Vitu Hivi Vinne (04) Ulivyovishikilia Ndiyo Vinakukwamisha Usipige Hatua.


Categories :

Maisha ya mafanikio yako yanapatikana kwa kupiga hatua. Ukipiga hatua kila siku ndipo mwisho wa siku unapoweza kukusanya matokeo makubwa ambayo yatakupa mafanikio makubwa. Katika harakati za kupiga hatua kuna vizuizi vingi vinavyosimama njiani. Hivi ndivyo vinavyosababisha watu wengi kutopata vile walivyotamani maishani mwao.

Kuna vizuizi ambavyo hutoka nje yako yaani mazingira wakati vingine vikitoka ndani yako. Kuna vizuizi ambavyo vipo ndani yako ulivyovitengeneza mwenyewe wakati wa makazi yako. Katika vizuizi hivyo hakuna mtu wa kumlaumu isipokuwa wewe mwenyewe. Na kwa asilimia kubwa vizuizi vya ndani mwako ndivyo vinavyosababisha kwa kushindwa kwako. Ndiyo maana wewe ndiyo mtu wa kwanza kulaumiwa kwa kushindwa kwako. Miongoni mwa vitu ambavyo umevishikilia na vinavyokukwamisha kupiga hatua ni;

Hofu. Hiki ni kizuizi kikubwa sana kwako katika kupiga hatua. Hiki umekijenga kwa  kutokuwa na uhakika wa kupata matokeo unayotarajia kuyapata. Hiki ni kitu ulipokiruhusu tu kikakuzuia usianze kuchukua hatua, kama kuanzisha biashara, kuanzisha uwekezaji, kuuza kwa watu usiowafahamu au kuweka mipango mikubwa zaidi ya ile uliyoizoea. Kila mtu ana hofu, lakini ili uweze kupiga hatua huna budi kuiendea hofu yako, yaani kufanya vitu unavyovihofia. Hivyo acha kushikilia hofu badala yake shikilia malengo yako na kuyatimiza.

Chuki. Kwa nini unajichukia mwenyewe? Kwa nini unamchukia jirani yako? Kinyume cha chuki ni upendo. Ukiishikilia chuki ndani yako, unaunyima nafasi ya upendo ndani yako. Huwezi kupiga hatua kama utakuwa hujipendi mwenyewe. Huwezi kujiona wa thamani kama hujipendi mwenyewe, ni rahisi sana kujifanyia mabaya kama utakuwa hujipendi. Huwezi kuwapa thamani watu wengine kama utakuwa unawachukia. Kumbuka unapata chochote kama utakuwa tayari kuwapa watu wengine kile wanachohitaji. Hii ni kuwa thamani, ambayo upendo inabidi utangulie badala ya chuki.

Hukumu. Kwa kuwa umekuwa bingwa wa kujipa hukumu kwa makosa unayotenda imekufanya usijipende na kujiona mnyonge. Pia hukumu hizo zimekufanya uendelee kukumbuka yale yaliyopita badala ya kuangalia kile unachoweza kufanya sasa. Kwenye kila kosa unalofanya au analolifanya mtu mwingine kwao usijihukumu bali angalia kile unachoweza kujifunza, jifunze kisha songa mbele.

Kujidharau. Umejipa thamani mbele ya watu wengine? Je unajiona wewe hufai mbele ya watu wengine? Je unajiona wewe ni wa kawaida na mafanikio makubwa ni ya watu fulani? Umejiweka kwenye mizani gani? Moja ya kitu kinachokufanya usipige hatua ni kujiona mnyonge baada ya kujidharau. Hili limetokea baada ya kuanza kujilinganisha na watu wengine. Jambo moja unalotakiwa kukumbuka ni kuwa wewe ni wa thamani kubwa sana na hakuna wa kujilinganisha naye. Thamani yako ni ya kipekee, hutakiwi kufananisha na mtu mwingine kisha kujidharau.

Hivi ni vitu vinne ulivyovishikilia kwa muda mrefu na kukufanya ushindwe kupiga hatua. Ni wakati sasa wa kuhakikisha unavitua na kutokuwa kikwazo kwako kupata kile unachokitaka. Usiache hofu ikakuzuia kuchukua hatua. Ukikosea usijihukumu bali jifunze. Usijichukie wala kumchukia mtu mwingine kwani unapunguza nafasi ya upendo. Jipe thamani kubwa kwani una uwezo wa kipekee. Weka malengo makubwa na jipe ujasiri wa kuyaendea licha ya changamoto unazoweza kukutana nazo ili kupata mafanikio unayoyataka kisha hakikisha unawapenda watu wengine kwa kuwapa thamani kubwa, hapo ndipo watakapokuwa radhi kukupa chochote unachotaka.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *