Pukutisha Majani Yako, Ni Kiangazi Sasa.
Miti mingi hupukutisha majani mengi kipindi cha kiangazi ili kuhifadhi maji. Hupukutisha majani kwani ndiyo yanayopoteza maji kwa njia ya mvuke. Baada ya kiangazi kupita na masika kuingia miti hiyo huchipusha majani mengine miti hiyo ikiamini kuwa kuna utele wa maji.
Miti isiyo na ufahamu kuhusu hilo huacha majani yake wakati wa kiangazi na hivyo kuendelea kupoteza maji, kudhoofika na baadaye hata kufa.
Kuna somo kubwa la kujifunza kutoka kwa miti hii. Kuna vipindi vigumu utapitia maishani mwako kama vile kipato kidogo, biashara ngumu, mahusiano mabovu, kutojipenda na kujiamini n.k. Hiki ni kipindi cha kiangazi ambacho unahitaji kufanya kila jitihada kuhakikisha unabaki kuwa hai. Muda wa kuhakikisha licha ya ugumu ambao biashara yako inaupitia, lakini bado inabaki kuwa hai. Hiki ni kipindi ambacho, licha ya kuwa na kipato kidogo, lakini huingii kwenye mikopo isiyo na tija. Hiki ni kipindi ambacho licha ya ugomvi uliopo kwenye mahusiano yenu, lakini unaulinda upendo kidogo uliopo wakati ukiendelea kutatua migogoro.
Watu wengi wamekufa kwa kuenda kinyume na busara hii ambayo miti inafanya. Baada ya kuona maisha ni magumu kwa kuwa na kipato kidogo, anaamua kwenda kukopa ili kukidhi matumizi na si kuongeza kipato ili kukidhi mahitaji aliyonayo. Kwa kufanya hivyo, mtu anaendelea kutaabika na madeni yasiyokuwa na ukomo.
Pukutisha tabia. Katika kipindi hiki kigumu unachopitia kuna tabia ambazo hazitakupa uhai bali kifo. Je ni tabia ya kukosa uvumilivu kwenye kipindi hicho kigumu? Je ni tabia ya kutowajibika yaani kuchukua jukumu la maisha yako? Hiki ni kipindi cha kupukutisha tabia hizi na nyingine zinazofanana na hizo ili uendelee kuishi.
Pukutisha matumizi yasiyo lazima. Kipindi cha kiangazi ambapo kina ukame wa fedha. Ili uweze kuishi katika kipindi kama hiki huna budi kutokuwa na matumizi ambayo siyo ya lazima. Haya ni matumizi ambayo inabidi yasifanyike ili biashara yako iendelee kuishi.
Ziba mianya ya upotevu. Katika kipindi cha kiangazi huna budi kuziba mianya yoyote ambayo inayoweza kupitisha kile ambacho tayari unacho. Kama ni biashara basi hakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri kuhakikisha hakuna fedha inayopotea. Kama ni kwenye mahusiano hakikisha hakuna uzembe wowote unaopunguza mawasiliano mazuri bali imarisha mawasiliano.
Ndugu! Huwa unafanya nini pale unapokutana na kiangazi maishani mwako? Je huwa unaweka jitihada kubwa kuhakikisha unaendelea kuishi? Au ndiyo unazidi kunyauka na kisha kufa.
Kipindi cha kiangazi ni cha wewe kuwa na nidhamu ya hali ya juu kuhakikisha hupotezi kile ambacho tayari unacho bali unakitunza. Hakikisha unalinda uhai wa kila ulichonacho, katika kipindi hiki. Linda mtaji wa biashara yako. Linda mawasiliano ya mahusiano yako yanayopitia wakati mgumu.
Kaa chini kisha tafakari ni kiangazi gani unachopitia sasa katika kila eneo la maisha yako? Baada ya kutambua kiangazi hicho, angalia ni kitu gani unaweza kukipukutisha ili usife katika kipindi hiki bali uendelee kuishi na kisha kukutana na masika yako. Weka nidhamu kubwa katika kipindi hiki kiangazi ili upate ujasiri wa kupukutisha kile ulichokipanga.
Linda ulichonacho kipindi cha kiangazi ili uendelee kuishi mpaka kipindi cha masika kitakapofika na kustawi sana.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz