Anza Kuishi Maisha Yako Sasa Baada Ya Kuishi Ya Watu Wengine Kwa Muda Mrefu.


Categories :


Maisha yako ya hapa duniani yameambatana na muda wako wa kuyaishi maisha hayo. Huu ni muda unaotarajiwa uishi maisha yako kikamilifu. Watu wengi wamekuja kushangaa kuwa, kumbe walikuwa hawayaishi maisha yap pale muda wao unapokuwa umeshaisha.

Kwa kufanya hivyo wamekuwa wakikazana kumsaidia ndege aruke wakati wao ni samaki na ilibidi waogelee. Wamewasaidia watu wengine kuishi ndoto zao na kutimiza malengo yao. Kumbe wengine wanapofanikiwa kuishi maisha yao wao ndiyo wanakuwa wasaidisizi wao.

Unaweza kujiuliza ni kwa namna gani wewe hujaishi maisha yako? Njia mojawapo ni ya kuwa bingwa wa kujibu maswali na sio kutengeneza maswali. Kuna utofauti mkubwa kati ya kujibu maswali na kuuliza maswali. Kujibu mswali ni kutoa mrejesho wa kazi ambayo mtu aliifanya wakati maswali ni kazi yako unayoianzisha. Majibu yanatokea nje wakati maswali yanaanzia ndani.



Ukiyakuta maswali na kuanza kuyajibu unamsaidia mtu aliyekaa chini na kuyafikiri na kuyatoa kutoka ndani mwake. Kujibu maswali ya watu wengine, si kazi yako bali yako unasaidia mtu mwingine kukamilisha kilicho ndani yake.

Kujiuliza maswali ni kutafuta ukweli kuhusu wewe, huwezi kuwa wewe usipoutafuta ukweli ndani yako. Ukweli huo utaupata kwa kujiuliza maswali na kuusikiliza moyo wako. Hii ni kazi kubwa ambayo inabidi uifanye ili uweze kuishi maisha yako na sio ya watu wengine. Pale utakapoanza kuishi maisha yako ndipo utakapoanza kupata mafanikio makubwa kisha kukua na kufikia utoshelevu.

Huwezi kufikia mafanikio makubwa kwa kujibu maswali ya watu wengine. Hata ukifanikiwa kupata majibu hyatakuwa makubwa na hata kama yatakuwa makubwa hayakupa utoshelevu. Je hujawahi kushuhudia mtu ana mafanikio makubwa lakini bado anahisi utupu ndani yake. Hii ni kwa sababu ya kuishi kwa kuendela kujibu maswali ya watu wengine

Ni wakati wako sasa wa kujiuliza maswali haya kuhusu wewe. Wewe ni nani? Unaweza kufanya nini? Umekuja hapa duniani kufanya nini? Nini ndoto ya maisha yako? Una malengo gani unayofanyia kazi? Haya ndiyo maswali ambayo inabidi ujiulize mara kwa mara na kuyatafutia majibu. Ukijikita kwenye maswali haya utaepuka kuishi maisha ya watu wengine.

Kwenye hali yoyote unayopitia sasa, jiulize wewe kama wewe unatokaje katika hali uliyonayo sasa? Jiulize pia nini unachokitaka maishani mwako? Kisha chunguza ndani yako silaha ulizonazo kupata kile unachotaka.

Maswali anayojiuliza samaki ni tofauti na maswali anayojiuliza ndege kwa sababu hawa wawili wana kusudi tofauti hapa duniani. Kwa sababu kila binadamu ana kusudi tofauti hivyo huwezi kufanikiwa kupata mafanikio makubwa u unayostahili kwa kujibu maswali aliyojiuliza mtu mwingine.
Kwa sababu ya upekee wako, anza na jibu maswali yako.


Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *