Hii Ndiyo Mitihani Minne(4) Unayotakiwa Uifaulu Ili Uweze Kupata Mafanikio Yako.


Categories :


Si kwamba walioshindwa hawapendi kuwa na mafanikio makubwa. Si kwamba walioshindwa hawakutengeneza ndoto kubwa kama za kwako. Wala si kwamba hawakuweka malengo na mipango ya kuhakikisha wanapata matokeo. La hasha! Vyote hivyo walivifanya.

Kuna kitu kinachowatofautisha waliofanikiwa na walioshindwa. Kuna kitu kinachowatofautisha wanaopata matokeo makubwa ambayo yanaonekana kuwa miujiza machoni pa watu na wale wanaoishia kupata mafanikio ya kawaida. Kitu hicho ni majaribio ya kukupima kana umejitoa kupata unachokitaka au la. Dunia humpa majaribio kila anayetangaza kuyasaka mafanikio. Utaweza kupata mafanikio makubwa kama utaweza kuifaulu mitihani ifuatayo;


1. Ulipofikiri ndoto kubwa fahamu zako zilikucheka.
Baada ya kutafakari na kupata hamasa ukaona unastahili kuwa na ndoto kubwa na kupata mafanikio makubwa. Ulifanikiwa kutengeneza ndoto yako kubwa. Lakini baada ya muda mfupi nafsi yako ikaanza kukuambia kuwa huwezi kutimiza ndoto hiyo, kuwa ndoto hiyo ni kubwa mno kwako. Pia ulikumbushwa yale uliyoshindwa wakati uliopita. Hili limekuwa jaribio mojawapo linalowapima watu wengi kujua kama kweli wana nia ya kupata kile wanachokitaka. Tambua kuwa baada ya kutengeneza ndoto yako kubwa na kuweka malengo yako makubwa lazima utapimwa kujua kama kweli umejitoa kupata mafanikio hayo. Jitoe kweli ili jaribio hilo likija ulishinde.

2. Watu wa karibu sana watasema huwezi. Siyo nafsi yako pekee itakayokupima kama kweli umejitoa kupata mafanikio uliyoyatarajia bali na watu wanaokuzunguka. Huku ni kukatishwa tamaa. Watu wanaokuzunguka wana mtihani wa kujaribu utayari wako kupata matokeo makubwa unayoyatafuta. Watu wengine wanaweza wakawa wa karibu yako. Jiandae vizuri kujaribiwa na watu wanaokuzunguka kwa kutoamini wanachokuambia, bali sikiliza moyo wako.

3. Vikwazo baada ya kuanza utekelezaji.
Unaweza kushinda mitihani yote miwili hapo juu, juu ya nafsi yako na jirani zako na ukafanikiwa kuanza utekelezaji. Lakini huo hautakuwa mwisho kujaribiwa, majaribu yataendelea hata baada ya hapo. Kuna vikwazo vingi vitaanza kuibuka kukujaribu kama upo tayari na safari hiyo nzito ya kufikia mafanikio. Kwa mfano unaweza kuibiwa mtaji wote baada tu ya kuanzisha biashara yako. Je utakata tamaa na kusema basi hutaendelea na biashara yako. Ushinde mtihani huu kwa kuendelea kwa namna yoyote ile unapoanza kufanyia kazi mipango.

4. Ulipopata mafanikio kidogo ukaridhika. Nini umefanya baada ya kupata mafanikio ya sasa? Je umehisi umeshafika kileleni kiasi cha kujiona huhitaji jitihada zaidi ili kusonga mbele? Je umejaribu kujifananisha na watu wengine na kujiona hakuna mtu mwingine anayeweza kukufikia. Kuja majaribu hata baada ya kupata mafanikio, hata yale makubwa. Utakapojaribiwa na mafanikio uliyopata na kushindwa, una nafasi ya kupoteza mafanikio uliyoyapata kwani kama hukui basi ujue unakufa. Tumia mafanikio uliyoyapata kama ngazi ya kupatia mafanikio.

Hii ndiyo mitihani inayokupasa uifaulu ili kupiga hatua kubwa. Mtihani gani unakusumbua, ambao umekufanya ushindwe kupata mafanikio maishani mwako. Wewe ni mwanafunzi wa maisha yako hakikisha unaifaulu mitihani yako. Dunia haitasita kukupima kama kweli umejitoa kupata mafanikio hayo, jitahidi kuonyesha kweli umejitoa kupata mafanikio unayoyatamani.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *