Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuuwa Ndege Wengi Maishani Kwa Manati Isiyovutika.
Manati hutumika kuua ndege. Nguvu ya manati hupatikana kwenye mipira yake yenye uwezo wa kuvutika. Kadri mipira hiyo inavyovutwa ndivyo inavyoweza kuzalisha nguvu kubwa ya kulirusha jiwe mbali zaidi na kwa nguvu zaidi. Lakini maisha yako yana manati ambayo hutumika kukupa kile unachokitaka. Bahati mbaya ni kuwa manati ya maisha yako huwa haivutiki. Hivyo urefu wake hubaki vile vile.
Manati ya kukupatia ndege wa maisha yako ni muda. Muda ni kila kitu kwenye kuhakikisha unapata ndege wa maisha yako. Ukubwa na idadi ya ndege hao utategemea namna utakavyotumia manati hiyo. Bahati mbaya muda ni manati ambayo haivutiki kama ile manati ya kuulia ndege. Huwezi ukavuta muda na kuongeza hata sekunde moja.
Kuna usawa katika muda. Kila mtu ana masaa 24 kila siku, na siku saba kila juma. Mtu hawezi kufanya jambo lolote bila muda. Kilio cha watu wengi ni kuwa wana mambo mengi kuliko muda uliopo. Walitamani sana hata wangekuwa na uwezo wa kuongeza hata saa moja kila siku yenye masaa 24. Lakini hili ni jambo ambalo haliwezekani kwa sababu muda ni manati isiyovutika.
Lakini licha ya muda kuwa manati isiyovutika, bado kuna watu waliofanikiwa kutumia manati hii na kuua ndege wengi katika maisha yao wakati wengine wakiendelea kulalamika kuwa muda ni mchache na kuishi kufanya vitu vya kawaida. Hivyo ili uweze kupata mafanikio makubwa lazima ujue namna ya kuitumia vizuri hii manati usiyovutika. Hivi ndivyo unavyoweza kupata mafanikio makubwa kwa kutumia manati muda isiyovutika;
Kuwa muwazi. Ili uweze kutumia vizuri manati ya muda isiyovutika huna budi kujua kwa wazi kabisa nini unataka kukipata maishani mwako na namna utakayotumia kukipata. Kama unafahamu wapi unaenda si rahisi kupotea na hivyo kuwa na nafasi nzuri ya kutunza muda. usipokuwa wazi nini unataka, utatumia muda mwingi kujiuliza ufanye nini huku ukipoteza muda. Baada ya kujua nini unataka, wekeza muda, nguvu na umakini wako kwenye kile unachotaka bila ya kuhangaika na vingine.
Jione ukiwa mtumiaji mzuri wa muda. Kila kitu unachokifanya huanzia ndani mwako. Ili uweze kutumia vizuri hii manati ambayo havutiki na kupata matokeo makubwa huna budi kujenga picha binafsi ya kuoana ni mtumiaji mzuri wa muda. Ukifanikiwa kujenga picha hiyo, akili yako itaratibu vyema matumizi yako ya muda, kwa kukukumbusha pale utakapokuwa unachepuka kwa kufanya mambo yaliyo nje na mpango au yenye tija ndogo.
Jitoe kujenga tabia mpya. Kutumia vizuri manati hii ya muda isiyovutika kufanya mambo makubwa inakuhitaji kujenga tabia ya matumizi mazuri ya muda. Kutotumia muda vizuri ni tabia uliyoijenga kwa muda mrefu sana, hivyo unahitaji muda na kujitoa ili uweze kuvunja tabia ya sasa kisha kujenga tabia ya kutumia muda kwa ufanisi. Pale unapotaka kurudia tabia ya zamani, jilazimishe kuiishi tabia mpya mpaka iwe sehemu ya maisha yako.
Anza kubadili eneo moja. Unapotaka kubadili tabia kwa ajili ya kuboresha matumizi yako ya muda na kuwa na ufanisi mkubwa na maendeleo makubwa, chagua eneo moja la kuanzia. Usianze kubadili maeneo mengi mara moja, itakuwa rahisi kukata tamaa. Kwa mfano unaweza kuanza kuamka mapema, au kutuliza akili unapofanya kazi nk. ukishafanikiwa kubadilika eneo moja itakuwa rahisi kwenda na kuboresha maeneo mengine.
Thamini maisha yako. Kama unathamini maisha yako ni rahisi kuthamini muda. Muda na maisha ni vitu viwili ambavyo huwezi kuvitenganisha. Huwezi kusema una maisha kama huna muda, huwezi kutengeneza maisha bora kama huthamini muda. Kama kweli unayajali maisha yako anza kwa kujali muda.
Muda ulionao hauwezi kunyumbuka kama ilivyo manati. Kiasi ulichonacho kitabaki kilekile bila kuwa na uwezo wa kuongeza hata sekunde moja. Ili uweze kupata mafanikio makubwa kwa kutumia rasilimali adimu muda huna budi kubadili mtazamo wa jinsi unavyotumia muda kisha panga kuwekeza muda wako kwenye maeneo muhimu ya maisha yako ambayo yataboresha maisha yako. Chagua leo tabia za kutumia muda vyema utakazoanza kuzijenga. Kuanzia leo ona kupoteza muda ni kupoteza maisha yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz