Hii Ndiyo Njia Ya Uhakika Ya Kupata Chochote Unachotaka.
Umekuwa ukitafuta nini maishani mwako? Nini kiu kuu ya maisha yako? Kitu gani unatamani ukipate kabla hujaondoka hapa duniani? Je umekata tamaa baada ya kukitafuta kile unachokitaka kwa muda mrefu?
Kuna namna ambayo watu waliofanikiwa wanapata vile walivyovitaka. Unaweza na wewe ukatumia njia hiyo kupata ulichokitafuta kwa muda mrefu. Njia yenyewe ni kutoa kafara. Ndiyo kafara.
Yamkini ni neno kafara limeshitua akili au imani yako. Hili ni neno ambalo limekuwa likitafsiriwa vibaya na kushirikisha na imani za kishirikina. Katika imani za kishirikina kutoa karafa kumehusishwa na kutoa mali, mifugo au hata binadamu ili uweze kupata kile unachokita. Watu hufikia hatua hii kama njia ya mkato ya kutaka mali nyingi au utajiri kwa haraka.
Kuna kafara ambazo unaweza kuzitoa ili kupata kile unachokitaka. Hii sio za kutoa uhai wa mtu au kutoa wanyama kwa mganga ili upate kile unachokitaka. Hii ni kafara inayokuhitaji kujitoa wewe mwenyewe.
Mafanikio makubwa uliyoyawinda kwa muda mrefu yana hitaji nguvu zako, akili yako, umakini wako, muda nk ambavyo watu wengi wamekuwa hawapo tayari kuvipata. Kuna vitu ambavyo vinaonekana kuwa vizuri sana kwako ambavyo umekuwa mgumu kuvitoa na hivyo kukufanya kukosa mafanikio hayo. Hivyo ili uweze kupata mafanikio hayo huna budi kujitoa kwa kuvitoa vile unavyovipenda.
Kafara ya muda. Mafanikio makubwa unayoyataka yanahitaji muda wa kutosha. Maisha yako ni muda bila muda hakuna maisha. Licha ya kuwepo kwa mambo mengine ambayo utataka uutumie muda wako, kipaombele cha kwanza inabidi kiwe kwenye kile unachokitaka maishani mwako. Uutoe muda wako mzuri, kwa kuacha mambo mengine yanaonekana mazuri kwako lakini hayana mchango makubwa kwenye mafanikio mama makubwa unayoyatafuta.
Kafara ya nguvu. Nguvu za mwili wako zina ukomo. Pia mwili wako una asili ya uvivu na uchoyo wa nguvu zake. Ndiyo maana unaweza ukawa umepania ufanye kitu fulani lakini kabla hujamaliza kitu hicho, mwili unaanza kujisikia umechoka na kutamani kupumzika. Hapa ndipo unapohitaji kujitoa kuendelea na kazi kwa kuyakataa matamanio ya mwili wako ya kupumzika. Hii hutokea pia wakati wa kuamka asubuhi. Ili uweze kupiga hatua unahitaji kuamka mapema kabla ya wengine hawajaamka. Ili uweze kufanikiwa hilo unahitaji kutoa kafara ya usingizi wako mtamu wa asubuhi.
Kafara ya anasa. Kuna vitu vingi vya anasa unavyopenda kuvifanya. Hivi vinahitaji muda wako, fedha zako, nguvu na umakini wako. Ili kuwa na uhakika wa kupata mafanikio makubwa kama uhuru wa kifedha, unahitaji kupunguza sana au kuepuka anasa ambazo umeshazizoea kuzifanya. Je muda unaotumia kufuatilia michezo unaotakiwa kuuelekeza kwenye kusaka mafanikio yako hayo? Je ni muda na fedha unazotumia kula bata unavyotakiwa kuwekeza kwenye kile unachokitaka? Toa kafara ya anasa zako ili kupata kile unachokitaka.
Ndugu haya ni baadhi ya mambo ambayo unayoyajali na kuyapenda ambayo yanakufurahisha na ulitamani uyatumie kama unavyotaka. Lakini mafanikio yako makubwa yanahitaji uyatolee kafara.
Mafanikio yako yanahitaji muda wako mzuri. Hivyo kuanzia sasa, elekeza muda wako mzuri kwenye kweli kile kitu unachotaka ukipate kipindi utakachokuwepo hapa duniani. Nguvu zako nyingi sasa zielekezwe kwenye j
ambo lako kuu unalohitaji. Lakini pia unahitaji kuacha anasa ambazo umekuwa unazitamani kisha kuelekeza muda,nguvu,umakini,na fedha zako kwenye ndoto zako.
Hizi ndiyo kafara sahihi zinazolipa, anza kuzitoa sasa upate uhakika kutimiza ndoto zako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz