Fanya Hivi Ili Kuifurahia Kesho Yako Kuliko Unavyoijutia Leo.
Maisha yako ya leo hayajatengenezwa leo, bali ni matokeo ya kile ulichokifanya siku za nyuma. Kama umepiga hatua kubwa au hujasogea, ujue si kwa sababu ya ulivyofanya leo bali ni matunda ya yale uliyafanya jana na muda uliopita. Ni sawa na matunda unayokula na kuyafurahia leo, hayatokani na mti uliyopanda leo bali miti uliyoipanda siku nyingi za nyuma.
Mafanikio ya maisha yako ni mkusanyiko wa matunda ya hatua ndogo ndogo unazozichukua kwenye vipindi mbalimbali vya maisha yako. Matokeo uliyonayo sasa ni kwa sababu ya hatua ulizozichukua siku za nyuma wakati matokeo ya maisha yako yajayo yatategemea kile unachokifanya leo.
Kwa sababu maisha ya mafanikio yanachukua muda mrefu kutokea, hivyo ulichonacho leo ni matokeo ya jitihada zako za siku nyingi zilizopita. Kama maisha yako ya leo hayakufurahishi, ujue ni kwa sababu ya yale uliyofanya miaka iliyopita. Kadhalika kama kuna mafanikio unayafurahia leo ujue ni kwa sababu ya jitihada ulizozifanya siku za nyumba zilizozaa matunda sasa.
Kuna maisha gani unayoyajutia sasa; je ni hali ngumu ya uchumi? Je ni mahusiano mabovu? Je ni thamani ndogo unayoitoa kazini? Je unajidharau na kutokujikubali? Hali hizi hazijazaliwa siku moja, bali ni matokeo uliyoyakusanya kwa siku nyingi zilizopita. Kwa sababu haya ambayo huyafurahii ilibidi yatengenezwe siku nyingi zilizopita, huna namna ya kuyabadili kwani muda wake umeshapita. Lakini kuna faida moja uliyonayo sasa, una nafasi ya kutengeneza kesho utakayoifurahia. Kuna mithali ya kichina inasema “muda mzuri sana wa kupanda mti ilikuwa miaka ishirini iliyopita, muda wa pili mzuri wa kufanya hivyo ni sasa’’
Hii ni methali inayokupa nafasi ya kurekebisha makosa uliyofanya nyuma. Ulikuwa na nafasi miaka nyuma ya kutengeneza maisha yako ya mafanikio ambayo ungekuwa unayafaidi leo lakini kama hiyo ilishindikana, bado una nafasi sasa ya kutengeneza maisha yako mazuri ya baadaye. Kumbuka kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa. Hii ni nafasi yako ya kutengeneza maisha ambayo matokeo yako utayapata muda ujao.
Anza kwa kutambua ulichotakiwa kuwa nacho. Kama unaona kuna mapungufu kwenye maisha yako, hii ina maanisha kuwa kuna vitu ambavyo ilibidi uwe navyo sasa lakini huna au umepungukiwa. Ili uweze kuitengeneza kesho yako iliyokamili ambayo utaifurahia huna budi kukaa chini na kujiuliza ni vitu unataka uwe navyo maishani mwako. Je unataka kuwa mtu wa namna gani? Unataka kuwa na kipato kiasi gani? Unataka kuwa na uwekezaji gani? Unatamani ufanye biashara gani? Kwenye mahusiano, unatamani uwe na familia ya namna gani? Kwenye kazi, unatamani utoe thamani gani kwa watu wengine kupitia kazi unazofanya? Haya ni maswali muhimu sana ambayo ukijiliza na kutafuta majibu sahihi utajua wapi uanzie kwa ajili ya kutengeneza kesho yenye mafanikio.
Weka mipango ya kuanza kuitengeneza kesho yenye mafanikio. Baada ya kujua maisha unayotamania kuwa nayo, hatua inayofuata ni kuweka mipango ambayo itakuwezesha kufikia mafanikio hayo. Kutamani peke yake hakutakupa kile unachokitaka bila kuweka kazi. Kwenye kila eneo muhimu la maisha yako; binafsi, biashara/kazi, fedha, afya na mahusiano, weka malengo na mipango ambayo utaanza mara moja kuifanyia kazi ili maisha yako ya kesho yawe ya mafanikio.
Huwezi kubadili chochote kwenye kitu ambacho ulitakiwa ukifanye jana kwa ajili ya mafanikio ya leo. Lakini una nafasi leo ya kufanya kitu kwa ajili ya mafanikio ya kesho. Anza leo.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz