Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukutana Na Bahati Yako Uliyoisubiri Siku Nyingi.
Licha ya jitihada kubwa na mipango mizuri amabyo mtu anaweza kuiweka, lakini bado kuna nafasi ya bahati inayomsaidia mtu kupata mafanikio hata yale makubwa. Yamkini umeanza kushangaa kama nafasi ya bahati ipo, kwa nini wewe kama hujapata nafasi hiyo mpaka?
Licha ya nafasi hiyo ya bahati kwenye mafanikio lakini watu wengi wamekuwa hawanufaiki na bahati hiyo. Ndiyo maana kuna wakati umediriki kusema kuna watu wana bahati zao. Lakini kila mtu ana nafasi ya kupata bahati yake. Hii ina maana kuwa kuna kitu cha kufanya ili bahati iweze kufika kwako. Hiki ndicho wale waliofanikiwa wanachokifanya, na wewe unaweza kukifanya hicho na bahati zikaanza kukufikia. Kitu hicho ni maandalizi.
Mwanaflsafa wa kiroma Seneca alisema “Luck is what happens when preparation meets opportunity.” akimaanisha kuwa bahati hutokea pale maandalizi yanapokutana na fursa. Kuna fursa nyingi huwa zinajitokeza kwenye safari ya mafanikio lakini fursa hizo zitakunufaisha kama utakuwa na maandalizi sahihi.
Kumbe kama umekuwa hupati bahati katika maisha yako, si kwamba wewe huna bahati la hasha bali ni kwa sababu umekuwa huna maandalizi mazuri ya kukutana na bahati. Kwa mfano kama una biashara ambayo ulishaiweka kwenye mfumo mzuri na ikatokeo kuna mtu anataka kununua biashara tena kwa bei kubwa, wewe utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufaidika na fursa hiyo kuliko yule ambaye biashara yake haieleweki.
Kama una tabia ya kuweka akiba kwa ajili ya uwekezaji, labda kwenye majengo na ikatokea kuna mtu anauza nyumba yake kwa bei ya chini sana ukilinganisha na thamani yake, wewe una nafasi kubwa ya kununua nyumba hiyo kuliko yule ambaye hana akiba zenye malengo. Je hujawahi kushuhudia mtu ananunua kitu kwa bei ndogo na mwisho watu wanamwambia yule jamaa ana bahati sana? Haya ni maandalizi yaliyokutana na fursa.
Ni wakati sasa umefika wa kuanza kutayarisha mazingira yako ili maandalizi yako yakutane na fursa kisha bahati yako izaliwe.
Jambo la kwanza ni wewe kujua unakoelekea na kuweka mipango yakuanza na kuendelea na safari. Unapoendelea na safari ndipo unapokutana na fursa zitakazokuinua na kukufanya ukimbie. Ndiyo maana wanasema mwenda bure si mkaa bure. Hii ina maana kubwa sana kuwa lazima uwe unafanya kitu uweze kukutana na bahati. Hivyo ishi maisha ya ndoto yako huku ukiweka mipango yako ya kufanyia kazi, ndipo utakuwa kwenye mazingira mazuri ya kukutana na bahati.
Kuwa barabarani ndipo utapata ‘lift’. Kama unatembea barabarani kwa miguu ni rahisi mtu mwenye gari akakuona na kukupa lift kuliko ungebakia umejifungia nyumbani. Kila wakati uwe kwenye mwendo wa kuishi ndoto yako, ndipo unapoweza kikutana na fursa ya kukufanya kupiga hatua kubwa. Usisubiri bahati ije ndiyo uanze mwendo, badala yake uwe kwenye mwendo na bahati itakukuta.
Jiandae. Kila wakati weka mazingira sawa ya kukutana na habati yako. Miongoni mwa maandalizi ni kuweka akiba au kuwa na maarifa muhimu ambayo unatambua kuwa muda wowote yatahitajika. Kwa mfano ni muhimu kuwa na ujuzi wa kuuza bidhaa au huduma kwa sababu katika maisha yako lazima utahitajika kuuza, hivyo kuwa na ujuzi kama huu utakuweka mazingira mazuri ya kukutana na bahati.
Ndugu! Umekuwa ukipishana na bahati kwa sababu fursa zinapokuja zinakukuta hujajiandaa hivyo zinaenda kwa watu wengine. Anza kufanya maandalizi sasa na endelea kuishi ungali umejiandaa ili fursa zitakapokuja unapata bahati kama watu wengine wanavyoendelea kupata bahati zako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz