Hili Ndilo Shamba Sahihi La Kupanda Mbegu Za Mafanikio Unayoyatamani.


Categories :

Ili uweze kuotesha zao lolote lile utahitaji kuwa na mbegu ya kupanda na baada ya kutengenezewa mazingira mazuri, mbegu hiyo huota na kisha kuzaa matunda. Kile unachokipanda ndicho kinachoota. Huwezi kupanda mbegu za mahindi halafu zikaota kunde. Ndiyo maana kuna msemo unasema unavuna unachopanda.

Mafanikio uliyoyatamani kwa siku nyingi ni kama mazao, ili yaweze kuota na kuzaa matunda unahitaji kupanda mbegu, tena mbegu bora. Watu wengi wamekuwa wakifikiri tu kuhusu mafanikio lakini wamesahau kuwa wanahitaji kupanda mbegu za mafanikio shambani. Mafanikio utakayoyapata yanategemea sana mbegu unazozipanda, eneo unalolipanda mbegu hizo na utunzaji wa mbegu hizo ili ziweze kuzaa matunda.

Mafanikio hupandwa kwanza akilini. Hili ndilo shamba la matokeo yoyote tunayoyapata. Bahati mbaya ni kuwa akili huotesha mbegu yoyote ile hata ile chafu. Ukipanda mbegu za kushindwa utapata matokeo ya kushindwa. Kadhalika ukipanda mbegu ya kufanikiwa utapata matokeo ya kushinda. Binadamu ana maeneo mawili ya akili yake, akili ya ufahamu wa nje na akili ya ndani. Akili ya nje hupatikana kwa milango ya mitano ya fahamu yaani macho, masikio, ulimi, ngozi na pua. Hii ni akili ambayo mtu hujifunza shuleni au kwa namna nyingine kwa kutegemea mazingira ya dunia ya nje. Sehemu ya pili ya akili ni akili ya ndani.

Akili ya ndani haina milango ya fahamu kama ilivyo kwenye akili ya nje. Hii ni akili yenye nguvu kubwa kuliko ile ya nje . Ili uweze kupata mafanikio makubwa huna budi kupanda mbegu za mafanikio yako katika shamba hili kwa usahihi mkubwa. Akili ya ndani hupokea mapendekezo na amri zote ambazo akili yako ya nje inakuwa inaamini kuwa ni za kweli.

Napoleon Hill alisema Whatever your mind can conceive and believe, it can achieve.Akimaanisha kuwa chochote ambacho akili inaweza kukipokea na kukiamini, utapokea. Kumbe hili ni shamba zuri sana la kupata chochote unachokitaka. Unataka nini maishani mwako? Mbegu hiyo lazima ipandwe kwanza kwenye  akili yako. Ukifanikiwa kupanda mbegu vizuri kwenye shamba hili utakuwa mwanzo mzuri wa kuja kuvuna mafanikio makubwa kutokana na uwezo mkubwa wa shamba hili. Hivi ndivyo unavyoweza kupanda mbegu kwenye shamba hili;

Kuwa na picha kamili ya nini unakitaka. Ili ujue utavuna nini shambani kwako, lazima utambue ni kitu gani ulichokipanda. Ili akili yako ya ndani ipokee na kuweza kukusaidia kukupa njia za kupata mafanikio, huna budi kuiambia kwa wazi kabisa ni nini unakitaka kitokee. Kama ni fedha basi weka kiwango kabisa na lini unataka kukipata.

Fikiri kwa kina. Baada ya kujua nini unakitaka, huna budi kupata muda wa kufikiri kwa kina kuhusu kitu hicho na matokeo unayotarajia. Pata muda wa utulivu ona ukifanya hicho kitu na kupata matokeo unayotaka. Wakati ukifikiri kwa kina jenga hisia za kuona tayari umeshapokea. Huku ndiyo kujenga imani kama Napoleon alivyosema.

Andika mara kwa mara. Kuna nguvu kubwa ya kupanda ya mbegu ya mafanikio unayoyataka kama utachukua hatua ya kuyaandika mara kwa mara mambo unayoyataka yatokee maishani mwako. Kwa kufanya hivyo utakuwa unazamisha vizuri mbegu za mafanikio kwenye shamba lako la akili ya ndani. Unaweza kuanza kuandika kile unachokitaka mara tatu kwa siku, asubuhi, mchana na jioni.

Waambie watu wengine kile unachotaka kitokee. Unapochukua jukumu la kuwaambia watu nini unakitaka kitokee maishani mwako, unajiongezea imani ya kuwa kitu hicho kitatokea. Kadri imani yako inavyozidia kuongezeka ndivyo na uwezekano wa jambo hilo kutimia unavyozidi kuongezeka.

Ndugu! Una shamba zuri kwa ajili ya mafanikio unayoyataka. Fanya hii hatua ya kuhakikisha unaanza kupata kile unachokitaka kwenye akili yako ya ndani. Usiruhusu kupanda uchafu humo, bali panda mbeu nzuri za mafanikio ili uweze kuvuna unachokitaka kwa kukiwaza na kukiamini hicho muda wote.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

2 thoughts on “Hili Ndilo Shamba Sahihi La Kupanda Mbegu Za Mafanikio Unayoyatamani.”

  1. Habari Kocha,
    Kunanguvu kubwa ya kuwaambia watu nini unataka utafanya au mategemeo Yako ya baadae lakini wengi wanashauri sana kuto kuwaambia watu malengo Yako maana wengi wataweka kuwa ndio wakatisha tamaaa. Vipi hapo unaonaje nguvu ya kusema ndoto Yako na matokeo ya waharibu ndoto? Nakubaliana na wewe asilimia mia moja kwenye nguvu ya kuandika mara Kwa mara nini matarajio Yako kuelekea kufanikiwa.

    1. Habari Wito, hongera pia kwa kunipa mrejesho,

      Ni kweli hakuna kitu chenye faida pekeyake, unapowashirikisha watu ndoto yako wapo watakaokukatisha tamaa.
      Lakini kun faida kubwa ambayo utaipata pale utakapotangaza kwa watu japo sio kila mtu ndoto yako.
      1. Utakusukuma ukifahamu vizuri kitu hicho. Huwezi kumwambia mtu kitu ambacho wewe mwenyewe hukifahamu vizuri. Utajiandaa ndipo uwaambie.

      2. Utakuwa umetengeneza deni kwa watu uliowaambia, ambapo kila wakati utatakiwa ulikumbuke na kulilipa.
      3. Ile hali ha kutopenda kuwaangusha wale uliowaambia, itakufanya ujisukume zaidi ili usionekane umeshindwa.
      4. Kama hakuna mtu anayejua unavhofanya, ni rahisi sana kuacha pale unapokutana na changamoto ukiamini hakuna atakayejua.

      Lakini angalia watu kuwaambia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *