Unaweza Kutengeneza Dunia Ya Kwako.


Categories :

Unavyoiona dunia unaweza kushawishika kuwa kila mtu ndivyo aionavyo. Ukitazama dunia utaona ina mambo au vitu fulani ambavyo haviko sawa. Unaweza kuhitimisha kuwa ndivyo dunia ilivyo. Ukiangalia hali ya uchumi unaweza kufikri kabisa kuwa dunia haina usawa, kwa nini kuna watu matajiri sana wakati wengine ni masikini sana? Ukiangalia dunia na matendo yake ya kikatili, unaweza kuhitimisha kuwa dunia haina upendo, inawa watu katili sana.

Ukiwa umevaa miwani ya rangi kila kitu unachokiona kitakuwa na rangi sawa na rangi ya miwani yako. Hii ni sawa na jinsi unavyoiona dunia. Hii dunia unayoiona ni kutegemeana na miwani yako ya ndani ilivyo. Miwani hiyo ni mtazamo ulionao ndani yako. Kila kitu unachokiona ni sawa kulingana na taarifa zako za ndani ambazo tayari ulishazijenga.

Sheria ya ulinganifu inasema, maisha yako ya nje ni taswira ya maisha yako ya ndani. Kumbe chanzo cha maisha unayoyaona nje kipo ndani yako. Kokote utakapokuwepo na wewe upo yaani wewe wa ndani. Huioni dunia ilivyo lakini kama ulivyo. Kioo cha kujitazamia huwa hakitengenezi taswira yake chenyewe bali ya kitu kile kitakachokuwa mbele yake.

Kumbe kama unataka mabadiliko yatokee kwenye taswira huna budi kuanza kubadili taswira ya kitu kinachosimama mbele ya kioo. Huwezi kupata taswira safi kama hujasafisha kitu kinachotengeneza taswira hiyo. Maisha yako ya nje hayawezi kubadilika kama ndani mwako hujafanya mabadiliko yoyote.

Unaiona dunia ya sasa kulingana na mtazamo ulioujenga ndani yako kwa muda mrefu. Mtazamo huo umetokana na vitu ulivyoviona, kuvisikia, kuamini, kujifunza kwa muda mrefu. Hiki ndicho kilichotengeneza miwani yako. Huu ndiyo msingi uliojenga kile ulichonacho sasa, kile unachokiamini na kukifanya. Hali ya maisha yako ya sasa ni kwa sababu ya mtazamo huu.

Kuna hali ambazo unatamani uzibadilishe, kuna hatua fulani ya maisha unatamani uifikie, kuna mtu wa namna fulani unataka uwe; sehemu sahihi ya kuanzia ni ndani mwako. Kama umekuwa ukiona kuna uhaba wa fedha  na hivyo huwezi kuwa tajiri kwa sababu matajiri wameshachukua fedha zote, huna budi kuanza kwa kubadili mtazamo huo ili miwani yako ione dunia ikiwa na utele. Hii ina nguvu kubwa sana kwani bila ya kuamini kuwa kuna utele wa fedha au utajiri ni vigumu sana kuweka jitihada za kutafuata utajiri pale unapokutana na changamoto.

Kama ndani yako kuna mtazamo wa kuwa inabidi ufurahi kwa matukio hutakuwa na furaha mpaka ukutane na matukio fulani ya kufurahisha. Kumbe unaweza kubadili mtazamo huu na kutengeneza dunia yako kwa kuamini kuwa furaha isiwe ni zao la matukio bali uhai wako. Ukifanikiwa kutengeneza mtazamo huo utaweza kutengeneza dunia yako kuwa na furaha muda wote bila kujali matukio unayokutana nayo.

Ndugu! Ni dunia gani unahitaji kuwa nayo katika dunia hii? Dunia hii ipo ndani mwako, hakikisha unapata maarifa sahihi ambayo yatajenga dunia sahihi ya ndani na baadaye kuwa na dunia unayokubali nje. Kama umekuwa ukilalamika kwa sababu ya  taswira unazoziona nje yako, basi tambua kuwa sehemu sahihi ya kuanza kurekebisha ni ndani yako. Huna budi kuanza kufuta mtazamo kwa kuubadilisha na mtazamo mpya ambao ni sahihi na utakaokusaidia Hivi ndivyo unavyoweza kutengeneza dunia yako unayoitaka.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *