza gari kurudi nyumbani akiogopa tuta la barabara hataweza kufika safari yake.
Haya ndiyo mazingira yalikufanya usifike safari zako za kusaka mafanikio kwa muda mrefu. Maisha ni safari utakamilisha safari hiyo ukifikia malengo uliyonayo. Kuna safari nyingi ulizozianzisha kupitia malengo yako, lakini ulipokutana na matuta, kuna muda uliamua kusimama na kubakia hapo hapo bila kupiga hatua yoyote. Lakini kuna muda ulipoona tuta ukageuka nyuma na kurudi nyumbani. Hii ndiyo sababu iliyokufanya uyakose mafanikio kwa muda mrefu licha ya malengo ambayo umekuwa ukiyaweka kila siku.
Matuta ya barabara yako ya mafanikio ni vikwazo ambavyo daima husimama mbele ya malengo yako na mafanikio yako. Unapokutana na vikwazo hivyo unafanya nini? Changamoto/vikwazo kwenye safari ya mafanikio haviepukiki. Ili uweze kufika safari yako huna budi kuvikabili vikwazo hivyo badala ya kuvikimbia. Wale waliofanikiwa, walipokutana na vikwazo hawakurudi nyuma na kuahirisha safari wala hawakubaki wamesimama pale wakilalamika kwa nini vikwazo vimekuja, badala yake walichukua hatua ya kukabiliana na vikwazo hivyo kisha wakaendelea na safari.
Muda umefika kwako wa kuhakikisha unafika safari uliyoianzisha na sio kuishia njiani. Ukifanikiwa kuweka malengo tarajia kukutana na vikwazo katika kuyatimiza. Ukitarajia kukutana na vikwazo, hutashangaa kama ukiviona njiani. Kwenye kila kikwazo unachofikiria kinaweza kujitokeza andaa namna ya kukikabilia nacho. Kama unafikiri utakutana na upinzani mkubwa kwenye biashara yako, jiandae kuukabili upinzani huo kwa njia kama kuongeza ubora wa bidhaa au huduma zako. Kama una mipango mikubwa unayoenda kuitimiza kawa mara ya kwanza kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na hofu ya kushindwa. Likabili hili kwa kuiaminisha akili yako ukweli huu kuwa mara nyingi vitu vingi binadamu anavyovihofia huwa havitokei na kwa kufanya hivyo utaiendea hatua hiyo kwa ujasiri.
Kama kulivyo na matuta mengi barabarani, ndivyo ilivyo kwenye safari yako ya mafanikio. Baada ya kumaliza kikwazo kimoja kuna nafasi yakukutana na kingine. Ukilifahamu hili litakusaidia kutokata tamaa kwa kuona kuwa mafanikio hayo hayawezekani kufikiwa kwa sababu ya vikwazo. Huna budi kuendelea kuvikabili vikwazo hivyo mpaka mwisho.
Kadri utakavyoendelea kupambana na kuvishinda vikwazo mbalimbali, ndivyo utakavyoweza kujenga uzoefu wa kuvikabili vikwazo vingine kwa urahisi zaidi. Pia kadri utakavyokuwa unaendelea kuvikabili vikwazo vingi ndivyo utakavyokuwa unakaribia mafanikio yako. Kuna watu wengi waliokata tamaa na kurudi nyuma wakati wakiwa wamebakiza umbali mfupi tu kutoka kwenye kituo ambapo mafanikio yalikuwepo. Usiwe miongoni mwao.
Kuna safari ngapi ulianzisha ukaishia njiani baada ya kukutana na vikwazo? Kuna mambo gani ya muhimu uliyoamini kuwa ungeyafanya ungepiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako lakini hukuanza kwa hofu ya kushindwa? Huu ni wakati wa kuzirudia safari zako ulizoziachia njiani. Weka mikakati mathubuti ya kuiendeleza safari hizo, huku ukijiandaa kukabiliana na changamoto zozote zile.
Ndugu! Mafanikio makubwa hayajawahi kuwa rahisi hata siku moja na ndiyo maana tuzo kwa washindi ni kubwa mno, kuwa miongoni mwa washindi hao kwa kukubali kuzikabili changamoto zote zitakazojitokeza kwenye mipango yako ya kutimiza malengo yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz