Ukilitambua Hili Utaweza Kuvumilia Maumivu Yoyote Yale Kupata Unachotaka.


Categories :

Kuna binadamu waliofanikiwa kufanya mambo makubwa sana hapa duniani ambayo yanaonekana kama miujiza. Kuna wengine bado wapo hai na wengine walishakufa siku nyingi lakini wanakumbukwa kwa michango yao mikubwa waliyoitoa hapa duniani.  Lakini safari za watu hawa hazikuwa rahisi hata kidogo. Wapo waliopitia mateso makali lakini walivumilia na kupata vitu ambavyo vinakumbukwa mpaka leo. Wapo walioshindwa mara nyingi sana na kupitia maisha magumu na ya ajabu, lakini walivumilia safari zao mpaka wanafika.

Viongozi wa siasa kama Nelson Mandela anakumbukwa mpaka leo kuwa ni kiongozi mashuhuri wa ukombozi wa Afrika. Lakini ukifuatilia mapito aliyopitia, unaweza kusema huyo alikuwa sio binadamu wa kawaida. Maana alikubali kukaa gerezani miaka ishirini na saba ili mradi tu Afrika  ya kusini ikombolewe, huku akipewa nafasi kadhaa za kuachiwa huru kama angekuwa radhi kuacha kudai ukombozi lakini alikataa. Wagunduzi wa dunia kama Thomas Edson alishindwa zaidi ya mara elfu moja katika ugunduzi wake wa taa ya umeme lakini aliendelea tu mpaka alipofanikiwa.

Unaweza kujiuliza hao watu wachache ambao wanaonekana ni mshaujaa wa dunia waliofanikiwa kupata ushindi mkubwa licha kushindwa mara nyingi au kupitia mateso makubwa makali wana nini cha ziada? Hakuna kitu cha ziada ambacho wanacho ukiwalinganisha na wewe. Walichokuwa nacho wao na wewe kipo ndani yako lakini hujakitumia. Kwa nini mara nyingi tu umeanzisha kitu fulani lakini hukufika mbali? Ulipokutana na changamoto tu, ulikata tamaa tena baada ya muda mfupi tu! Hawa watu waliofanikiwa kufanya makubwa licha ya maumivu waliyokuwa wanayapitia, walifanikiwa kuusikia wito wao wa ndani na kuuitikia.

Wito wako wa ndani ni sauti yako kutoka ndani mwako na sio nje ambayo inakuita ukafanye jambo fulani hapa duniani kwa manufaa ya watu wengi. Hii ni sauti inakuonyesha safari yako ya kuisafiri hapa duniani. Hii ni sauti ambayo ukiisikia na kuiitikia itakuwa rahisi kuianza safari hiyo na kuuona mwisho ambao inabidi uufikie. Pia hii ni sauti ambayo itakufanya uendelee na safari hata pale utakapotakiwa kupanda mlima mrefu ili usogelee mwisho wa safari yako.

Watu wengi wameshindwa kufanya mambo makubwa hapa duniani na kuishia kuwa watu wa kawaida kwa sababu ya kutoisikiliza sauti hii ndani yao na badala yake kuendelea  kusikiliza sauti za dunia ambazo ni za watu wengine. Huwezi kufanya miujiza kwa kuitika sauti za watu wengine. Kwa kuitika sauti za wengine wameishia njiani. Wapo watu wengine waliozisikia sauti zao za ndani lakini wakazipuuzia na kuzisikiliza sauti za wengine hii ndiyo imewafanya kuishi maisha ya kawaida.

Naamini unatamani uishi maisha yenye maana hapa duniani. Maisha ambayo yatakufanya uendelee kukumbukwa hata baada ya kufa. Haya ni maisha ambayo yatagusa maisha ya watu wengine na wakatambua mchango wako. Utafanikiwa kufanya hiyo kama utatulia na kutega masikio yako ya ndani ili uweze kusikia sauti inayokuita. Sauti yako ya ndani haidanganyi maana ndiyo inayokufahamu wewe kuliko mtu mwingine yoyote hapa duniani. Ukiisikiliza sauti hiyo na kuitii ndipo utakapokuwa radhi kuendelea na safari hiyo hata kama utakapokumbwa na changamoto kubwa na zenye maumivu makali.

Ndugu! Pata muda wa utulivu ambapo utajitenga na sauti nyingine kisha sikiliza ndani mwako kwa kujiuliza wewe ni nani? Kwa nini upo hapa duniani? Kitu gani unatamani ukikamilishe hapa duniani kipindi chako cha uhai?. Moyo wako ni mwaminifu, utaongea nawe utasikia wito wako kisha anza kuuishi ndipo utakapokuwa radhi kuvumilia maumivu yoyote yale.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *