Anza Kuitumia Silaha Hii Kubwa Ya Kuangamiza ‘Stress’.
Maisha ya stress (sonona) yamekuwa mwiba mkubwa kwa watu katika zama hizi. Watu wamepoteza maisha kwa sababu ya sonona. Watu wameshindwa kupiga hatua kubwa maishani mwao kwa sababu ya sonona. Watu wameyachukua maisha yao na kuona raha kwa sababu ya sonona.
Sababu mojawapo zinazosababisha watu kuwa na stress ni ugumu wa maisha, upendo wa watu kupoa, kutaka mafanikio ya haraka, changamoto za maisha kuongezeka, kuiga maisha ya watu wengine. Kwa sababu ya maisha ya stress kuongezeka, watu wametafuta mbinu za kukabiliana na stress hizo hata zisizo halali. Wapo wanaoamua kutumia madawa ya kulevya ili kupata ahueni ya muda mfupi. Wapo wanaoamua kutumia vileo ili kuzikata stress hizo. Lakini mbinu zote hizo zimekuwa za muda mfupi, kwani mara tu baada ya vitu wanavyotumia kumalizika watu hao hurudia taabu zao.
Lakini licha ya changamoto hii kuwa kubwa na kuwa na athari kubwa za kiafya pia hata kiutendaji lakini kuna silaha ambayo unaweza kuitumia kuangamiza stress hizo. Silaha hiyo ipo ndani yako. Ndiyo ipo ndani yako bila kujali unaitumia au la. Watu walioitumia wameendelea kuishi maisha ya furaha na mafanikio licha ya changamoto kubwa walizoendelea kukutana nazo. Silaha hiyo ni uwezo wa kuchagua jambo moja juu ya jingine.
Umepewa ‘uboss’ wa nini ukifikiri na nini uamue kukifanya. Pia wewe ni boss wa hisia zako ambazo ndiyo barabara ya stress zako. Kwenye kila jambo linatokea maishani mwako una uwezo wa kuchagua kitu gani ukikatae na kitu gani ukipokee. Kumbe hata kama mtu akikuudhi, unaweza ukachagua ukasirike au usikasirike. Ndiyo maana umeshawahi kumshuhudia mtu akiendelea kunyamaza wakati akitukanwa na mtu mwingine.
Chagua upendo juu ya chuki. Chuki ni moja ya hisia hasi ambazo hupelekea stress za maisha. Chuki ni kinyume cha upendo. Wakati upendo ukileta furaha maishani, chuki huumba huzuni na maumivu makali ambayo huweza kusababisha magonjwa na ufanisi mdogo wa kazi. Lakini ndani yako una uwezo wa kuanza kuchagua upendo badala ya chuki. Kwenye kila jambo linalotokea kuna nafasi ya kuchagua kutoa upendo badala ya chuki, ukiangalia nafasi hiyo utaipata na ndivyo utakavyoweza kuziangamiza stress zako.
Chagua kusamehe badala ya kisasi. Kama upo hapa duniani huwezi ukakwepa kutokukosewa. Kila mara watu watakukosea na kukuonea. Je watu wakikukosea huwa unafanya nini? Unawasamehe au unajipanga kulipa kisasi? Mipango yako ya kulipa kisasi ndiyo inayokupa stress. Unapoamka asubuhi jiambie leo nitaenda kukutana na watu wema na waovu, wale watakaonikosea nitawasamehe kwani hawajui walifanyalo. Ukitanguliza msamaha hata kabla watu hawajakukosea, unaandaa silaha ua kuangamiza stress.
Chagua furaha badala ya huzuni. Furaha ni hisia chanya. Hisia hii inabidi iwe ya kudumu na sio ya matukio. Kinyume cha furaha ni huzuni. Huzuni ni zao linalokujengea stress maishani mwako. Angamiza stress kwa kuchagua kuwa na furaha badala ya huzuni licha ya changamoto unazoweza kukutana nazo. Kwenye kila tukio linalotokea kuna kitu cha kufurahia, na chagua hicho na kuangamiza stress.
Chagua kuwajibika badala ya kulaumu. Kati ya kitu ambacho huwezi kukosa ni mtu wa kumlaumu kwa ajili ya kushindwa kwako. Watu wakikosa kitu fulani hutafuta mtu ambaye anaweza akawa amesababisha matokeo hayo. Watu wakiwatafuta watu wa kuwalaumu hupatikana kirahisi japo wengi hujisahau wao. Ndugu! Mtu wa kwanza kumlaumu au kumlalamikia juu ya kushindwa kwako ni wewe mwenyewe. Hivyo ili kuziyeyusha stress, kuchukua jukumu la maisha yako ili lolote linalotokea utambue kuwa na wewe mhusika. Ukitambua kuwa na wewe ni mhusika, itayeyusha stress zako.
Una silaha ndani yako ya kuchagua nini ukichukue au ukiache ili kuweza kuyeyusha stress zilizokusumbua muda mrefu. Anza kuchagua haya manne hapo juu ili kuishi maisha yenye furaha na mafanikio makubwa.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz