Imani Hizi Nne (4) Ndiyo Zilizokuzuia Usipige Hatua.


Categories :

Sheria ya kwanza ya mwendo ya Newton inasema, hakuna kitu chochote kinachoweza kutokea au kubadilika bila kuweka nguvu kutoka nje. Hii ina maana kuwa hakuna kitu chochote kinachoweza kutokea bila kuchukua hatua. Sababu mojawapo kuu inayokusukuma kuchukua hatua ni imani uliyonayo. Ni imani pia inayokufanya usite kuchukua hatua.

Kuna hatua umeshindwa kuchukua na kukufanya uwepo hapo ulipo leo, ambapo hukustahili kwa sababu ya imani ulizozijenga juu ya maisha yako. Unaamini nini, ndicho kinachoamua ufanye nini. Unafanya nini ndicho kinachoamua unapata nini. Imani hujengwa kwa kusikia, kuona na kuhisi kwa muda mrefu. Mazingira uliyokulia, malezi uliyoyapata, watu waliokuzunguka kwa muda mrefu ndiyo waliokufanya ujenge imani hizo. Kuna imani nne ambazo zimechangia watu wengi kushindwa maishani yaani kuishi maisha ya chini kabisa kuliko vile walivyostahili.

Utajiri ni mbaya. Je unaamini nini juu ya utajiri? Utajiri ni kuwa na utele wa kila kitu maishani mwako. Watu wengi wameangalia utajiri kwenye upande wa fedha na mali. Utajiri wa fedha au mali hutatua changamoto nyingi zinazowakabili watu. Hivyo Yule anayefanikiwa kuwa na utajiri huwa kwenye nafasi nzuri ya kutatua matatizo mengi ya kwake na ya watu wengine. Oh! Kumbe utajiri ni mzuri. Je unaamini kuwa utajiri ni mbaya na matajiri ni watu wabaya. Huwezi kuupata utajiri kama unaamini kuwa ni mbaya. Ili kuanza kuutengeneza na kuupata utajiri huna budi kubadili imani uliyonayo juu ya utajiri. Ukishaamini weka nguvu za kuupata.

Utajiri ni wa watu fulani. Inawezekana unaamini kuwa utajiri ni mzuri lakini wewe umejiweka kando. Mafanikio ni haki ya kila mtu, ikiwemo utajiri. Kila mtu ana haki ya kuwa tajiri, kwa nini una amini kuwa utajiria ni wa watu fulani yaani kabla fulani. Je unaamini kuwa utajiri ni wa watu wa kabila fulani? Rangi ya ngozi fulani? Ukoo fulani? Umri fulani? Au ngazi fulani ya elimu? Mtu yoyote ukiwemo wewe anaweza kuwa tajiri kama ataziishi kanuni za utajiri. Jiambie sana na wewe ni miongoni mwa matajiri kisha anza kanuni za utajiri ambayo kuu ni kutoa thamani kwa watu wengine.

Dunia ina uhaba.  Je na wewe ni miongoni mwa watu wanaoamini kuwa utajiri ulishachukuliwa na watu wengine na wao hawana cha kupata? Huku ni kuamini kuwa dunia ina uhaba na hivyo utajiri waote ulishachukuliwa na watu wachache waliowahi, hivyo wewe huna chako. Dunia ina utele, bado kuna thamani unayoweza kuitoa kwa kiasi kikubwa na watu wakakulipa utajiri. Thamani ni kutatua matatizo yanayowakabili watu. Angalia jamii inayokuzunguka, kuna changamoto nyingi yanayowakabili, weka mipango ya kuitatua ili upate utajiri.

Kuna watu wanaohusika na mafanikio yako. Sababu kubwa ya watu kuwa walalamishi juu ya ugumu wa maisha ni kuamini kuwa kuna watu wanawajibika kwenye mafanikio yao. Wanaamini serikali ndiyo itakayowapa mafanikio, hivyo kama hawayaoni mafanikio wanaanza kuilalamikia serikali. Wengine wanaamini wazazi wao ndiyo wa kuwapa mafanikio, hivyo ikitokea wazazi hawajawawezesha kuwapa elimu kwa mfano, wanaamini wana haki ya kuwa masikini kwa sababu watu hao hawakuwawezesha. Jukumu la kutengeza mafanikio yako ni la kwako mwenyewe. Kama unamtafuta mtu wa kumlaumu kwa ajili ya kushindwa kwako, basi namba moja ni wewe mwenyewe. Chukua jukumu la kutengeneza mafanikio yako kwa asilimia mia moja.

Ndugu! Hizi ni imani nne zilizokuzuia wewe kupiga hatua. Uzuri ni kuwa una uwezo wa kuziyeyusha imani hizi kwa kuanza na kubadili mtazamo na kujenga imani zilizo sahihi. Tangu sasa amini kuwa utajiri ni mzuri, una haki ya kuwa tajiri, kuna utele wa mafanikio ambayo na wewe unaweza kuyapata na kisha chukua jukumu la kutengeneza mafanikio makubwa unayoyataka.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti:  www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *